Waziri
wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt Philip Mpango (kushoto) akiongea na
waandishi wa habari (hawamo pichani)jijini Dar es Salaam, kuhusu hatua
zilizochukuliwa na Serikali dhidi ya Benki ya Stanbic Tanzania kutokana
na ushiriki wake katika kuwezesha mkopo wa Serikali wa Dola za
Kimarekani Milioni 600 na Kulia kwake ni Naibu Gavana wa Benki Kuu ya
Tanzania(BOT) Bw. Lila Mkila.
Waziri
wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt Philip Mpango (katikati) akitoa tamko kwa
waandishi wa habari (hawamo pichani) jijini Dar es Salaam, kuhusiana na
kusudio la kuitoza Benki ya Stanbic faini ya shilingi bilioni 3. Kulia
kwake ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa
Serikali Dkt. Servicius Likwelile na Kushoto kwake ni Naibu Gavana wa
Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Bw. Lila Mkila.
………………………………………………………………………………………
Utangulizi
Mwezi
Julai 2013, Benki Kuu ya Tanzania kupitia ufuatiliaji wa kawaida wa
shughuli za mabenki iligundua matatizo yaliyohusiana na hasara itokanayo
na mikopo na pia kuacha na kuondolewa kazini kwa viongozi waandamizi wa
Stanbic Bank Tanzania Limited (Stanbic) katika muda mfupi. Kutokana na
hilo, Benki Kuu iliamua kufanya ukaguzi wa kulenga (Targeted
Examination) katika benki hiyo. Ukaguzi huo ni kwa mujibu wa mamlaka
iliyopewa Benki Kuu chini ya Kifungu 47 cha Sheria ya Benki Kuu ya mwaka
2006 na Kifungu 31 cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka
2006.
Matokeo ya Ukaguzi wa Benki Kuu
Katika
ukaguzi huo, wakaguzi wa Benki Kuu, pamoja na mambo mengine walibaini
miamala ya kutia shaka iliyohusu malipo kwa kampuni ya kitanzania ya
Enterprise Growth Market Advisors (EGMA). Kampuni ya EGMA ilihusika
katika uwezeshaji wa upatikanaji wa Mkopo kwa Serikali ya Tanzania
ambapo Standard Bank Plc (ambayo kwa sasa inajulikana kama ICBC Standard
Bank) na Stanbic Bank Tanzania Limited kwa pamoja walikuwa “Mwezeshaji
Mkuu” (Lead Arranger). Malipo hayo kwa kampuni ya EGMA yalikuwa
yamefanyika kinyume na taratibu za kibenki na yalihusisha uongozi wa
benki ya Stanbic. Jumla ya malipo yalikuwa ni kiasi cha dola za
kimarekani milioni 6, na zililipwa katika akaunti ya EGMA na kutolewa
kwa muda mfupi kwa njia ya fedha taslimu (cash) ambayo ni nje ya
taratibu za kibenki.
Taarifa
ya ukaguzi huo iliwasilishwa kwa benki ya Stanbic kwa mujibu wa
taratibu, na Benki Kuu iliiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo
kuchukua hatua stahiki za kurekebisha kasoro zilizoonekana. Aidha, benki
ya Stanbic iliagizwa kutoa taarifa kwa Kitengo cha Financial
Intelligence Unit (FIU) kilichopo Wizara ya Fedha na Mipango kuhusiana
na miamala hiyo yenye mashaka katika akaunti ya EGMA kama Sheria ya
Kuzuia Utakatishaji wa Fedha Haramu ya mwaka 2006 (The Anti-Money
Laundering Act, 2006) inavyoelekeza. Benki ya Stanbic ilitekeleza
maagizo na kutoa taarifa FIU kuhusu miamala inayotiliwa shaka.
Mnamo
29 Septemba 2015, Benki Kuu ilipokea barua toka Idara ya Serikali ya
Uingereza inayohusika na Upelelezi wa Makosa ya Kugushi na Rushwa
(Serious Fraud Office – SFO) ikiiomba Benki Kuu ruhusa ya kutumia ripoti
yake ya ukaguzi kama ushahidi katika kesi dhidi ya Standard Bank Plc
ambayo ilikuwa ni mshirika wa Stanbic Bank Tanzania Limited katika
kuwezesha mkopo wa dola za kimarekani milioni 600 kwa Serikali na kwamba
ripoti hiyo ingekuwa wazi kwa umma. Benki Kuu iliijibu SFO kuwa kwa
mujibu wa Sheria ripoti za Benki Kuu zinatolewa tu kwa benki au taasisi
ya fedha inayohusika, hata hivyo, Benki Kuu haikuwa na pingamizi kwa SFO
kutumia taarifa za ripoti hiyo kwa kuzingatia chanzo cha ripoti hiyo.
Hatimaye,
Standard Bank Plc ilikubali makosa na ilitozwa faini ya jumla ya dola
za kimarekani milioni 32.20, ambapo kiasi cha dola za kimarekani milioni
7 zinalipwa kwa Serikali ya Tanzania (dola za kimarekani milioni 6
zilikuwa ni fidia na dola za kimarekani milioni 1 ni riba).
Kwa
kuzingatia mapungufu ya kufanya miamala iliyohusisha EGMA na pia
kutokuweka taratibu madhubuti za udhibiti wa ndani, na kwa kuzingatia
Kifungu 67 cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006,
Benki Kuu imeiandikia benki ya Stanbic barua ya kusudio la kuitoza faini
ya shilingi bilioni 3. Sheria inaitaka benki ya Stanbic kutoa utetezi
katika kipindi cha siku ishirini (20) ambacho kitaisha tarehe 30 Januari
2016. Endapo Benki Kuu haitaridhika na utetezi, benki ya Stanbic
italazimika kulipa faini hiyo.
Hitimisho
Benki
Kuu imechukua hatua hizo kama onyo kwa benki ya Stanbic na ili iweze
kuwa makini katika kuhakikisha kuwa shughuli zake zinaendeshwa kwa
mujibu wa taratibu za kibenki na kuzingatia Sheria.
Aidha,
hatua hii ni onyo kwa mabenki na taasisi za fedha zisijihusishe na
makosa ya aina hii ambayo ni kinyume cha taratibu za kibenki na ni
uvunjaji wa Sheria za nchi. Hatua kali zitaendelea kuchukuliwa kwa benki
au taasisi ya fedha yoyote itakayobainika kwenda kinyume na taratibu za
kibenki na Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269