Rais wa Baraza Kuu la 65 la Umoja wa Mataifa, Bw. Joseph Deiss akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dkt. Asha-Rose Migiro kufungua majadiliano kuhusu Maendeleo. Mkazo ukiwa katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia ( MDGs) hususani lengo namba 4 na 5 yanayohusu afya ya mama na mtoto. katika mazungumzo yake, Naibu Katibu Mkuu pamoja na mambo mengine, ameyahimiza mataifa kuwekeza katika huduma za afya hasa kwa mama na mtoto kwakuwa kuna manufaa makubwa na ni chachu katika kunasukuma mbele ajenda za maendeleo.
-----------------------------------------------------------------------------
Na Mwandishi Maalum,New York
Imeelezwa kuwa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete imekuwa nchi ya kupigiwa mfano , katika utoaji na uboreshaji wa huduma ya afya kwa mama na mtoto.
Ni kutokana na juhudi hizo, Tanzania imetajwa kama mdau muhimu katika utekelezaji wa Mkakati wa Kimataifa kuhusu afya ya mama na mtoto.
Hayo yameelezwa na Bw. Joseph Deiss, Rais wa Baraza Kuu la 65 la Umoja wa Mataifa, wakati alipokuwa akimkaribisha Mhe. Juma Duni Haji, Waziri wa Afya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kuzungumza katika mjadala kuhusu Maendeleo uliofanyika siku ya jumanne Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
Mhe. Juma Duni Haji alikuwa miongoni wa jopo la wazungumzaji waliojadili utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia na Uwajibikaji, hususani utekelezaji malengo namba 4 na 5 yanayohusu afya ya mama na mtoto.
Majadiliano hayo yalifunguliwana Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Dkt. Asha-Rose Migiro.
“ Tanzania ni mdau muhimu sana katika utekelezaji wa Mkakati wa Kimataifa kuhusu Afya ya Mama na Mtoto. Rais wake ni Mwenyekiti mwenza wa kamisheni ya habari na uwajibikaji katika masuala yanayohusu afya ya mama na mtoto. Tanzania inapiga hatua kubwa na nzuri na umejiwekea malengo na mikakati mbalimbali katika eneo hilo” akasema Bw. Deiss.
Akasema kuwa Tanzania imefanya vizuri katika usambazaji wa huduma za afya, utoaji wa chanjo za kuzuia maradhi mbalimbali kwa wanawake wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.
Aidha ameongeza kuwa Tanzania , imejitahidi sana kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano, na inatoa huduma za kinga ya maambukizi ya virusi vinavyosababisha ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto huku ikiendelea na jitihada za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
Mbali ya Mhe. Juma Duni Haji wengine waliokuwa kwenye jopo hilo la mzunguko wa kwanza katika majadiliano hayo ni pamoja na Mhe. Gilles Richard, Naibu Balozi wa Canada katika Umoja wa Mataifa, Bw. Babatunde Osotimehin, Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA. Bi Donna J. Hrinak, Makamu wa Rais kuhusu sera na masuala ya serikali (PepsiCo) na Ms. Nyaradzayi Gumbonzvanda, Katibu Mkuu , World YWCA.
Akichangia majadiliano hayo, Waziri wa Afya Juma Duni Haji, alisema anajisikia fahari kubwa kutamka kwamba Tanzania ilikuwa katika mwelekeo sahihi wa kufikia utekelezaji wa baadhi ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia ( MDGs).
Waziri aliwaeleza washiriki wa majadiliano hayo, hatua mbambali ambazo serikali ya Muungano na ile ya Zanzibar, zimetekeleza wa malengo namba 4 na tano katika utoaji wa huduma za afya ya mama na mtoto, ingawa bado kuna changamoto kadhaa.
Kwa mfano alieleza kuwa hivi sasa huduma za afya zimesogezwa karibu zaidi na wananchi ili kuwapunguzia wananchi na hasa wanawake mwendo mrefu wa kufuata huduma hizo.
Akasisitiza kuwa chanjo za magonjwa mbalimbali zimekuwa zikitolewa kwa wakati na kwa gharama nafuu, huku akielezea kuwa matumizi ya vyandarua vyenye viatilifu kumesaidia sana kupunguza siyo tu vifo vinavyosababishwa na malaria, bali kumetokomeza kabisa ugonjwa huo Zanzibar.
Aidha amesema kumekuwa na ongezeko la ajira kwa wataalamu wa masuala ya afya. Huku akisema ndoa za umri mdogo hasa kwa Tanzania Visiwani bado ni tatizo
Awali akifungua majadiliano hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dkt. Asha-Rose Migiro amerejea tena wito wake wakuzitaka serikali kuwekeza zaidi katika huduma za afya na mama na mtoto.
Akasema uwekezaji katika afya ya mama na mtoto unalipa, kwa sababu mama akiwa na afya nzuri atazaa mtoto mwenye afya nzuri na ambaye hatimaye atakuja kuwa kiongozi mzuri.
Akasema kuwa katika dunia ambayo hivi sasa inakabiliwa na changamoto nyingi, ni rahisi sana kwa baadhi ya makundi ya watu na hasa wale wanaoishi katika mazingira magumu kusahauliwa
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269