Na Mwandishi Maalum, New York
Tanzania kupitia Uwakilishi wake wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa, imeshiriki kikamilifu katika vikao vya kawaida vya Bodi Tendaji ya Mashirika na Mifuko inayosimamia Maendeleo ya Umoja wa Mataifa.
Tanzania imeingia katika Ujumbe wa Bodi Tendaji ya UNDP (United Nations Development Program), UNFPA ( United Nations Population Fund ) na UNOPS ( United Nations for Project Services) kwa kipindi cha mwaka 2014- 2016.
Licha ya kuwa mjumbe, Tanzania pia ni Makamu Rais wa Bodi nafasi inayoifanya Tanzania kuziwakilisha za Afrika na kupitia umakamu huo wa Rais, Tanzania inakuwa pia mjumbe wa Ofisi ya mtedaji wa Bodi(Bureau) yenye jukumu la kuratibu na kusimamia shughuli za vikao vya Bodi.
Bodi Tendaji ya UNDP, UNFPA na UNOPS yenye wajumbe 36 iliundwa kwa mujibu wa Azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la mwaka 1993.
Mgawanyo wa wajumbe hao ni kama ifuatavyo, wajumbe 8 hutoka mataifa ya Afrika, wajumbe 7 hutoka mataifa ya Asia na Pacific, wajumbe 5 ni kutoka Amerika ya Kati na Visiwa vya Karibiani, wajumbe 4 hutoka mataifa ya Ulaya Mashariki na wajumbe 12 kutoka Mataifa ya Ulaya Magharibi na Mataifa mengine.
Kwa mujibu wa kanuni zinazosimamia utendaji kazi wa Bodi, wajumbe wake huhudumu kwa mzunguko wa kupokeza .
Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania ukiongozwa na Kaimu Muwakilishi , Bi. Maura Mwingira, na kwa kushirikiana na Maafisa wa Uwakilishi, umeshiriki kikamilifu katika vikao hivyo kwa kuogoza baadhi ya majadiliano na kuchangia mijadala.
Ujumbe wa Tanzania katika Vikao hivyo vilivyodimu kwa wiki moja, ulitumia ushiriki wake kusimamia na kutetea maslahi ya Tanzania. Na katika nafasi yake ya Makamu Rais kutetea maslahi ya Afrika.
Miongoni mwa masuala yaliyotiliwa mkazo na Tanzania katika michango yake ni pamoja na kusisitiza fursa na nafasi ya nchi zinazoendelea kuanisha, kuibua na kumiliki miradi ya maendeleo kwa kuzingatia vipaumbele ambavyo nchi yenyewe imejiwekea.
Tanzania pia ilitambua mchango wa Mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa, katika usimamizi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo na miradi mbalimbai ikiwamo ile inayosimamia na kutetea fursa sawa za kijinsia hususani kwa wanawake na watoto wa kike.
Yakiwamo pia masuala ya kilimo, lishe, elimu na afya, vita dhidi ya umaskini na maendeleo shirikishi.
Ikizungumza kwa kwa niaba ya nchi za Afrika, Tanzania pamoja na masuala mengine, imetoa wito kwa washirika wa maendeleo kuongeza michango yao katika Mfuko wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNCDF).
Mfuko huu wa Maendeleo ( United Nations Capital Development Fund) unatoa mchango mkubwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa nchi zinazoendelea na Tanzania ni mmoja wa wanufaika wa mfuko huo.
Tanzania imebainisha katika vikao hivyo kuwa licha ya kazi nzuri iniayofanywa na UNCDF), bajeti ya Mfuko huo imeendelea kupungua ikilinganishwa na mahitaji yaliyopo. Ni kwa sababu hiyo imeomba wadau wa maendeleo hususani wale wenye uwezo na nia kuangalia uwezekano wa kutunisha Bajeti ya mfuko kutoka bajeti ya sasa ya dola za kimarekani 16 milioni angalau ifikie dola milioni 25.
Bodi Tendaji ya Mashirika na Mifuko ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa, (UNDP, UNFPA na UNOPS) imekamilisha vikao vyake vya kawaida kwa wajumbe wa Bodi kupitisha maazimio na mapendekezo mbalimbali.
Vikao vya Bodi, ambavyo vilifunguliwa na Bi. Helen Clark Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa, ( UNDP) ambaye aliainisha na kuelezea mafanikio na changamoto za utekelezaji wa taasisi hizo kwa mwaka uliopita.
Katika ufunguzi wake, Mkuu huyo wa UNDP pamoja na kuelezea shughuli za taasisi hizo pia alielezea ushiriki wa UNDP katika utoaji wa misaada ya kibinadamu katika nchi ambazo zimekubwa na machafuko kama vile Sudan ya Kusini, Syria na Afrika ya Kati.
Aidha alitoa taarifa ya kuanza kwa utekelezaji wa Mpango Mkakati mpya wa UNDP utakaotekelezwa kwa kipindi cha 2014-2017.
Kwa mujibu wa Bi. Clark, mpango mkakati huo mpya unalenga pamoja na mambo mengine, katika kuratibu na kuboresha utendaji kazi wa taasisi hiyo , pamoja na kuleta uwiano, usimamizi na matumizi bora na yenye tija ya raslimali zake ikiwamo raslimali watu.
Pamoja na Mtendaji Mkuu wa UNDP kuanisha shughuli zake, Wakuu wa UNFPA, UNOPS , UN- Women na UNICEF nao waliwasilisha taarifa za Taasisi zao na kujadiliwa na wajumbe.
Wajumbe wa Bodi walipata fursa pia ya kupitia na kujadili nafasi na mchango wa Taasisi hizo kuelekea ukingoni mwa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia ( MDGs) na wajibu wa taasisi hizo katika maandalizi ya malengo mapya ya maendeleo endelevu baada ya 2015 (SDGs).
Vile vile wajumbe wa Bodi walipokea taarifa za utendaji na vipaumbele vya taasisi hizo, ikiwa ni pamoja na bajeti zao na mapendekezo yaliyotolewa na wakaguzi wa Bodi.
Baadhi ya Maafisa wa Uwakilishi wa Kudumu, Bw. Noel Kaganda na Bi.
Ellen Maduhu wakifuatilia moja ya vikao vya Bodi ambapo Tanzania
ilishiriki.
Wajumbe wakifuatilia majadiliano
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269