ZANZIBAR, Tanzania
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imejikita katika kuona mazingira ya uwekezaji sambamba na Vitega Uchumi vya wawekezaji
vinalindwa ili viendelee kusaidia pato la Serikali pamoja na kutoa ajira kwa
wananchi wanayovizunguuka vitega uchumivya wawekezaji hao.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipotembelea Hoteli ya Paradise
Beach Resort iliyopo Marumbi Wilaya ya
Kati ambayo imeungua kabisa kwa moto siku mbili zilizopita.
Balozi Seif alisema Serikali imekuwa
ikisisitiza na kuweka mikakati ya miundo
mbinu katika eneo la uwekezaji hasa kwenye sekta ya Utalii kwa lengo la
kuimarisha nguvu za kiuchumi na kupunguza umaskini miongoni mwa wananchi walio wengi
nchini.
Akiupa pole Uongozi na wafanyakazi wa Hoteli hiyo ya Paradise
Beach Resort kutokana na hasara iliyowapata kufuatia kukumbwa na moto huo
Balozi Seif lakini pia akaupongeza Uongozi huo kwa uamuzi wake makini wa kufikiria
kuiwekea Bima Hoteli hiyo.
Alisema ipo miradi mingi ya uwekezaji
inayoanzishwa katika maeneo mengi Nchini na hushindwa kuendelea wakati inapopatwa na majanga kama ya moto kwa kukosa
kuiwekea Bima ya ajali.
Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar alizikumbusha Taasisi na mashirika ya uwekezaji kuzingatia ubora wa
miradi wanayoanzisha ili iweze kutoa tija kubwa zaidi.
Mapema Mkurugenzi wa Hoteli hiyo ya
Paradise Beach Resort Bwana Egbaert Schoonvelde alimueleza Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar kwamba uchunguzi wa
chanzo cha moto huo umeanza kuchukuliwa na Taasisi ya Bima ili kuendelea na
hatua nyengine ya fidia.
Bwana Egbaert alimuhakikishia Balozi
Seif kwamba licha ya hasara iliyopatikana kutokana na moto huo lakini Uongozi
wa Hoteli yake bado una nia ya kuendelea kuwekeza katika masuala ya Utalii hapa
Zanzibar.
Alisema Zanzibar imebarikiwa kuwa na
mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta ya utalii hali iliyoufanya uongozi
wa hoteli hiyo kushawishika kuwekeza
hoteli ya Kitalii hapa Nchini.
Mkurugenzi huyo wa Paradise Beach
Resort alifahamisha kwamba wateja wao wengi ambao wanatokea Nchini Uholanzi
wanapendelea kutembelea visiwa vya Zanzibar ili kuona mandhari yake yenye fukwe
za kuvutia.
“ licha ya baadhi ya watu
kutulalamikia katika matumizi ya makuti kwenye uwekezaji wa majengo yetu lakini
tunafanya hivyo ili kutoa fursa ya kuimarisha utamaduni wa Zanzibar katika
matumizi ya Makuti kwenye uwekezaji.
Utaratibu huu hata wageni wetu wamekuwa
wakiufurahia mno “. Alifafanua Mkurugenzi huyo wa Hoteli ya Paradise Beach
Resort Bwana Egbaert.
Naye Meneja Mkuu wa Paradise Beach Resort Ali Mgeni Mjombo alisema moto huo ambao
hadi sasa chanzo chake kimekuwa na utata umeanzia katika eneo la mapumziko
liliopo ufukweni mwa Hoteli hiyo (Jet) majira ya saa 10.00 za jioni.
Ali Mgeni alisema moto huo uliopata
kasi kutokana na upepo mkubwa uliokuwa ukivuma katika eneo hilo umesababisha
kuungua kwa karibu majengo yote ya Hoteli hiyo ikiwemo minazi pamoja na miti iliyopo pembezoni mwa bara bara
karibu na hoteli hiyo.
Alieleza kwamba Wafanyakazi na
Viongozi wa Hoteli hiyo walilazimika kufanya kazi ya ziada katika kusaidia
kuokoa maisha na mali za wageni waliokuwa wamepanga kwenye hoteli hiyo.
Hata hivyo Meneja Mkuu huyo wa
Paradise Beach Resort alionyesha kusikitishwa kwake na baadhi ya watu waliofika kusaidia uokozi huo
ambao hawakuonyesha uaminifu kwa tabia yao mbaya ya kudokoa vitu na mali za
wageni wao.
Hadi sasa bado haijajuilikana
hasara halisi iliyotokana na moto
uliounguza Hoteli hiyo ya Paradise Beach Resort ya Marumbi ambayo imekuwa
ikitoa huduma za wageni ambao wengi kati yao hutokea Nchini Uholanzi.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269