Breaking News

Your Ad Spot

Jul 3, 2010

POLISI AJIUA KWA KUJIPIGA RISASI CHUO CHA POLISI DAR

Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi
POLISI mkufunzi katika Chuo Cha Polisi (Tanzania police Academy), Kurasini Dar es Salaam,  Konstebo Noel Paul Jenga (33), amejiua leo kwa kujipiga risasi moja kichwani akiwa kwenye chumba cha kutunzia silaha kwenye Chuo hicho Jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Tanzania Police Academy SACP Alice Mapunda, amesema kuwa Kostebo Noel Jenga, amejiua majira ya saa moja asubuhi baada ya kupokea zamu ya ulinzi katika kituo kidogo cha Polisi cha Mfano, kilichopo Chuoni hapo.

SACP Mapunda amesema kuwa mara baada ya kupokea zamu ya ulinzi askari huyo aliwaruhusu wenzake waliokesha kwa ulinzi katika kituo hicho kisha kuandika taarifa ya kusudio lake la kujiua kwenye kitabu maalum cha shughuli za zamu maafufu kama OB.

Katika taarifa hiyo, iliyoandikwa saa 12.45 asubuhi, Konstebo Noel Jenga, alisema kuwa ameamua kujiua mwenyewe kwa hiyari yake bila ya kulazimishwa na mtu yoyote na ameomba asisumbuliwe mtu yeyote kutokana na tukio hilo.

Amesema baada ya kuandika taarifa hiyo, Konsetebo Noel Jenga, alianza kuwapigia simu baadhi ya nduguzake kuwaaga buriani na baada ya kumaliza kufanya hivyo alizima simu na kisha kuweka mtutu wa bunduki mdomoni na kujifyatulia risasi ambayo imesababisha kifo chake.

Marehemu Noeli alizaliwa Desemba 25, 1977 huko mjini Morogoro na baadaye kupata elimu ya msingi katika sule moja mjini Morogoro tangu mwaka 1986 hadi 1992 na kujiunga na masomo ya Sekonda kwenye Shule ya Sekondari ya Center mjini Dodoma kati Ya mwaka 1993 na 1996 kabla ya kujiunga na kidato cha tano na cha sita katika shule ya Sekondari ya Forest mjini Morogoro kati ya mwaka 1998 na 2000.

Alijiunga na Jeshi la Polisi katika Chuo cha polisi cha Kimataifa cha CCP cha Mjini Moshi mkoani Kilimanjaro mnamo Septemba 25, 2000 na kuhitimu mafunzo ya awali ya uaskari Polisi Mei 25, 2001.

Mara baada ya kumaliza mafunzo hayo alipangiwa mkoa wa Iringa ambapo alipelekwa katika kituo cha Polisi Ludewa kabla ya kuhamishiwa CCP Moshi mkoani kama Mkufunzi mwaka 2006 na kutokana na juhudi yake ya ukufunzi alihamishiwa katika Chuo Kikuu cha Polisi Jijini Dar es Saam ambacho sasa ni Tanzania Police Academy.

Kamanda Mapunda amesema kuwa Polisi wameanza uchunguzi wa chanzo cha kifo cha marehemu na kwamba mipango ya kusafirisha mwili wa marehemu kwenda kwao Morogoro inafanywa.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages