Mahmoud Ahmad Arusha
Jaji Mkuu wa Zanzibar Othman
Makungu amezitaka nchi za Afrika kujiunga na Mahakama ya Afrika ya Haki
za Binadamu ilikutekeleza matakwa ya wananchi kupata haki yao ya kupata
masuala ya kisheria kwa upana Zaidi na kuweka msukumo katika suala hilo.
Kauli hiyo ameitoa leo wakati
akiongea na waandishi wa habari aliposhiriki kongamano la pili
linalojadili Masuala ya upatikanaji wa haki za binadamu na kuandaliwa na
mahakama ya Afrika ya haki za binadamu yenye makao makuu jijini Arusha.
Jaji Makungu alisema kuwa
mkutano huo ni sehemu ya kupata uzoefu na kujua wenzao kote duniani
wanavyoshiriki katika kutoa haki kwa Raia pindi wanapopeleka masuala yao
Mahakamani na itasaidia kuendesha mashauri ya kesi mahakamani kwa
haraka Zaidi na kutoa hukumu kwa muda muaafaka bila manung’uniko.
Alisema kuwa ifike mahali
Tanzania ikajiunga na kufuata sharia na hukumu za mahakama hiyo kwani
zitaweka wigo mpana wa Raia kupata haki zao kusikilizwa kwa upana katika
mahakama za hapa nchini na pia katika mahakama ya Afrika ya haki za
binadamu pindi wanapoona kuwa hawakutendewa haki na mahakama za hapa
nchini.
“Nazishauri nchi ambazo bado
hazijajiunga zifanye hivyo ilikuweka usawa wa wananchi kupata haki zao
pindi wanapoona mahakama za chini hazijawatendea haki na hivyo kuwapasa
kupeleka mashauri yao katika mahakama za juu Zaidi ikiwemo mahakama hiyo
ya Afrika ya haki za binadamu”alisema Jaji Makungu
Alisema kuwa kuna baadhi ya
kesi za hapa nchini zimefunguliwa na wananchi ikiwemo ya marehemu
mchungaji Mtikila ambayo hadi mda huu hukumu haijatekelezwa kutokana na
katiba kutokamilika hivyo akaishauri serikali kuifanyiakazi suala hilo
ilikuendana na mikataba iliyojiunga.
Mkutano huo wa pili wa masuala
ya haki za binadamu utakaofanyika kwa siku tatu utasaida kukuza uelewa
wa uendeshaji kesi na wananchi kupata fursa za kupeleka mashauri yao
wanayoona kuwa hawajatendewa haki na mahakama za nchi husika katika bara
la Afrika.
Hadi sasa ni nchi 29 tu katika
ya nchi 54 ndio zimejiunga na mahakama hiyo zikitekeleza maagizo ya
umoja wa Afrika na nchi 7 ndio zimeridhia wananchi wao kupeleka mashauri
mahakama hiyo.
Nchi hizo ni Tanzania,Mali,Burkinafaso, Ivory
Coast,Rwanda,na Malawi ambazo zimeridhia wananchi wao kupeleka mashauri
yao kwenye mahakama ya Afrika ya haki za binadamu ambapo hadi sasa bado
hazijatekeleza huku zilizotolewa na mahakama hiyo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269