WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imepanga kufungua viwanda vya
kusindika ngozi kwenye mikoa ya Shinyanga, Geita na Dar es Salaam ili
kutoa soko kwa ngozi za wanyama wanaochinjwa kwenye machinjio ya mikoa
hiyo.Ametoa
kauli hiyo jana jioni (Jumatatu, Januari 18, 2016) wakati akizungumza
na baadhi ya Watanzania waishio Botswana kwenye kikao kilichofanyika
kwenye kituo cha mikutano ya kimataifa (GICC), jijini Gaborone,
Botswana.Waziri
Mkuu alikuwa nchini Botswana kwa ziara ya siku moja kumwakilisha Rais
Dk. John Pombe Magufuli kwenye mkutano wa SADC Double Troika yaani kikao
maalum cha Wakuu wa Nchi na Serikali (SADC Summit) na Wakuu wa Nchi
wanaounda Chombo cha Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama (SADC Organ
on Politics, Defense and Security Cooperation) uliofanyika kwenye kituo
cha mikutano ya kimataifa (GICC), jijini Gaborone, Botswana
Akizingumza
na Watanzania hao, Waziri Mkuu alisema: “Tumeamua kufungua viwanda vya
kusindika ngozi kwenye mikoa ya Shinyanga, Geita na Dar es Salaam (kule
Pugu) ili ngozi zikishachunwa, zipelekwe moja kwa moja kiwandani,”
alisema.
Alisema
Serikali imeamua kuongeza viwanda nchini kama njia mojawapo ya kukuza
uchumi, kuacha kuuza mali ghafi lakini pia ni fursa ya kuongeza ajira
kwa Watanzania.
Akijibu
hoja zilizoainishwa kwenye risala yao, Waziri Mkuu alisema Serikali
bado ina nia ya kuhamia Dodoma na kwamba itaendelea kutenga fedha zaidi
ili wizara nyingi zijenge ofisi zao Dodoma. “Serikali ilikwishaamua
kwamba Dodoma ni mji wa kiserikali na Dar es Salaam ni mji wa
kibiashara. Kwa sasa kuna baadhi ya Wizara zimeshajenga ofisi Dodoma na
kuna taasisi kama vile Benki Kuu nazo pia zimejenga ofisi zake Dodoma.
Tutaendelea kutenga fedha zaidi ili wizara nyingine zikamilishe ujenzi
wa ofisi zao,” alisema.
Waziri
Mkuu Majaliwa alitumia fursa hiyo kuwataka Watanzania waishio ughaibuni
(Diaspora) watafute fedha za mitaji ama zao ama kupitia kwa marafiki
zao ili waweze kuwekeza nyumbani (Tanzania).
“Nia
ya Serikali sasa hivi ni kufungua milango kwa wawekezaji hasa wenye nia
ya kujenga viwanda. Njooni nyumbani muone ni eneo gani mnaweza
kuwekeza, kama mna miradi huku fungueni matawi kule nyumbani. Serikali
inajivunia uwepo wenu kwa sababu inatambua kwamba huku mliko kuna kitu
mnajifunza na mnaweza kukirudisha nyumbani kwa manufaa ya Watanzania na
Taifa kwa ujumla,” alisema.
Mapema,
akisoma risala yao kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa Chama cha
Watanzania waishio nchini Botswana (The Association of Tanzanians in
Botswana – ATB), Bw. Neiman Kissasi alisema chama hicho kilianzishwa
mwaka 1992 kikiwa na lengo la kuwaunganisha Watanzania waishio Botswana
pamoja kujenga undugu wao na kusaidiana.
Katika
risala yao, walishauri wafugaji wa Tanzania waelimishwe na kuwezeshwa
kufuga kisasa na kuondokana na ufugaji wa kurandaranda. Pia waliiomba
Serikali iongeze kasi ya mpango wake wa kuhamisha shughuli zote za
Serikali mjini Dodoma, kwani itasaidia kupunguza matumizi ya Serikali
kwa kuwa shughuli za Serikali zitakuwa zinafanyika eneo moja.
Vilevile,
waliiomba Serikali ifungue fursa za kiuchumi kwenye mikoa mingine ya
Tanga, Lindi, Mtwara, Pwani, Kigoma, Mbeya, Mwanza na Arusha badala ya
kuziacha ziwe Dar es Salaam peke yake. “Hii itasaidia kuibua fursa za
kiuchumi na kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam”, ilisema
sehemu ya risala yao.
Waziri Mkuu alirejea jijini Dar es Salaam jana usiku (Jumatatu, Januari 18, 2016.)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
- L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMANNE, JANUARI 19, 2016
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269