Kiongozi
wa ofisi na mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi
na Utamaduni (UNESCO) nchini, Zulmira Rodrigues (kulia) akisalimiana na
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo (kushoto) alipomtembelea ofisini
kwake jijini Mwanza akiwa ameambatana na Mbunge wa Viti Maalum CCM,
anayetetea maslahi ya watu wenye albinism, Mh. Al-Shaymaa Kwegyir (wa
pili kulia) pamoja na Semeni Kingaru (wa tatu kulia).(Picha zote na
Zainul Mzige wa modewjiblog).
Na Mwandishi wetu, Mwanza
SHIRIKA
la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) limeahidi
kusaidia mapambano dhidi ya unyanyasaji na dhuluma zinazofanywa jamii
dhidi ya watu wenye albinism.
Kauli
hiyo imetolewa hivi karibuni na Kiongozi wa ofisi na mwakilishi wa
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO)
nchini, Zulmira Rodrigues wakati akizungumza na mkuu wa mkoa wa Mwanza
Magesa Mulongo.
Mwakilishi
huyo wa Unesco amesema hayo alipomtembelea Mkuu wa mkoa kumsalimia na
kumweleza hatua zinazochukuliwana Unesco katika kukabiliana na ukatili
dhidi ya watu wenye albinism.
Akifafanua
zaidi alisema kwamba UNESCO haijatenga fedha zitakazotumika kuendesha
kampeni mahsusi bali itatumia uwezo wa kiufundi uliopo kwa wataalamu
walionao na kwamba wanakusudia kuona kwamba miaka 15 ijayo watoto
wanaozaliwa nchini Tanzania wanakuwa huru pasipo na viashiria vya
kuhatarisha maisha vinavyosababishwa na mauaji ya watu wenye albinism.
Akimkaribisha
Bi Zulmira ofisini kwake, Mkuu wa mkoa Magesa Mulongo alisema kwamba
ingawa kuna utulivu katika kipindi hiki mkoani Mwanza, bado mkoa wake
unaendelea kukabiliana na viashiria vinavyosababisha ukatili kwa watu
wenye albinism na wazee.
Bwana
Magesa alisema imani potofu zilizopo zinazosadikika kufanikisha
biashara za uvuvi wa samaki, uchimbaji wa madini na wanasiasa kuendelea
na madaraka ni miongoni mwa sababu kubwa za mauaji hayo yaliyoitia doa
jeusi jamii ya kitanzania nje ya mipaka.
Alisema
kwamba jitihada zinafanywa kukabiliana na imani hizo potofu kwa
kuihamasisha jamii kutoziamini na kwamba madaraka na utajiri unatokana
na juhudi, kufanya kazi kwa bidii na si vinginevyo.
Aidha
amesema mkoa wake umekuwa ukihakikisha kwamba makundi yanayotumika kuua
watu wengine kwa kushirikisha jamii yanavunjwa na pia kuwachukulia
hatua kali wote wanaobainika kushiriki kwa njia moja au nyingine.
Hata
hivyo mwakilishi wa umoja wa mataifa alisema kwamba hali ya amani
itatawala pale tu watu watakapobaini kwamba kuua ni ukiukwaji wa haki
za binadamu na ni kosa la jinai.
Alisema
pindi binadamu watakapokiri kwamba binadamu wote ni sawa na kuishi na
albinism sio ‘mzimu’ watabadili mwelekeo mzima wa fikra potofu
kimaisha na kuishi kwa amani na kuthaminiana.
Bi
Zulmira alimwambia mkuu wa mkoa kwamba UNESCO kwa kushirikiana na wadau
wengine wataendesha makongamano yenye lengo la kushirikisha jamii
katika kuandaa na kutekeleza mikakati itakayo changia kuzuia na
kutokomeza unyanyasaji na dhuluma zinazofanya dhidi ya watu wenye
albinism.
Mkuu
wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo (kushoto) akizungumza na Kiongozi wa
ofisi na mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na
Utamaduni (UNESCO) nchini, Zulmira Rodrigues (kushoto) aliyeambatana na
Mbunge wa Viti Maalum CCM, anayetetea maslahi ya watu wenye albinism,
Mh. Al-Shaymaa Kwegyir (wa pili kulia) pamoja na Semeni Kingaru (wa tatu
kulia) alipomtembelea ofisini kwake jijini Mwanza. Wa pili kushoto ni
Katibu Tawala wa mkoa wa Mwaza, Faisal Issa.
Warsha
hizo zitafanyika kwa wakati tofauti katika kipindi cha wiki mbili
wilayani Sengerema, Misungwi, Msalala na Bariadi. Warsha hizo
zilizoanzia Sengerema Jumatano na kumalizika Ijumaa zitafuatiwa na
Misungwi Mei 25 hadi 27, Msalala Mei 28 hadi 30 na Bariadi kuanzia Mei
28-30.
Katika
warsha hiyo pamoja na kujadili mada mbalimbali, mijadala itahusisha
viongozi wa serikali, wanasiasa, viongozi wa kidini na kimila na hoja
kubwa itakayojadiliwa ni dhana ya kisayansi ya albinism, mitazamo ya
jamii kuhusu dhana hiyo, makundi mbalimbali ndani ya jamii, tofauti kati
ya utamaduni na asili.
Pia
watajadili kubainisha na kuanisha matatizo, changamoto na hatari
zinazowakabili watu wenye alibinism na kuchambua mambo yanayochangia
uwepo wa changamoto na hatari kwa watu wenye alibinism.
Katika
majadiliano hayo pia mikakati inayoweza kupunguza au kumaliza kabisa
matatizo changamoto na hatari zinazowakabili watu wenye alibinism
katika jamii yetu itatazamwa.
Watoa
mada wanatarajiwa kutoka katika halmashauri, vyama vinavyotetea maslahi
ya albinism, mbunge anayetetea maslahi ya watu wenye albinism
Al-Shaymaa Kwegyir na mwakilishi kutoka baraza la taifa la dawa asilia.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo akiendelea na maongezi na ugeni huo ofisini kwake jijini Mwanza.
Kiongozi
wa ofisi na mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi
na Utamaduni (UNESCO) nchini, Zulmira Rodrigues (kulia), akielezea nia
ya Shirika lake kusaidia mapambano dhidi ya unyanyasaji na dhuluma
zinazofanywa jamii dhidi ya watu wenye albinism nchini alipomtembelea
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo ofisini kwake jijini Mwanza.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269