TUCTA YAWATAKA WAFANYAKAZI KUWAPIMA WAGOMBEA WA NAFASI MBALIMBALI UCHAGUZI MKUU WA OKTOBA MWAKA HUU KUONA KAMA WANA MASLAHI NAO
SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), limewataka wafanyakazi watumie muda wa kutosha kuwapima wale wote wanagombea nafasi mbalimbali za uongozi.Rais wa TUCTA, Omary Juma aliyasema hayo jana katika maadhimisho ya sikukuu ya Mei Mosi, mwaka huu, yaliyofanyika kitaifa kwenye Uwanja wa Uhuru, mkoani Dar es Salaam.
Juma alisema kauli mbiu ya mwaka huu, inayosema “Uchaguzi Mkuu 2010 uwe ufumbuzi wa kero za wafanyakazi” inalenga kuwataka wafanyakazi wote nchini kuwa makini katika kuchagua viongozi wa kuwaongoza.
Alisema wawachague viongozi wanaoonyesha kwa dhati kabisa kuyajua matatizo ya wanayakazi na dhamira ya kweli ya kuyashughulikia.
“Nawasihi wafanyakazi kote nchini kuhakikisha mnajitokeza kwa wingi kupiga kura ya kuchagua viongozi,” alisema
Juma aliwaasi wafanyakazi waachane na ushabiki wa vyama vya siasa, waangalie zaidi sera na uwezo wa viongozi wa vyama vinayotaka kuunda serikali.
Alisema wanataka viongozi watakaowavusha katika kundi la umaskini na kwamba fursa za maendeleo zipo nyingi, watu wapo kinachokosekana ni uongozi bora.
Rais huyo akizungumzia kuhusu mgomo unaotarajiwa kufanyika Mei 5, mwaka huu, nchi nzima, alisisitiza kuwa mgomo utafanyika kama ulivyopangwa.
Alisema mgomo huo unafanyika kisheria kwa kuzingatia taratibu zote kama zilivyoelekezwa kwenye kifungu cha 85 cha sheria ya ajira na uhusiano kazini namba sita ya mwaka 2004 iliyopitishwa na Bunge.
Juma alisema vikao vya TUCTA vya kitaifa vya Kikatiba viliamua na kupitisha uamuzi wa kutumia njia zingine mbadala za kisheria zitakazowawezesha kufanikisha madai yao kutekelezwa.
Alisema shirikisho limeandaa utaratibu wa mgomu huo na kwamba hakuna mfanyakazi yeyote atakayechukuliwa hatua zozote za kisheria na mwajiri yeyote na wala wasiogope vitisho vyovyote vitakavyotolewa.
"Tunawaomba mfuatilie na kusikiliza kwa makini maelekezo tutakayotoa mara kwa mara na mtekeleze kama tutakavyowaelekeza. Msitishwe na vitisho vyovyote kutoka taasisi ama mtu yeyote,”
Aliongeza kuwa: Mgomo huu tumeuandaa kwa kufuata sheria za nchi yetu na tunataka uwe ni mgomo wa amino mpaka hapo madai yetu yatakapotekelezwa,”.
Juma alisema wafanyakazi watambue kuwa haki haiji hivi hivi, haki ni maisha , haki ni uhai na kwa hiyo nin lazima itafutwe na kudaiwa kwa namba na hali yeyote ile.
Alisema wanafahamu katika hatua hiyo ya mgomo, watakuwepo waogo, wanafiki na wasaliti, hao hawapaswi kuwafahamu na kuwatega ili lengo lao liweze kufanikiwa na anaunga mkono mgomo huo.
Juma alisema matajiri na wafanyabiashara wameteka uchumi wa nchi na wamejihusisha na siasa na kujipenyeza katika vyombo vya maamuzi ya kisera yanayohusu uchumi na jamii.
Alisema uchumi wan chi umemilikiwa na matajiri wachache wakiwemo wa ndani na nje ya nchi na kwamba mfumo huo wa siasa umepanua ufa wa kipato kati ya maskini na matajiri.
Mapema akimkaribisha mgeni rasmi, Kaimu Katibu wa TUCTA, Nicholaus Mgaya alisema madai yao ni ya muda mrefu na kwamba wametumia kila aina ya taratibi katika kuyafikisha na kuyawasilisha kwenye vikao halali vya shirikisho.
Alisema madai yao makuu matatu pia limo la muda mrefu la kurekebisha matatizo yaliyomo katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Mgaya alisema wanataka tofauti ya mafao katika mifuko hiyo ziondolewe mara moja, ili kuhakikisha mafao hayo yanamnufaisha mwanachama.
Alisema kuna mifuko ambayo wanachama wake wameneemela jambo linaloleta dhana ya ubaguzi ndani ya jamii ya wafanyakazi na kwamba wanataka kima cha chini cha mshahara sh. 315,000 na usikatwe kodi yoyote.
HABARI KATIKA PICHA
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269