Mahakama ya Kadhi, Ripoti ya Msola Kutikisa Bunge
Bunge linaendelea na mkutano wake wa 18, ambao kamati mbalimbali zitaendelea kuwasilisha taarifa kwa ajili ya majadiliano.
Licha
ya kamati za kisekta na zisizo za kisekta, kabla ya Bunge kuahirishwa
wiki hii, pia Kamati Teule iliyoundwa kuchunguza na kuchambua Sera
mbalimbali zinazohusu masuala ya ardhi, kilimo, mifugo, maji na
uwekezaji kubaini kasoro zilizomo katika matumizi ya ardhi, pia
itawasilisha taarifa yake.
Kwa
mujibu wa ratiba ya mkutano huo, miswada miwili itasomwa na kupitishwa
na wabunge. Miswada hiyo ni ya Sheria ya Marekebisho ya Sheria
Mbalimbali wa mwaka 2014 na ule wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi wa mwaka
2014.
Ndani
ya wiki hii, pia wabunge watajadili taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali (CAG) zilizowasilishwa katika mkutano wa Bunge wa
15 uliofanyika Aprili, mwaka jana. Taarifa hizo za CAG zitajadiliwa na
wabunge kwa siku mbili mfululizo. Zinahusu hesabu zilizokaguliwa za
Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma.
Kamati
za kisekta zitakazowasilisha taarifa zake wiki hii ni Kamati ya Ardhi,
Maliasili na Mazingira; Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji; Katiba, Sheria
na Utawala; Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Kamati ya Masuala
ya Ukimwi.
Nyingine
zitakazowasilisha taarifa zake kwa ajili ya majadiliano ni Kamati ya
Ulinzi na Usalama; Kamati ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa;
Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara; Huduma za Jamii na Kamati ya
Maendeleo ya Jamii.
Wiki
iliyopita, Bunge lilipokea na kupitisha taarifa za Kamati za Bunge
zinazosimamia Fedha za Umma ambazo ni Kamati ya Hesabu za Serikali
(PAC); Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Kamati ya Bajeti.
Pia Kamati ya Miundombinu na ya Nishati na Madini, ziliwasilisha
taarifa na kujadiliwa katika kupitishwa na wabunge.
Wakati
mjadala wa taarifa za kamati ulianza wiki iliyopita, wingu la uchaguzi
mkuu linaonekana kutanda miongoni mwa wabunge, kutokana na wengi
kujikita kwenye kero za majimboni mwao kuliko za kitaifa.
Wengi
walilalamikia miundombinu ya majimboni mwao; hususani barabara, viwanja
vya ndege na usafiri wa treni. Pia kwa upande wa taarifa ya Kamati ya
Nishati ya Madini, wengi waliochangia, walilalamikia vijiji vyao
kutofikiwa na umeme.
Mathalani,
katika kujadili taarifa za Kamati ya Miundombinu na ile ya Nishati na
Madini, wabunge wengi waliochangia, walitetea maeneo wanayotoka tofauti
na taarifa za kamati zilivyoainisha, kiasi ambacho hata Spika wa Bunge,
Anne Makinda alibaini hali hiyo.
Akizungumza
baada ya mjadala wa kamati hizo kuhitimishwa mwishoni mwa wiki, Spika
Makinda alipongeza taarifa zote za kamati za kudumu za Bunge
zilizowasilishwa kwa kusema zimeboreshwa inavyopaswa.
Makinda
alisema katika michango ya wabunge, wengi wamechangia kwa kujielekeza
kwenye majimbo tofauti na taarifa za kamati zilivyowasilisha. Aliweka
wazi kwamba hayo yanajitokeza kutokana na ukweli kwamba hiki ni kipindi
cha ‘lala salama’ kwa maana ya kipindi kuelekea uchaguzi mkuu.
Baada
ya kamati zote kukamilisha uwasilishaji wa taarifa wiki iliyopita,
utakuja Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali, kabla ya
taarifa ya Kamati Teule iliyoundwa kuchunguza na kuchambua sera
mbalimbali zinazohusu masuala ya Ardhi, Kilimo, Mifugo, Maji na
uwekezaji kubaini kasoro zilizomo katika matumizi ya ardhi.
Kamati
hiyo teule iliundwa na Spika Makinda Novemba mwaka jana. Alifikia hatua
hiyo baada ya Bunge kuridhia kuundwa kwake kutokana na malalamiko ya
wabunge bungeni, kuhusu migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji,
ambayo kwa muda mrefu haijapatiwa ufumbuzi na kusababisha madhara
ikiwamo mauaji.
Alipoiunda,
Makinda alisema baada ya kazi yake, kamati itapeleka mapendekezo yake
bungeni yatekelezwe na serikali kupunguza au kuondoa migogoro ya muda
mrefu kati ya wakulima, wafugaji, wawekezaji na watumiaji wengine wa
ardhi.
Hadidu
rejea za kamati hiyo ni kuchambua sera mbalimbali zinazohusu matumizi
ya ardhi kubainisha kasoro zilizomo na kuchunguza mikakati ya
utekelezaji wa sera hizo iliyowekwa na serikali.
Imefanya pia mapitio ya taarifa nyingine za kamati na tume zilizoundwa nyuma kushughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji.
Hadidu
nyingine ni kuchambua mikakati yote ya serikali ya kusuluhisha migogoro
ya wakulima na wafugaji; Kuchambua mikakati ya kulinda vyanzo vya maji
pamoja na uharibifu wa mazingira.
Kamati
hiyo katika hadidu nyingine, inapaswa kutoa mapendekezo yatakayoondoa
migogoro iliyopo na kudumisha uhusiano mzuri na utangamano kati ya
wakulima na wafugaji na pia itapendekeza hatua za kuchukua za
kiuwajibikaji.
Walioteuliwa
kuunda kamati na kufanya kazi hiyo ni Profesa Peter Msola (Kilolo-CCM),
Jenista Mhagama (Peramiho-CCM), Magdalena Sakaya (Viti Maalumu-CUF),
Joseph Selasini (Rombo-Chadema) na Christopher ole Sendeka
(Simanjiro-CCM).
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269