Katika
siku za hivi karibuni kumekuwa na taarifa za kuwepo kwa Programu
(Application) ya simu ikijulikana kama SOFTBOX TANZANIA iliyosemekana
iko kwenye Google PLAYSTORE.
Ilidaiwa kuwa program (Application) hiyo ya SOFTBOX TANZANIA
ilikuwa na uwezo wa kunasa au kuingilia mazungumzo ya simu, ujumbe mfupi
pamoja na mawasiliano ya WhatsApp kutoka kwenye simu ya mtu binafsi.
Kwa yeyote aliyekuwa na nia hiyo ya kunasa au kuingilia
mazungumzo ya simu, ujumbe mfupi pamoja na mawasiliano ya WhatsApp
kutoka kwenye simu ya mtu mwingine alihitajika kulipia fedha kiasi cha
Tshs 35,000/= kupitia mitandao ya simu ili kupata namba ya siri kwa
ajili ya kuwezesha nia hiyo.
Mamlaka ya Mawasiliano imefanya uchunguzi kubaini kuwepo kwa
programu hiyo na ukweli kuhusu uwezo wake wa kufanya kilichodaiwa, ikiwa
ni pamoja na kuangalia madhara ya program hiyo na sheria inasema nini
kuhusu suala hili. Baada ya kufanya uchunguzi wa kina, Mamlaka ya
Mawasiliano ilibaini na imejiridhisha kuwa program (Application) hiyo
haina uwezo huo wa kunasa au kuingilia mazungumzo ya simu, ujumbe mfupi
pamoja na mawasiliano ya WhatsApp kutoka kwenye simu ya mtu binafsi kama
ilivyodaiwa.
Aidha Mamlaka imebaini kuwa watengenezaji (Developers) wa
programu hiyo walikuwa na nia ya kutapeli na kujipatia fedha hiyo kiasi
cha Tshs 35,000/= kwa njia ya udanganyifu wakitumia kivutio cha kunasa
au kuingilia mazungumzo ya simu, ujumbe mfupi pamoja na mawasiliano ya
WhatsApp kutoka kwenye simu za watu binafsi.
Programu (Application) nyingine ya aina hiyo iliibuka tena ikiitwa SIMNET Tanzania ikiwa na maelezo kama ya awali.
Wakati Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania pamoja na Jeshi la Polisi
wakiendelea na uchunguzi zaidi, tunapenda kuuarifu umma wa Watanzania
kuepuka kufanya mambo yafuatayo:
1. Kuvutiwa na matendo yaliyo kinyume na sheria na maadili ya
matumizi mazuri ya mawasiliano kama hili la kunasa au kuingilia
mazungumzo ya simu, ujumbe mfupi pamoja na mawasiliano ya WhatsApp
kutoka kwenye simu ya mtu binafsi. Kitendo hiki ni kosa la jinai kwa
mujibu wa kifungu cha 6 na 10 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka
2015 na kifungu cha 123 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na
Posta (EPOCA) ya Mwaka 2010. Sheria katika vifungu hivyo inakataza mtu
yeyote kuingilia mawasiliano ya mtu mwingine. Adhabu kali ya makosa haya
ni faini isiyopungua shilingi milioni tano au kutumikia kifungo kwa
kipindi kisichopungua mwaka mmoja au vyote kwa pamoja.
2. Mamlaka inawatahadharisha watumiaji wa huduma za mawasiliano
kutokuwa wepesi na kudanganyika kufanya malipo yoyote kwa njia ya
mitandao kwa huduma wasiyokuwa na uhakika nayo au bila kujiridhisha na
uwepo wa huduma hiyo. Ni vizuri kutoa taarifa kwa mtoa huduma wako au
kuwasiliana na Mamlaka ya Mawasiliano kupitia barua pepe
malalamiko@tcra.go.tz au kupiga simu namba 0784558270/1.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
04/12/2015
Your Ad Spot
Dec 4, 2015
Home
Unlabelled
TAHADHARI KUHUSU KUINGILIA MAWASILIANO YA WATU AU KUFUATILIA
TAHADHARI KUHUSU KUINGILIA MAWASILIANO YA WATU AU KUFUATILIA
Share This
About khamisimussa77@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269