Na Magreth Kinabo
Tanzania imetangazwa rasmi kuwa ni mojwapo ya nchi isiyokuwa na
ugonjwa wa polio katika nchi za Afrika katika mkutano wa Tume ya Afrika
ya kuthibitishwa kutokomezwa kwa polio(Afrika Regional Certification
Commission for Polio Eradication).
Kutangazwa kulifanyika katika mkutano huo uliofanyika nchini Madagascar, Novemba 26, mwaka huu.
Kauli hiyo ilitolewa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii, Dkt. Donan Mmbando wakati wa mkutano wake na waandishi
wa habari kuhusu ugonjwa huo ulifanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa
wizara hiyo jijini Dar es Salaam.
“Hii inamaanisha kuwa kwa sasa hatuna ugonjwa wa polio tena
nchini kwa sababu tumeweza kuwafikia watoto wengi zaidi kwa kuwapatia
chanjo ya polio na hivyo kuongeza kinga kwenye jamii.Kutokana na
mafanikio hayo, tunatakiwa bado kuendelea na kutoa chanjo ya polio kwa
watoto wote stahiki ili kuongeza kinga kwa jamii pamoja kuimarisha mfumo
wa ufutiliaji wa mgonjwa yoyote mwenye ulemavu wa ghafla,” alisema Dkt.
Mmbando.
Katibu Mkuu huyo alifafanua kwamba mgonjwa wa mwisho wa polio alipatikana Julai mwaka 1996 hapa nchini.
Aliongeza kuwa ufuatiliaji wa magonjwa yanayokingwa na chanjo
uliimarishwa na kufikia viwango vinavyo kukubalika kimataifa na
kuthibitisha kuwa watoto wenye umri chini ya miaka 15 waliopata ulemavu
wa ghafla wanapatikana na sampuli zao kuchukuliwa mara moja.
Hivyo kuanzia mwaka 1997 mpaka Oktoba 2015 jumla ya sampuli
6,249 za watoto waliopata ulemavu zilipelekwa kwenye maabara za
kimataifa na kuthibitishwa kuwa hakuna sampuli iliyoonesha uwepo wa
ugonjwa wa polio.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269