Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama mfumo wa kukagua makontena bandarini
kwa kutumia scaner huku akipata maelzo kutoka kwa Ofisa wa forodha,
January Shauri wakati alipotembelea bandari ya Dar es salaam Desemba 3,
2015 kutaka kujua ukweli wa tuhuma za makontena 2431 yaliyopita
bandarini hapo bila kulipiwa kodi ya serikali. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kuhusu utoaji bili za kulipia
kodi za serikali kwa watumiaji wa bandari ya Dar es salaam kutoka kwa
ofisa mwandamizi wa masuala ya fedha , Bw. Sartho Mbuya wakati
alipotembelea bandari hiyo Desemba 3, 2015 kutaka kujua ukweli wa
tuhuma za makontena 2431 yaliyopita bandarini hapo bila kulipiwa kodi za
serikali.(Picha na Ofisi ya Waziri )
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akimwonyesha Kaimu Meneja wa Bandari ya Dar es
salaam, Bw. Abel Mhanga (kulia) orodha ya makontena 2,431 yaliyopitia
kwenye banda ya Dar es salaam bila kulipiwa kodi wakati alipofanya ziara
kwenye bandari hiyo Desemba ,3, 2015. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akitembelea steheni ya reli ya Dar es salaam Desemba 3, 2015. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akizungumza na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
Shirika la Reli nchini TRL wakati alipotembelea stesheni ya Dar es
salaam kukagua uendeshaji wa Shirika hilo Desemba 3, 2015. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akikagua bandari ya Dar es salaam Desemba
3, 2015 ambako alikwenda kupata ukweli kuhusu makontena 2,431yaliyopitia
kwenye bandari hiyo bila kulipiwa kodi ya serikali. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
………………………………………………………………………………………………….
*Akuta makontena 2,431 yametoka bila kulipiwa ushuru
*Ataka majina yaletwe ofisini leo saa 11 jioni
*Atoa wiki moja kwa mfumo wa malipo kubadilishwa
*Akagua mabehewa, awaweka kiporo TRL
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amefanya ziara nyingine ya kushtukiza bandarini na kukagua mfumo wa
upokeaji na utoaji mizigo na utozaji wa malipo baada ya kupewa taarifa
kwamba kuna makontena 2,431 yametolewa bila kulipiwa ushuru.
Waziri Mkuu alisema kwa mujibu wa
taarifa ya ukaguzi wa bandari ya kuanzia Machi hadi Septemba 2014,
makontena hayo yalipita bila kulipiwa kodi kupitia bandari kavu nne
(ICDs) ambazo ni JEFAG, DICD, PMM na AZAM.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ni
watumishi 10 tu ambao wamesimamishwa kazi kutokana na makosa hayo.
“Mmeamua kuwasimamisha kazi watu wadogo na kuwaacha wakubwa wanaendelea
na kazi. Hatuwezi kuendelea kuikosesha Serikali mapato namna hii,”
alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amemtaka Kaimu Meneja
wa Bandari, Bw. Hebel Mhanga amletee ofisini majina ya watumishi wote
waliohusika na ukwepaji kodi huo ifikapo leo saa 11 jioni. Pia amempa
Meneja huyo wiki moja kuhakikisha kuwa mamlaka hiyo inabadilisha mfumo
wa utozaji malipo kutoka kwenye billing system na badala yake kuweka mfumo wa malipo wa kielektroniki (e-payment).
Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi,
Desemba 3, 2015), wakati akikagua idara mbalimbali za mamlaka ya bandari
na kuona ukaguzi wa mizigo unavyofanyika kwa kutumia scanners. Akiwa
kwenye chumba cha scanner mojawapo, Waziri Mkuu alikuta manifest moja ikisema kontena limejaa diapers lakini picha ya kwenye kompyuta ya scanner ilionyesha kuwa ndani ya kontena hilo kuna vitu kama vifaa vya umeme.
Kwa mujibu wa Kaimu Meneja Bandari
upande wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Ben Usaje ambaye pia ni
msimamizi wa kitengo cha scanner, inapobainika taarifa kama
hiyo inapaswa itumwe kwa wenye ICDs ili wafanye ukaguzi kwa kulifungua
kontena ili kuhakikisha mali zilizomo ndizo zilizoandikishwa kwenye manifest.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
Majaliwa amefanya ziara ya kushtukiza kwenye ofisi za Shirika la Reli
(TRL) na kukagua mabehewa yaliyokuwepo kisha akazungumza na baadhi ya
wafanyakazi waliokuwepo kwenye stesheni hiyo ambako alibaini madudu
kwenye malipo ya mishahara na makato ya michango ya wafanyakazi.
Akizungumza na Mkurugenzi Mkuu
TRL, Mhandisi Elias Mshana, Waziri Mkuu alisema amefika kwenye shirika
hilo ili kujifunza utendaji wao kazi lakini anazo taarifa za wao kupewa
fedha na Serikali kiasi cha sh. bilioni 13.5/- ili waendeleze
miundombinu ya reli lakini hawakufanya hivyo. “Nia ya kuwapa fedha hizo
ilikuwa ni kuboresha miradi ili muweze kujiendesha kibiashara lakini
nyie mkaamua kujilipa wenyewe,” alisema.
“Ninazo taarifa kuwa baada ya
hapo, mlikopa sh. bilioni 3 kutoka benki ya TIB ili kuendesha miradi ya
shirika lakini badala ya kufanya miradi, fedha hizo mkaamua nazo
kujilipa mishahara. Sasa sijui mnarudishaje huo mkopo wakati hakuna
mradi wowote uliofanyika,” alihoji bila kupata majibu.
Alipoulizwa wafanyakazi wana
matatizo gani hapo TRL, Katibu wa TRAWU, Bw. Boaz Nyakeke alisema
wanadai malimbikizo ya makato yao kwenye mifuko ya pensheni, malimbikizo
ya makato kwenye SACCOS na malimbikizo ya kuanzia Julai – Novemba 2014.
Waziri Mkuu kwa upande wake
alimtaka Mhandisi Mshana asimamie uboreshaji huduma za usafiri wa treni
katika Jiji la Dar es Salaam ili hata mabasi ya mwendo kasi yatakapoanza
wananchi waweze kuwa na uhuru wa kuchagua aina ya usafiri wautakao.
“Tunataka kujenga yadi kubwa nje
ya mji ili watu wenye magari wawe wanayaacha huko na kutumia usafiri wa
treni au DART kuja mjini kama njia mojawapo ya kupunguza msongamano wa
magari jijini Dar es Salaam,” alisema.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269