Picha Ya Maktaba. |
Mtoto wa umri wa miaka sita, mwenye ulemavu wa ngozi (albino), anayeishi Kijiji cha Ndoleleji, amekoswakoswa na watu waliokuwa wakimvizia akiwa katika michezo, baada ya watoto wenzake kuchukua uamuzi wa kumlinda.
Taarifa
zilizomfikia mwandishi, zilieleza kuwa ‘wawindaji’ hao waliokuwa na
gari lililokuwa na vioo vya giza, walionekana wakimfuatilia mtoto huyo
Jumamosi ya wiki iliyopita alipokuwa akiogelea mtoni na baada ya
kumkosa, wakamfuatilia katika uwanja wa mpira Jumatatu, ambako nako
walimkosa.
Akizungumza
na mwandishi, diwani wa Kata ya Shagihilu wilayani Kishapu mkoani hapa,
Mohamed Amani alisema kumefanyika majaribio mawili ya kutaka kumteka
mtoto huyo (jina limehifadhiwa), lakini kwa msaada wa watoto wenzake
hayakufanikiwa.
Kwa
mujibu wa Diwani Amani, Jumamosi iliyopita watu watatu wakiwa kwenye
gari hilo, walifika kijijini hapo na kwenda mpaka mtoni, ambako mto huyo
mwenye ulemavu wa ngozi alikuwa akicheza na wenzake.
Baada
ya kufika mtoni, watu hao wote watatu waliteremka kwenye gari na
kusogea katika eneo la mto, hatua iliyowashitua watoto wenzake waliokuwa
wakicheza wote mtoni.
Kwa
mujibu wa Amani, watoto hao wenye umri mkubwa zaidi ya mtoto huyo,
walitambua hatari iliyokuwa ikimkabili mwenzao mwenye ulemavu wa ngozi
na dalili za watu hao waliokuwa hawawafahamu, waliokuwa wakizidi
kuwasogelea.
Baada
ya kuona watu hao wakizidi kusogelea eneo lao la michezo, watoto hao
walimshauri mwenzao mwenye ulemavu wa ngozi, akimbilie nyumbani kwao na
mtoto huyo akasikia ushauri huo na kurudi nyumbani.
“Baada ya mtoto (albino) kukimbilia nyumbani kwao, wale watu waliingia kwenye lile gari na kuondoka,” alisema Amani na kuongeza kuwa hatua ya watu hao kutosema lolote kwa watoto hao lilizidi kuwapa mashaka.
Jumatatu
ya wiki hii jioni wakati mtoto huyo alipokuwa na wenzake, wakiwemo wale
aliokuwa nao mtoni, wakicheza mpira wa miguu katika kiwanja cha
kijijini hapo, gari hilo lililoonekana mtoni, lilifika uwanjani hapo na
kusimama.
Inaelezwa
kuwa baada ya kusimama, watu wale watatu walioonekana mtoni walishuka
katika gari hilo, wakaegemea gari na kuangalia watoto hao wakicheza
mpira, akiwemo mwenzao mwenye ulemavu wa ngozi.
“Safari
hii haikuwa mtoni, bali katika eneo jingine tena la wazi ambalo mtoto
huyo alikuwa akicheza mpira na wenzake… walipofika walisimama nje ya
gari lao,” alisema Diwani Amani.
Kutokana
na hali hiyo, watoto hao walihisi kuna hali ya hatari kwa mwenzao,
baada ya watoto hao kuona gari hilo kwa mara nyingine, na watu hao
wakiwa wamewasimamia na hawakuwa wakizungumza chochote.
Diwani
huyo alisema watoto hao walisitisha mchezo wao, na kumtaka mwenzao kwa
mara nyingine akimbilie nyumbani kwao, ili kusalimisha maisha yake
kutokana na utata wa usalama ulioanza kujitokeza hapo.
Akizungumza
na mwandishi, mama mzazi wa mtoto huyo, Regina Malando, alithibitisha
kurejea nyumbani mara mbili kwa mtoto wake huku akikimbia.
Regina
alisema baada ya kurejea nyumbani, mtoto huyo alimweleza kuwa kuna watu
asiowafahamu waliokuwa wamesimama kando ya uwanja waliokuwa wakifanyia
mazoezi na kwamba anawaogopa.
Mama
huyo alisema, baada ya kupewa taarifa hizo mara mbili, alimsihi mtoto
wake aingie ndani na atulie na akome kwenda kucheza mbali na nyumbani
kwao na mtoto huyo akatii ushauri wa mama yake.
Baba
wa mtoto huyo, Tito Shija, alisema aliposikia taarifa hiyo ya pili,
alikwenda katika uwanja huo na kukuta watu hao wakiingia kwenye gari na
kuondoka kwa kasi.
Shija
alisema kwa bahati mbaya hakuweza kuchukua namba za usajili wa gari
hilo, ila alishuhudia kuwa gari hilo lilikuwa na vioo vya giza sehemu
zote.
Kwa
mujibu wa Shija, kesho yake binti mmoja ambaye hakumtaja jina,
alimwambia kuwa alipita karibu ya hao watu wakamfokea na kumuuliza
anatafuta nini huko na kumwamuru aondoke haraka karibu yao.
Shija
alidai kuwa binti huyo alimwambia kuwa wakati akiondoka, alisikia watu
hao wakijadili namna ya kumpata mtoto huyo, wakati alipokuwa
akikimbilia kwao.
Diwani
Amani alisema, kutokana na hali hiyo alifikisha suala hilo kwenye Kikao
cha Kamati ya Maendeleo ya Kata na ikaamuliwa mtoto huyo mwenye ulemavu
wa ngozi, apelekwe kwenye kituo cha watoto wenye ulemavu wa ngozi,
kilichopo Buhangija katika Manispaa ya
Shinyanga.
Mwandishi
alifuatilia utekelezaji wa uamuzi huo na kuhakikishiwa na Mkuu wa Kituo
hicho cha Buhangija, Peter Ajali, kwamba amempokea mtoto huyo na
kuongeza kuwa idadi ya watoto katika kituo hicho inaongezeka kila siku,
na sasa wamefikia watoto 349 wenye ulemavu wa ngozi.
Mwanzoni
mwa mwezi huu, mtoto mwingine wa kiume mwenye ulemavu wa ngozi, Baraka
Cosmas (6) aliyekuwa akiishi na wazazi wake kijijini Kipeta, Bonde la
Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga, alishambuliwa na kujeruhiwa vibaya kwa
kukatwa kiganja cha mkono wake wa kulia na watu wasiojulikana kisha
kutokomea nacho kusikojulikana.
Mama mzazi Prisca Shaaban (28), alisema tukio hilo lilimkuta saa saba usiku, wakati akitaka kutoka nje kujisaidia.
“Nilikutana
na mtu akifungua mlango, akanipiga na kitu kichwani kisha nikazimia,
nilipozinduka nikapiga kelele na majirani wakafika ndipo nilipogundua
mtoto wangu amekatwa kiganja cha mkono wa kulia,”alisema mama mzazi.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269