Wizara
yangu inaendelea kutoa taarifa ya wiki kwa umma kuhusu mwenendo wa
ugonjwa wa kipindupindu hapa nchini. Hadi kufikia tarehe 24 Januari
2016, jumla ya watu 14,608 wameugua ugonjwa huo, na kati yao watu 228
wamepoteza maisha kwa ugonjwa huu. Njombe, Ruvuma na Mtwara ndiyo Mikoa
pekee ambayo haijawahi kuripoti mgonjwa yoyote wa kipindupindu, tangu
mlipuko huu uanze mnamo mwezi Agosti mwaka huu.
Kwa mujibu wa Takwimu za kuanzia
tarehe 18 hadi 24 Januari 2016, ni kuwa jumla ya Mikoa ambayo imeripoti
kuwa na wagonjwa ni 15 ambapo idadi ya wagonjwa 524 na vifo 10
vimeripotiwa. Idadi ya wagonjwa walioripotiwa wiki hii imepungua
ukiliinganisha na idadi ya wiki iliyoishia tarehe 17 ambapo kulikuwa na
wagonjwa 621 na vifo 14 ambalo ni punguzo la asilimia (16%). Mkoa wa
Morogoro bado umeendelea kuripoti idadi kubwa zaidi ya wagonjwa
ukilinganishwa na Mikoa mingine, (Manispaa ya Morogoro 89, Halmashauri
ya Morogoro 36, Mvomero 17), ukifuatiwa na mikoa ya Mwanza (Ukerewe 36,
Nyamagana 19 na Ilemela 13), Simiyu (Bariadi DC 29 na Bariadi municipal
23), Manyara (Simanjiro 48), Mara (Musoma Manispaa 11, Musoma DC 8,
Rorya 8 na Butiama 8), Geita (Geita DC 21 na Geita TC 6) na Mbeya (Kyela
26).
Mikoa mingine ambayo bado pia imeendelea kuripoti wagonjwa ni
pamoja na Dodoma (Wagonjwa 22), Arusha (21), Tabora (18), Singida (18),
Lindi (12), Rukwa (7), Kilimanjaro (6) na Kagera (2).
Mwanzoni mwa mwezi Januari mwaka huu, Wizara yangu kwa
kushirikiana na wadau ilituma timu ya jopo la wataalam kutoka ngazi ya
Taifa kwenda kusaidiana na wataalam waliopo katika ngazi ya mkoa na
halmashauri katika mikoa 7 iliyokuwa inatoa taarifa ya kuwa na wagonjwa
wengi zaidi. Mikoa hiyo ni Arusha, Manyara, Mwanza, Simiyu, Singida,
Mara na Morogoro. Mafanikio ya kazi iliyofanywa na Jopo hilo yameanza
kuonekana kwani katika Mikoa hiyo saba idadi ya wagonjwa wa kipindupindu
imeanza kupungua. Pamoja na mafanikio hayo zipo changamoto ambazo timu
hizo ilizibaini kuwepo ambazo zinachangia kulegalega kwa juhudi za
kupambana na Kipindupindu nazo ni;
i. Kuwepo na idadi ndogo ya kaya ambazo zinamiliki na kutumia
vyoo bora hususani katika maeneo ambayo yameathirika zaidi na ugonjwa
huu.
ii. Kutokuwepo kwa miundombinu stahiki ikiwemo vyoo na maji katika Maeneo ya mikusanyiko kama masoko na minada kutokuwa na
iii. Wananchi kutokutii sheria zilizopo kwa kuendelea kuuza
chakula bila kuzingatia kanuni za afya na kuuza matunda yaliyokwisha
katwakatwa maeneo yasiyo salama.
iv. Utiririshaji wa maji taka kwenye vyanzo vya maji, pamoja na
kujisaidia maeneo ya wazi na pembezoni karibu na vyanzo vya maji.
v. Kuwepo kwa idadi ndogo ya watu wanaopata maji safi na salama
ya kunywa. Aidha utakasaji wa maji katika ngazi ya kaya kwa kuyachemsha
au kwa kutumia vidonge vya kutakasia bado ni changamoto kubwa.
vi. Wagonjwa wa Kipindupindu kuchelewa kufika Kambi za Matibabu.
Kutokana na changamoto hizo, napenda kuikumbusha jamii kuwa
kipindupindu ni ugonjwa unaochochewa na mazingira machafu ikiwemo
ukosekanaji wa vyoo na hivyo kuletea vinyesi vyenye vimelea kuwa chanzo
kikuu cha maambukizi, utiririshaji wa maji taka na vinyesi ambao unaweza
kupelekea kuchafuka kwa vyanzo vya maji, kutokuzingatia kanuni za afya
wakati wa utayarishaji wa vyakula na matunda, Kula vyakula au vinywaji
au pombe za kienyeji zisizoandaliwa kwa kufuata kanuni za afya na kugusa
matapishi ya mgonjwa wa kipindupindu au kwenye kitu chochote
kilichochafuliwa na kinyesi au matapishi ya mgonjwa.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inaendelea kusisitiza kwa jamii kuzingatia yafuatayo:
– Kunywa maji yaliyo safi na salama.
– Kuepuka kula chakula kilichoandaliwa katika mazingira yasiyo safi na salama.
– Kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka hasa kabla ya kula na baada ya kutoka chooni.
– Kutumia vyoo wakati wote na kutokujisaidia ovyo katika vyanzo vya maji vya mito, maziwa na mabwawa.
– Kutokutiririsha maji taka na vinyesi ili kuepuka uchafuzi wa vyanzo vya maji.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269