Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, akizungumza na Waandishi wa Habari, leo kwenye ukumbi wa Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam. (Picha na Bashir Nkoromo)
IFUATAYO NI TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KAMA ILIVYOWASILISHWA LEO NA KINANA
Jana tarehe 07/12/2015
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ilifanya kikao chake cha kawaida
mjini Dar es salaam kwa siku moja. Kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti wa CCM,
Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
Kamati Kuu pia ilipokea
taarifa juu ya utendaji wa Serikali katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya
CCM ya mwaka 2015-2020. Kwa ujumla na
kwa kauli moja Kamati Kuu ya CCM Taifa iliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano
chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mheshimiwa
Samia Suluhu na Waziri Mkuu Mhe. Kassim M. Majaliwa kwa kasi nzuri waliyoanza
nayo katika utekelezaji wa Ilani hiyo.
Kamati Kuu kwa niaba ya
Chama imeunga mkono hatua kadhaa zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano
katika kuhakikisha Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2015-2020 inatekelezwa kwa
ufanisi. Aidha, inapongeza na kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na
Serikali katika maeneo ya:-
(1)
Kusimamia
vyanzo vya mapato ya Serikali:
Kamati
Kuu inapongeza na kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu
ya Tano katika kuhakikisha kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya
Bandari Tanzania (TPA) zinasimamia ukusanyaji wa kodi za Serikali ipasavyo.
Juhudi hizi za Serikali ya Awamu ya Tano kwa muda mfupi zimezaa matunda
yanayoonekana wazi. Aidha, Kamati Kuu inawataka wahusika mbalimbali kwenye
maeneo hayo ya udhibiti wa vyanzo vya mapato kuhakikisha wanatoa ushirikiano
kwa Serikali ili lengo liweze kutimia.
(2) Kudhibiti matumizi ya Serikali:
Kama
ilivyoagizwa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2015-2020, Serikali ya Awamu ya
Tano imeanza vizuri na kwa kasi kusimamia udhibiti wa matumizi yasiyo ya lazima
katika Serikali, ili kutumia fedha hizo kwenye utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kamati Kuu inaunga mkono juhudi hizi na kuwataka wote wanaohusika kwa namna
moja ama nyingine na udhibiti wa matumizi hayo wamuunge mkono Rais Dkt. John
Pombe Magufuli na Serikali yake katika jitihada hizi.
(3) Uhimizaji
wa wananchi katika kufanya kazi kwa bidii:
Kamati
Kuu inawataka wanaCCM na wananchi wote kwa ujumla nchini kumuunga mkono Rais na
Serikali yake kwa kuitikia wito wa kufanya kazi kwa bidii, kwa maarifa na
uzalendo. Kamati Kuu inawahimiza watu wote kwenye maeneo yao ya kazi kujituma
na kuchapa kazi ili kujenga nchi yetu na kumuunga mkono Rais Magufuli.
(4) Kusimamia
na kuhimiza uwajibikaji katika Serikali, Taasisi na Mashirika yake:
Kamati
Kuu pia inapongeza na kuunga mkono juhudi zinazoendelea za kuhakikisha kunakuwa
na uwajibikaji mkubwa Serikalini ili kuongeza kasi na ubora wa utoaji huduma. Katika
kipindi cha muda mfupi matunda yake yameanza kuonekana na hivyo kuweka msingi
mzuri wa kuboresha huduma kwa umma kwa njia endelevu.
(5) Juhudi na jitihada hizi za Serikali ya
Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Magufuli zimeleta matumaini mapya kwa
sehemu kubwa ya wananchi na kukuza imani kwa Serikali yao. Hivyo, kila Mtanzania ana wajibu wa kuunga
mkono jitihada hizi.
Pamoja na kuunga mkono na
kupongeza kasi waliyoanza nayo Rais Magufuli, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu, Kamati
Kuu inawataka Viongozi wengine wote kuiga mfano huu mzuri na kuhakikisha
wanatimiza wajibu wao ipasavyo ili kutekeleza kwa haraka zaidi Ilani ya Uchaguzi
ya CCM na kuleta maendeleo nchini.
Aidha, Kamati Kuu
inawatakia Watanzania wote kheri ya Krismas na mwaka mpya wa 2016, na inaamini mwaka
ujao utakuwa wa kuchapa kazi na wenye mafanikio zaidi.
Imetolewa na:-
Abdulrahman O. Kinana,
KATIBU
MKUU WA CCM
08/12/2015
08/12/2015
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269