Shirika la Majisafi na Majitaka
Dar es salaam (DAWASCO), limetangaza tatizo la upatikanaji wa huduma ya Maji katika maeneo yote
yanayohudumiwa na mtambo wa kuzalisha Maji wa Ruvu chini pamoja na baadhi ya
maeneo ya Mji wa Bagamoyo mkoani Pwani kutokana na mtambo huo kuzimwa kwa wastani saa 24 siku
ya Jumapili tarehe 13/12/2015.
Sababu ya kuzimwa kwa mtambo
huo ni kuruhusu kufanya matengenezo na
maboresho ya njia kubwa ya Maji inayohudumia eneo la Salasala na viunga vyake
vyote.
Akiongea na Waandishi wa habari
jijini Dar es salaam Kaimu Meneja uhusiano wa Dawasco, Bi. Everlasting Lyaro, ametoa
wito kwa wateja na wananchi wote kuhifadhi
Maji ya kutosha na kuyatumia kwa matumiz ya muhimu ili kuweza kukidhi mahitaji
husika kwa kipindi hicho.
“Tupo katika maboresho ya huduma
ya Maji, mtambo wetu wa Ruvu chini utazimwa kwa takribani saa 24, tunawaomba
wateja wetu muhifadhi Maji ya kutosha na kuyatumia vizuri mpaka maketengezo
yatakapokamilika, nasi tutajitahidi kadri tuwezavyo kuhakikisha tunarejesha
huduma ya Maji kwa wakati uliopangwa”
alisema Bi. Lyaro
Amebainisha kuwa matengenezo
hayo yatasababisha maeneo mengi ya Jiji la Dar es Salaam kukosa huduma ya Maji
ikiwemo Mji wote wa Bagamoyo, Bunju,
Boko, Tegeta, Kunduchi, Salasala, Jangwani, Mbezi beach na Kawe, Mlalakuwa,
Mwenge, Mikocheni, Msasani, Sinza, Manzese, Mabibo, Kijitonyama, Kinondoni,
Oysterbay, Magomeni, Upanga, Kariakoo, City Centre, Ilala, Ubungo Maziwa,
Kigogo, Mburahati, Hospitali ya Muhimbili pamoja na eneo la Buguruni.
Everlasting Lyaro
Kaimu Meneja Uhusiano
022 2194800 / 0800110064
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269