Redds Miss Kanda ya Kati 2014/15, Doris Mollel akiongea Maneno machache wakati akikabidi mashine mbili za kupumulia kwa watoto waliozaliwa kabla ya muda wa kawaida zenye thamani ya Tsh millioni 1.2 kwenye wodi ya watoto njiti ya hospitali ya mkoa wa Singida, msaada alioutoa kwa ushirikiano na Manifester brand. Mgeni rasmi kwenye hafla hiyo alikua ni mkuu wa wilaya ya Singida Bi. Queen Mlozi.
Redds Miss Kanda ya Kati 2014/15, Doris Mollel akiwaona watoto njiti baada ya hafla ya kukabidhi mashine mbili za kupumulia kwa watoto waliozaliwa kabla ya muda wa kawaida zenye thamani ya Tsh millioni 1.2 kwenye wodi ya watoto njiti ya hospitali ya mkoa wa Singida, msaada alioutoa kwa ushirikiano na Manifester brand. Mgeni rasmi kwenye hafla hiyo alikua ni mkuu wa wilaya ya Singida Bi. Queen Mlozi.(Picha na Albert Manifester).
Na mwandishi wetu, Singida.
Katika kuianza safari yake ya huduma za jamii kwa mwaka 2015, Redds Miss Kanda ya kati 2014-2015 Doris Mollel ametoa msaada wa mashine 2 za kupumulia kwenye hospitali ya mkoa wa Singida zenye thamani ya Tsh 1,200,000/=. Mashine hizo huwasaidia watoto waliozaliwa kabla ya muda wa kawaida (Pre-mature babies) katika mfumo wao wa upumuaji ambao huhitaji msaada wa juu zaidi mara tu wanapozaliwa.
Doris ambaye pia ni mshindi wa tatu wa Redds Miss Tanzania 2014 ni mwanaharakati wa dhana ya Urembo wenye Malengo endelevu kwa jamii ‘Beauty with a Purpose’. Amefanya kazi kubwa kwenye sekta ya elimu akijikita zaidi kwenye kuchangia Vitabu kwa shule za msingi na sasa, akiwa ni mmoja ya watu ambao walizaliwa kabla ya muda wa kawaida ameamua kupanua wigo wake wa huduma za jamii kuleta mwamko na kusaidia kuokoa maisha ya watoto hawa.
Akiongea kwenye hafla ya kukabidhi mashine hizo iliyofanyika hospitalini hapo, Mollel alisema. “Kiwango cha vifo kwa watoto wanaozaliwa kabla ya kukomaa ni karibu 30% vikichangiwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa vifaa vya kutosha kusaidia mifumo yao ya upumuaji mara tu wanapozaliwa. Nikiwa moja ya watoto hao ambaye nilibahatika kupata msaada na huduma ya kutosha nilipozaliwa, Ninaelewa ni jinsi gani matunzo haya ya awali yalivyo muhimu kwenye kuokoa maisha ya watoto hawa na ninajikita kuwasaidia”.
Bw. Albert Mbepera, Mkurungezi Manifester brand ‘huduma kwa jamii ni eneo muhimu sana kwetu. Tunafurahi kujitolea kufanya kazi na Doris katika maswala ya kusaidia jamii na tunaamini kuwa ushirikiano huu utasaidia kukusanya na kuonyesha matatizo ya wahitaji ili kuongeza uelewa na msukumo wa misaada kutoka kwa sekta binafsi na wanajamii kwa ujumla’
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa ni mkuu wa wilaya ya Singida Bi Queen Mlozi na ilihudhuriwa na Mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa wa Singida Bw. Daniel Tarimo, Daktari bingwa wa watoto wa Hospitali ya Singida, Muandaaji wa Redds Miss Singida 2014 Bora Lemmy na washindi wengine wa Redds Miss central Zone Linda Bureta, Blath Chambia, Suzy Wahere.
Doris Mollel na Manifester brand wanapenda kuwashukuru ANUDHA PHARMACEUTICALS LTS kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha shughuli hii.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269