Breaking News

Your Ad Spot

Jun 2, 2011

NAPE AWASHUKIA WATEDAJI WABOVU SERIKALINI

Nape akikagua ujenzi wa zahanati ya Majimoto
NA MWANDISHI WETU,MPANDA
KATIBU wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye amewashukia watendaji wa serikali wenye tabia ya kukaa ofisini badala ya kwenda kusimamia miradi ya maendeleo na hivyo kuigombanisha CCM na wananchi kwa miradi hiyo kutokamilika kwa wakati na kutokuwa na thamani ya fedha iliyokusudiwa.
Nape ametoa kauli hiyo leo kwenye mkutano wa hadahara uliofanyika kwenye kata ya Majimoto, wilaya ya Mpanda mkoani Rukwa baada ya kukagua miradi kadhaa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM na kukuta miradi hiyo haijasimamiwa ipasavyo.

Nape aliwashukia watendaji baada ya yeye na ujumbe wake kuamua kukagua ghafla miradimbalimbali ukiwemo ujenzi wa kituo cha afya kinachotegemewa kutoa huduma kwa wananchi wa Kata ya Majimoto wilayani Mpanda baada ya kushtukia taarifa aliyopewa kuhusu ujenzi huo.

Baada ya kufika kwenye eneo la ujenzi alishangaa kuona kwamba kituo hicho ambacho ujenzi wake utagharibu sh. milioni 60 ukikamilika, unafanyika kwa ubabaishaji, ambapo kwanza imepotezwa nguvu kazi kwa kuchimbwa msingi katika eneo la kwanza na kuachwa msingi huo baada ya kuona kwamba majengo yatakuwa karibu na barabara.

Mbali na kupoteza ghara za kuchimba msingi na kuuacha na kisha kwenda kuhimba eneo lingine, lakini eneo ulikohamishiwa ujenzi huo pia hapafai kwa kuwa ni eneo linalotuamisha maji na kibaya zaidi ujenzi huo umewekwa mbali na makazi ya wanakijiji.

Kufuatia kasoro hizo, Nape alitaka kujua ikiwa ujenzi wa Zahanati hiyo umesimamia na Mhandisi wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda, akaambiwa kwamba mhandisi huyo hakuwahi kufika hata siku moja isipokuwa aliagiza ujenzi uendelee.

"Baada ya fedha kupatikana kutoka Halmashauri ya Wilaya, tumewasiliana na Mhandisi wa halmashauri yetu, akasema tuendelee tu, lakini hajawahi kuja", Alisema  Ofisa Mtendaji wa Kata ya Maji Moto, Julius Milambo.

Kufuatia hali hiyo, Nape aliagiza ujenzi usimamishwe na eneo la kujengwa zahanati hiyo libadilishwe ili kuwa karibu na makazi ya wananchi, ili kuweza kuwapatia huduma karibu itakapokamilika.

"Inaonekana kuna utamaduni unaimarika wa watendaji katika halmashauri nchini kuvaa suti na kukaa ofisini badala ya kwenda kusimamia kazi za maendeleo, matokeo yake miradi inajengwa bila utaalamu na chini ya kiwango. CCM iliyojivua gamba haiwezi kuvumilia uzembe huu kwasababu ni usaliti kwa CCM na wananchi, lazima wawajibike" alisema Nape.

"Wataalamu hawa wanalipwa mishahara kwa fedha za walipa kodi wakitarajiwa watumie utaalamu wao kuwahudumia wananchi, wanapofanya kinyume ni usaliti ambao hauwezi kuvumiliwa", alisema Nape.

 Akitolea mfano alisema ipo miradi mingi fedha hazitoi matokeo yaliyokusudiwa na nyingi huibiwa na miradi kuwa chini ya kiwango kwa sababu wataalamu wanakaa maofisini kupiga soga.

" Watendaji wengi wa namna hii wanaigombanisha CCM na wananchi kwa matendo yao halafu wakati ukifika inaulizwa CCM sio wao, kabla wananchi hawajatubana lazima sisi tuwabane hawa." alisema Nape.

Pamoja na mradi huo wa zahanati Nape pia alipewa taarifa ya ujenzi wa kituo cha polisi ambapo ilidaiwa mtendaji wa kijiji, mwenyekiti wake na mtendaji wa kata walichakachua fedha za ujenzi wa kituo hicho na kusababisha kisimalizike hadi sasa tangu mwaka juzi.

Nape aliambiwa katika sakata hilo, viongozi wa kijiji walijiuzulu lakini mtendaji wa kata,Thomas Senga, alihamishiwa kata nyingine ya Mwamakuli bila kuchukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Kata ya majimoto, Nape aliagiza viongozi hao washughulikiwe kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi kwa upande wa mtendaji aliyehamishwa kituo kingine, na wote wafikishwe katika vyombo vya sheria.

Nape alishutumu utaratibu wa watendaji kuhamishiwa eneo lingine baada ya kufanya kosa alikokuwa na kusema utaratibu huo ni mbovu na haustahili kuendekezwa katika CCM iliyojivua gamba.

"Utaratibu huu nao mbovu mtendaji anakosea mahali anahamishiwa eneo jingine bila kuchukuliwa hatua, huu ni kuhujumu juhudi za serikali kuleta maendeleo, msiendelee na utaratibu huu" Alisisitiza.

Katika tuhuma hizo, viongozi wanadaiwa kuyeyusha sh. milioni 5, zikiwemo sh. 200,000, zilizotolewa na Mbunge wa eneo hilo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na kufuatia kushindwa kukamilika kituo hicho, Wananchi wamelazimika kukodi jengo kwa ajili ya kituo cha polisi.

Jengo hilo la kukodi limegeuka kero kwa wananchi kutokana na kulazimika kuchangia ulipaji kodi ya kila mwezi ambapo hadi sasa wanadaiwa zaidi ya sh. milioni moja.

Akizungumzia deni hilo, Nape aliagiza fedha hizo, na kodi zinazoendelea za pango la kituo hicho, zilipwe na halmashauri yenyewe ilizyozembea kkujenga kituo, badala ya kuwachangisha wananchi kwa kuwa jukumu jukumu la ulinzi na usalama wa raia na mali zao ni la serikali.

Ili kuonyesha mfano CCM katika deni hilo la pango la kituo cha polisi wamechangia sh. 500,000o kama njia ya kuonyesha uongozi kwa mfano na kuitaka serikali ya CCM kujihadhari wa watendaji wanaofanya vibaya nahivyo kuitukanisha serikali na kusababisha wananchi kuichukia CCM.

Nape na ujumbe wake wanaendelea na ziara yao mkoani Rukwa na kesho ambapo  watafanya mkutano mkubwa mjini Mpanda.

1 comment:

  1. Erick Mapunda6/2/11, 8:42 PM

    Kama Halmashauri Kuu CCM wilaya zingeshiriki kikamilifu kusimamia utekelezaji wa ilani ya chama chetu CCM, kusingekuwa na uzembe wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo unaofanywa sasa na halmashauri zetu.

    Haiwezekani tusubiri kiongozi ngazi ya Taifa aje aseme kuwa eneo hili ni la ardhi oevu (marshland)halifai kwa kujengwa, au eneo hili halina walengwa wa mradi husika hivi halifai kuwa eneo la mradi (proper site selection)wakati tuna wataalamu katika halmashauri zetu tuliowasomesha kwa pesa za walipa kodi ("... tena mpaka ulaya..." JK) na kumaliza vidato vyote vya elimu halafu hawawajibiki.

    Je kama huyo kiongozi wa CCM Taifa hana jicho hilo la utaalamu (ilivyo kwa viongozi wetu wengi)kuona mapungufu yaliyopo, mwisho wake utakuwa nini?

    Kwa kuwa serikali hii ni ya CCM, viongozi wetu wa kata katika kila wilaya washiriki kikamilifu katika utendaji wa kila siku wa halmashauri za wilaya badala ya kusubiri uwakilishi wa makatibu na wenyeviti wa wilaya katika vikao vya baraza la madiwani kwani hicho si chombo cha utendaji cha halmashauri.

    Miradi inatekelezwa kwenye kata na matawi, kwa nini viongozi wa CCM katika maeneo hayo wasishiriki katika upangaji na usimamizi wa miradi hiyo katika maeneo yao?

    Sisemi sasa nao wawe katika budget za halmashauri zetu za wilaya, bali CCM ina wajibu wa kuwezesha viongozi wetu kushiriki katika zoezi hili ili hatimaye iweze kuwabana watendaji wabovu katika halmashauri tena kwa vielelezo kamili bila hiyana wala majungu.

    Ikifikia hatua hiyo, CCM haitahitaji tingatinga (mzee malechela) toka eneo moja kwenda kuomba kura kwa wanachi walio eneo jingine, kwani utendaji wetu utajiuza wenyewe kwa wananchi.

    Erick Mapunda

    ReplyDelete

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages