Mkuu
wa Operesheni wa Jeshi la Polisi Mkoani Arusha (ACP) Edward Balele
akifungua kikao kati ya Jeshi hilo na Taasisi za ulinzi kujadili
mustakabali wa usalama ndani ya mkoa huu. Kikao hicho kilifanyika katika
ukumbi wa Bwalo la Polisi Jijini hapa (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi
la Polisi Arusha)
Meneja
Mkuu wa Kampuni ya Ulinzi ya KK kanda ya Kaskazini Claude Herssens
akichangia mada katika kikao kilichoandaliwa na Jeshi la Polisi Mkoani
hapa na kuziusisha taasisi mbalimbali za ulinzi (Picha na Rashid Nchimbi
wa Jeshi la Polisi Arusha)
Baadhi
ya washiriki wa Taasisi za Ulinzi wakiwa wanasikiliza moja ya mada kwa
umakini ili baadae waweze kutekeleza kwa vitendo. (Picha na Rashid
Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Katibu
wa TUPSE kanda ya Kaskazini Aisha Masoud akielezea umuhimu wa mikataba
baina ya waajiri na waajiriwa wa Makampuni ya Ulinzi. (Picha na Rashid
Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Mkuu
wa Upelelezi ya Makosa Jinai Mkoa wa Arusha (SSP) Muliro Jumanne Muliro
akielezea athari za kuwa na waajiriwa ambao hawana sifa kwenye kazi za
ulinzi. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi.
Mkuu wa Kitengo cha Polisi Jamii Mkoa wa Arusha (SSP) Mary Lugola
akitoa elimu ya Huduma bora kwa mteja kwa Makampuni ya Ulinzi (Picha na
Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
……………………………………………………………………………………………………..
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi la Polisi mkoani hapa
limeazimia kushirikiana na Makapuni binafsi ya Ulinzi na taasisi za
Ulinzi kutoka UN-ICTR, UNMICT, kitengo cha Ulinzi cha B.O.T pamoja na
Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu katika kupeana baadhi ya
taarifa za uhalifu na wahalifu mara kwa mara kwa njia mtandao wa kijamii
wa “whatsApp”.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa
Operesheni wa Jeshi hilo mkoani hapa (ACP) Edward Balele wakati
akifungua kikao kilichofanyika katika Bwalo la Polisi mjini hapa
alipokuwa anazungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoani hapa
mwishoni mwa wiki kati ya Jeshi hilo na wawakilishi wa Makampuni 31 ya
Ulinzi, Benki Kuu Kanda ya Kaskazini, Mahakama ya Afrika ya Haki za
Kibinadamu,UN-ICTR na UNMICT.
Mkuu huyo wa Operesheni alisema
kwamba imefika wakati sasa kwa taasisi hizo kuzidi kuimarisha mahusiano
kwa ukaribu huku njia za kisasa za mawasiliano zikitumika katika kupeana
taarifa za uhalifu na pia kubadililishana uzoefu katika masuala ya
ulinzi na usalama.
Alisema awali taarifa juu ya
matukio mbalimbali sio kwamba zilikuwa hazipatikani bali zilikuwa
zinawafikia walengwa kwa mtindo wa ujumbe mfupi yaani SMS lakini kwa
kutumia mfumo wa kikundi cha “WhatsApp” ambacho kitapewa jina maalum,
taasisi hizo zitakuwa zinapata na kutoa taarifa kwa pamoja na kila
mhusika atakuwa anachangia mawazo yake huku wanachama wengine wa kikundi
hicho wakiwa wanaona ushauri wa kila mchangiaji.
Aidha mbali na uundaji wa kundi
hilo litakalotumia mtandao huo wa kijamii mbao umeshika kasi katika
mawasiliano pia aliyaomba Makampuni hayo kutoa ushirikiano zaidi hasa
kwa kutoa rasilimali vifaa pamoja na askari katika kuelekea mwisho wa
mwaka kwa nia ya kufanya doria ya pamoja hivyo kudhibiti vitendo vya
uhalifu ndani ya Mkoa wa Arusha.
Kwa upande wake Mkuu wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Arusha (SSP) Muliro Jumanne Muliro
alisema kwamba Jeshi la Polisi na Makampuni hayo kila chombo kikiwa
kinawajibika ipasavyo katika nafasi yake mafanikio ya kudhibiti vitendo
vya uhalifu yatakuwa makubwa.
Alisema anathamini mchango
mkubwa unaotolewa na Makapuni hayo ya Ulinzi kwani matukio mengi ya
uvunjaji wa Maghala ya viwanda, Ofisi mbalimbali na Makampuni yamepungua
ukilinganisha na miaka ya nyuma kabla Makapuni hayo ya Ulinzi
kukubaliwa kisheria.
Mkuu huyo wa Upelelezi alisema
kwamba wakati wa uajiri wa askari hao wanatakiwa waangalie mambo
mablimbali ikiwemo akili ya kuweza kugundua kitu kinachoashiria uhalifu,
kuwa mwaminifu, kuwa mtulivu na kuwa mvumilivu na kusema kwamba huwa
anafadhaishwa sana pale anapopata shauri linalomhusisha askari yoyote
katika uhalifu hali ambayo inatia doa na aibu kwa taasisi zote za
Ulinzi.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Polisi
Jamii Mkoa wa Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (SSP) Mary
Lugola ambaye alizungumzia juu ya huduma bora kwa Mteja ambapo aliwataka
Wawakilishi wa Makampuni hayo kuwaelekeza askari wao kuwa, wawe na
lugha nzuri kwa wateja wao jambo ambalo pengine litakuwa linazidi
kuwavutia wengine na hatimaye kupata malindo mengi ambayo yatawaongezea
kipato, mbali na hilo pia aliwataka kutotumia nguvu kupita kiasi katika
ukamataji ili kupunguza madhara makubwa yanayoweza kutokea.
Kwa upande wake Mkuu wa kikosi
cha kutuliza ghasia (FFU) Mkoa wa Arusha (SSP) Ramadhani Giro yeye
aliyataka makampuni hayo kufanya mazoezi ya mara kwa mara na alisema
baadhi ya Makampuni ya Ulinzi huwa yanapata mafunzo mbalimbali kama
vile matumizi sahihi ya silaha, ukakamavu na mbinu mbalimbali za kuweza
kubaini uhalifu na wahalifu toka kwa askari waliopo katika kikosi hicho
na kutoa wito kwa askari wa makapuni mengine kujitokeza ili waweze
kupata mafunzo hayo na kupunguza madhara yanayoweza kutokea huko
mbeleni.
Wakichangia katika kikao hicho
baadhi ya wawakilishi wa Makampuni ya Ulinzi, Mwakilishi toka Kampuni ya
KK Security ambaye pia ni Meneja Mkuu wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini
Bw. Claude Herssens alilisifu Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa kuitikia
wito kwa haraka pindi wanapoomba msaada na kuongeza kwamba mtandao huo
utawasaidia sana na hivyo kuwafanya wajue tukio ambalo wanatakiwa kwenda
kutoa msaada nje ya mipaka yao ya kazi na tukio ambalo litakuwa
linawahusu Polisi pekee.
Naye Katibu wa Chama Cha
waajiriwa wa Makampuni Binafsi Kanda ya Kaskazini (TUPSE) Aisha Masoud
alizidi kusisitiza kwamba bado baadhi ya Kampuni hizo zinachangamoto
hasa katika suala zima la mishahara ya wafanyakazi wao japokuwa
serikali toka mwaka 2013 mwezi Agosti ilishatangaza mishahara mipya
lakini baadhi yao hawajatekeleza hilo na kuwataka wafanye hivyo pamoja
na kuwaingiza katika mifuko ya Jamii.
Mara kwa mara Jeshi la Polisi
Mkoani hapa limekuwa likifanya vikao na Makapuni ya Ulinzi lengo likiwa
ni kukumbushana majukumu ya utendaji wa kazi za kila siku hali ambayo
inasababisha kuimarika kwa hali ya usalama.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269