Ofisi ya Taifa ya Takwimu imesema
kuwa Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Januari, 2015 umepungua hadi
kufikia asilimia 4.0 kutoka asilimia 4.8 ya mwezi Desemba, 2014 kutokana
na kuendelea kupungua kwa kasi ya bei ya bidhaa na huduma mbalimbali
nchini.
Akitoa taarifa ya mfumuko huo leo
jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa
ya Takwimu Bw. Ephraim Kwesigabo amesema kuwa kupungua kwa mfumuko wa
Bei katika maeneo mbalimbali nchini kumesababishwa na kupungua kwa kasi
ya bei ya bidhaa za vyakula na zile zisizo.
Amesema kiwango cha badiliko la
kasi ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya kimeonyesha
kupungua katika maeneo mbalimbali nchini kikihusisha bei ya mahindi,
Unga wa mahindi , ndizi, ndizi za kupika na mihogo.
Aidha, Bw. Kwesigabo ameeleza
kuwa bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei
nchini ni pamoja na mafuta ya taa asilimia 8.4, dizeli asilimia 10.2,
Petroli kwa asilimia 6.8 na gesi ya kupikia kwa asilimia 2.9.
Akitoa ufafanuzi kuhusu kiwango
cha badiliko la kasi ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na
kaya binafsi kwa kipimo cha mwezi kati ya mwezi Desemba 2014 na Januari
2015 , amesema kuwa mwezi Januari umekuwa na ongezeko la asilimia 1.0
ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 2.0 la mwezi Desemba , 2014.
Kuhusu Fahirisi za bei kwa maana
ya kiwango cha badiliko la kasi ya bei za makundi ya bidhaa na huduma
zote zinazotumiwa na Kaya binafsi kwa kuzingatia kipimo cha mwezi
zimeonyesha kuongezeka hadi kufikia 152.43 kwa mwezi Januari 2015 kutoka
150.92 za mwezi Desemba, 2014.
Amebainisha kuwa kuongezeka kwa
Fahirisi hizo kumechangiwa na bidhaa za mchele, nyama, samaki ,lishe
kwa watoto, mbogamboga, mavazi ya wanawake, kodi ya pango na mkaa kwa
asilimia 1.6 .
Kwa upande wa uwezo wa shilingi
100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma za mlaji kwa mwezi
Januari , 2015 Kwesigabo amesema kuwa umefikia shilingi 65 na senti 60
ikilinganishwa na kiasi cha shilingi 66 na senti 26 za mwezi Desemba
2014.
“Uwezo wa shilingi 100 ya
Tanzania katika kununua bidhaa na huduma zilezile kwa mlaji kwa mwezi
Januari 2015 na Desemba 2014 umepungua kidogo, hii inamaanisha sasa mtu
hahitaji kuongeza ziada ili aweze kununua bidhaa na huduma
anazozihitaji”
Kwa upande wa mfumuko wa Bei wa
mwezi Novemba 2014 katika nchi za Afrika Mashariki amesema una mwelekeo
unaofanana , Kenya ukipungua na kufikia asilimia 5.53 kwa mwezi
Januari 2015, kutoka asilimia 6.02 za mwezi Desemba 2014, Uganda
mfumuko wa bei kwa mwezi Januari 2015 umepungua hadi asilimia 1.3 kutoka
asilimia 1.8 za mwezi Desemba 2014.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269