Mratibu wa Mradi wa Ukimwi ILO, Getrude Sima (kushoto) akitoa maelezo ya kikundi cha kina mama ambao ni walengwa wa mradi wa Ukimwi unaofadhiliwa na SIDA chini ya shirika la kazi duniani (ILO), kwa Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez, katika ziara ya kikazi ya kutembelea miradi inayosaidiwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa mkoani Iringa na Njombe. Kulia ni Practice Specialist HIV/AIDS, Dr Bwijo Bwijo.
Na Mwandishi wetu, Iringa
KIKUNDI cha wafinyanzi wanawake cha Lungemba,kilichopo Wilaya ya Iringa, wameomba kusaidiwa vifaa vya kisasa vya ufinyanzi, ili waweze kutengeneza vitu bora vitakavyokubalika katika soko.
Maombi hayo wameyatoa katika risala yao kwa Mratibu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini na Mkurugenzi mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP, Alvaro Rodriguez.
Mratibu huyo alikuwa katika ziara ya kikazi ya kutembelea miradi inayosaidiwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa mkoani Iringa na Njombe.
Makundi yaliyotembelea ni yale ya ujasiriamali, yanayosimamiwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) chini ya mpango wa Kupunguza Maambukizi ya UKIMWI kwa Njia ya Uwezeshaji wa Kiuchumi kwa Wafanyakazi walio katika Sekta Isiyo Rasmi kando kando mwa Barabara Kuu iendayo Tanzania-Zambia maarufu kama “Corridor Economic Empowerment Project (CEEP)"
Aidha makundi mengine yaliyotembelewa ni ya wakulima wanaosaidiwa pembejeo na wanaotengeneza vikapu na kufanya shughuli binafsi ikiwamo mabucha.
Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akiwa amembeba mtoto wa mwanachama wa Mtwango SACCOS ya wilaya ya Njombe.
Mmoja wa wanachama hao Anna Nyongole alisema wanafanya kazi hiyo katika mazingira magumu, kwani bado wanatumia mikono pekee, badala ya kutumia vifaa vya kisasa, na hivyo kusababisha bidhaa zao kukosa ushindani katika soko jambo linalowadumaza kiuchumi.
“Tunatengeneza vyungu, sufuria, majiko, mitungi ya maji na ya maua, na vitu mbalimbali, lakini changamoto yetu kubwa ni namna tunavyotengeneza, kwani hatuna mashine za kutengenezea vitu hivyo wala mitambo ya kuchomea, tunaiomba serikali na wadau wa maendeleo nchini watusaidie, kwani tukipata vifaa vya kisasa tutaweza kutengeneza vitu vingi kwa muda mchache kuliko ilivyo sasa,” alisema Nyongole.
Naye Zena Omary amesema kukosekana kwa usafiri wa gari kwenda kusomba udongo wa kufanyia ufinyanzi kunawafanya kutembea umbali wa kilomita 40 kwenda na kurudi, kutoka katika eneo la Ikekeke katika kijiji cha Kitelewasi.
Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez katika picha ya pamoja na Wanchama wa Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo kinachofadhiliwa na SIDA chini ya Shirika la kazi Duniani (ILO).
“Tunakokwenda kuchimba udongo ni Ikekeke katika kijiji cha Kitelewasi, tunatembea kilomita 20 kwenda na kurudi kilomita 20, kwa hiyo unajikuta siku moja umeshindia kuchimba udongo na kusomba tu, na kwa kuwa tunajitwisha kichwani, huwezi kuchukua udongo mwingi,” alisema Zena.
Licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali, akinamama hao wamesema kupitia mafunzo ya UKIMWI na Ujasiriamali waliyopata kutoka ILO wameweza kuboresha biashara hiyo ya ufinyanzi kwa kujenga banda la kuhifadhia bidhaa hizo, kuweka akiba na kukopeshana katika kikundi hatimaye wamefanikiwa kuyabadili maisha yao kwa kujenga nyumba bora na hata kuwasomesha watoto wao kwa kumudu gharama za ada.
“Hapa kila mmoja wetu anayo nyumba ya kisasa ya tofali za kuchomwa na iliyoezekwa kwa bati, na pia tumefanikiwa kusogeza huduma ya maji ya bomba katika nyumba zetu, ili kupunguza usumbufu wa kuchota maji visimani... kwa kweli biashara hii ya ufinyanzi imetusaidia lakini tukiboreshewa zaidi mazingira tutakua zaidi kiuchumi,” Walisema.
Msafara wa Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, Alvaro Rodriguez ukiongozwa na Mratibu wa Mradi wa Ukimwi ILO, Getrude Sima (kushoto) kuelekea kukagua baadhi ya miradi inayofadhiliwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa wilayani Njombe.
Hata hivyo Umoja wa Mataifa UN kupitia Shirika la Kazi Duniani “ILO” Kwa mkoa wa Iringa pekee- limefanikiwa kuwafikia akinamama na vijana wapatao 1,000 wa vikundi mbalimbali vya kiuchumi na vyama vya Kuweka na Kukopa (SACCOS), huku wanachama wa vikundi hivyo wakipatiwa mikopo, Elimu ya Maambukizi Virusi vya UKIMWI, pamoja na mafunzo ya Ujasiriamali.
Mratibu huyo alitembelea vikundi hivyo kuona namna msaada wa Umoja wa Mataifa ulivyobadili maisha ya wahusika ambao walikuwa katika mazingira magumu hapo awali.
Makundi mengine yaliyotembelewa yapo Nyololo na pia hospitali ya Mafinga ambako kuna mafunzo yanayoendeshwa kwa ajili ya ushauri nasaha kwa wanawake wenye kuishi na VVU.
Miradi hiyo ambayo mashirika ya UNICEF na IFAD yanashiriki, imelenga kusaidia makundi hata yale yenye wanachama wanaoishi na virusi vya ukimwi kujitambua na kuishi kwa kujitegemea.
Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez kwenye picha ya pamoja na kikundi cha kinamama wa Nyololo wanaotengeneza vikapu.
Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akicheza na baadhi ya watoto yatima wa kituo cha Nyololo Centre ambao wengine wakiwa ni ndugu wa wakinamama wanaosaidiwa na ILO.
Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akikagua shamba la Mradi wa miche na matunda ambalo linasimamiwa na wanawake wa kikundi cha Nyololo wanaofadhiliwa SIDA chini ya shirika la kazi duniani (ILO).
Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akishiriki kupanda mti kwenye shamba hilo kama kumbukumbu wakati wa ziara yake ya kutembelea miradi inayosaidiwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa mkoani Iringa na Njombe.
Katibu wa Kikundi cha wafinyanzi wanawake cha Lungemba, Bi. Leokadius Mfukwe akisoma risala ya kikundi chao na changamoto zinazowakabili mbele ya Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (mwenye miwani) alipokuwa katika ziara ya kikazi ya kutembelea miradi inayosaidiwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa mkoani Iringa na Njombe.
Baadhi ya vyungu vinavyotengenezwa na kikundi hicho.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269