Breaking News

Your Ad Spot

Feb 2, 2014

RAIS JAKAYA KIKWETE AGUSWA NA UTENDAJI WA KINANA, ATAKA AWE MFANO WA KUIGWA

Kikwete akihutubia leo mjini Mbeya. Kushoto ni Kinana na Mzee Mangula
NA BASHIR NKOROMO, MBEYA
MWENYEKITI wa CCM, Rais Jakaya Kikwete leo amevunja ukimya na kuzungumzia suala la mawaziri waliotuhumiwa na wananchi kuwa mizigo wakati wa ziara za Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na baadhi ya wajumbe wa sekretarieti katika mikoa kadhaa nchini mwishoni mwa mwaka jana.
 
"Najua wapo baadhi ya watanzania, walitaka Mawaziri waliotajwa kuwa ni mizigo wafukuzwe kazi, na kwa vile halikufanyika basi suala hilo limegeuzwa kuwa la malumbano,  ni vyema ieleweke kuwa kuitwa kwa Mawaziri hao na Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hakuna maana ya kuishia kufukuzwa", alisema, Kikwete leo akihutubia maelfu ya watu katika sherehe za kilele cha miaka 37 ya CCM, kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya. 

Alisema Mawaziri hao waliitwa kwa sababu ya kuwepo matatizo yaliyoonekana yanatakiwa yapatiwe ufumbuzi, matatizo hayo yamezungumzwa na maelekezo kutolewa kuhusu cha kufanya.

"Kamati Kuu ya CCM imetimiza wajibu wake uliobaki ni wa serikali.Kamati Kuu itaendelea kufuatilia na kama hakuna maendeleo ndipo inapoweza kuamua kuomba mamlaka ya uteuzi ichukue hatua zipasazo dhidi ya mhusika.Huko hatujafika" alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete alimpongeza Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, akisema, ziara ambazo amekuwa akifanya ni mfano unaopaswa kuigwa na viongozi wengine hasa wa CCM kwa sababu ndio hasa unaotakiwa.

Alisema ziara za Kinana zinakijenga Chama na kutoa taswira nzuri ya CCM katika jamii kwani zinahuisha uhai wa CCM kwa kuwa Katibu Mkuu huyo katika ziara hizo huenda hadi kwa wanachama waliopo ngazi za chini.

"Katibu Mkuu Kinana amekuwa anafanya mambo ambayo baadhi ya watu wanadhani kuwa ni mageni, lakini katika kufanya hayo amekuwa pia akionyesha umahiri na ujasiri mkubwa kwa kwenda  maeneo ambayo ni magumu kufikika" alisema Rais Kikwete na kuongeza;

"Katika ziara hizo  wakati mwingine amekuwa anatumia njia za usafiri zinazoogopesha, amewahi kutumia meli  ya MV Songea kutoka mkoani Ruvuma hadi Mbeya, amepanda milima na mabonde kwa magari katika maeneo ambayo ni hatari, lakini lengo likiwa ni kuhakikisha anawafikia wanachama wa ngazi za chini kabisa".

Rais Kikwete alisema mambo mengine yalivyomvutia katika ziara za Kinana, ni hatua ya Katibu mkuu huyo kwenda kukaa na  kula na wananchi katika ngazi za chini na kisha kufanya nao kazi za maendeleo  na zaidi kutoa fursa kwa wananchi kueleza matatizo na manung'uniko yanayowasibu.

Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa alisema Katibu mkuu wa Chama amekuwa anashiriki katika kutafuta majawabu na matatizo anayoambiwa hali ambayo imesaidia sana kumaliza baadhi ya matatizo kulekule mikoani.

"Pale ambapo pamekuwa panahitaji hatua zaidi za serikali hakusita kutoa taarifa kwa Waziri Mkuu, vile vile amekuwa anatoa taarifa ya ziara zake kwenye Kamati Kuu ya CCM" alisema Rais Kikwete.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages