Na Mwaandishi wetu Washington
Wakati
hali ya kisiasa Visiwani Zanzibar ikiwa inazidi kutokota, bila kujali
theluji na baridi kali, Wazanzibari waishio nchini Canada mnamo tarehe
27 mwezi huu walifanya maandamano katika Mji Mkuu wa nchi hiyo, Ottawa
katika juhudi za kutafuta uingiliaji kati wa kimataifa katika kusaka
suluhisho la amani kwa mgogoro wa kisiasa Visiwani humo.
Mandamano ya Wazanzibari waishio nchini Canada wakiwa mwenye ofisi ya European Union Mjini Ottawa
Wazanzibari
hao waliandamana hadi kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu wa Canada kwa lengo
la kufikisha ujumbe wao kukhusiana na hali mbaya ya kisiasa huko
Zanzibar.
Akizungumza
na Swahilivilla, mmoja wa waandaaji wa maandamano hayo Bwana Zamil
Rashid alisema kuwa lengo la maandamano hayo ni kuwaunga mkono ndugu zao
Wazanzibari katika harakati za kudai demokrasia ya kweli na kupinga
hatua za kufutwa kwa uchaguzi Mkuu Zanzibar.
"Madhumuni
ya maandamano yetu yalikuwa ni kuwaunga mkono ndugu zetu wa Zanzibar
kwa mambo yaliyofanyika, na kwamba hatukubaliani nayo" alisema Bwana
Zamil na kuendelea "Wazanzibari walioko nchini Canada wanapinga jambo
hilo lilofanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na matamshi
aliyoyatoa Bwana Jecha Salim Jecha ya kufuta uchaguzi"
Aidha
maandamano hayo yalikuwa na lengo la kuiomba Serikali ya Canada
kuingilia kati katika kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa Visiwani
Zanzibar kabla hali haijawa mbaya zaidi.
Mbali
na Ofisi ya Waziri Mkuu wa Canada, Wazanzibari hao pia waliandamana
hadi kwenye Ofisi za Umoja wa Ulaya nchini humo kwa dhumuni hilo hilo.
"Vilevile
tumefikisha ujumbe wetu kwa Umoja wa Ulaya (EU) ili walishighulikie
swala hili haraka iwezekanavyo kabla hayajatokea maafa kwa Wazanzibari",
alisema Bwana Zamil.
Katika
Risala yao kwa pande zote mbili, waandamanaji hao wametoa wito wa
kutangazwa mshindi badala ya kurejewa kwa uchaguzi kama ilivyotangazwa
na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Bwana Jecha Salim
Jecha. "Tumetoa wito wa yule aliyeshinda uchaguzi atangazwe, na siyo
kurejea uchaguzi" alisisitiza Bwana Zamil.
Kwa
kufikisha ujumbe wao kwa Umoja wa Ulaya, wazanzibari hao pia walikuwa
na lengo la kutoa wito kwa nchi nyengine duniani kusaidia katika
kuupatia suluhu mzozo wa kisiaza Zanzibar, ikiwemo pia kusitisha missada
ya kiuchumi kwa Tanzania.
"Tumeziomba
serikali za Canada, Umoja wa Ulaya na nchi nyengine duniani kusitisha
misaada kwa Zanzibar na Tanzania ili kushinikiza haya mambo yaliyotokea
yasifanyike tena", alisema Bwana Zamil.
Mbali
na Wazanzibari, maandamano hayo pia yalihudhuriwa na wanafunzi kutoka
Chuo Kikuu cha Ottawa, Vyuo vyengine, Waandishi wa Khabari pamoja na
wapenda amani na demokrasia duniani.
Kufutwa
kwa uchaguzi wa Zanzibar kinyume na sheria na tangazo la kurudiwa tena
kwa uchaguzi huo kuliwakasirisha Wazanzibari wengi, na ndiyo moja ya
siri ya kujitokeza kwa wingi kwa Wanzibari katika kufanikisha maandamno
hayo.
"Wazanzibari
walijitokeza kwa wingi na tumefarajika kwa hilo", alisema Bwana Zamil
na kuongeza kuwa "Wazanzibari walikasirishwa na kitendo kile
kilichofanywa na Jecha Salim Jecha pamoja na Serikali ya CCM cha kufuta
Uchaguzi na kutaka kurudiwa mwengine"
Alifafanua msingi wa demokrasia umejikita kwenye msemo wa Kiswahili usemao kuwa "asiyekubali kushindwa si mshindani".
"Maana
ya kuwa na mfumo wa vyama vingi ni kukubali kushinda au kushindwa, sasa
ikiwa mmoja kashindwa na hakutaka kukubali kushindwa, basi itakuwa
hakuna haja ya kufanya mambo ya vyama vingi" alifafanua Bwana Zamil na
kusisitiza "Hilo ndilo lililowakasirihswa Wazanzibari, kwani wanahisi
wanadharauliwa".
Itafaa
kukumbusha kuwa mfumo wa vyama vingi ulikuweko Zanzibar kabla ya
Mapinduzi ya mwaka 1964. Kufuatia Mapinduzi hayo mfumo huo ulitoweka na
kurejea tena mwaka 1992 ambapo uchaguzi wa mwanzo ulifanyika mwaka 1995.
Chaguzi zote ambazo hufanyika kila baada ya miaka mitano visiwani humo
huwa zinagubikwa na utata huku Chama Kikuu cha Upinzani cha Wananchi
(CUF) kikidai kuporwa ushindi wake.
Katika
sherehe za kuadhimisha miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar zilizofanyika
tarehe 12 mwezi huu, baadhi ya wanachama wa Chama Tawala cha CCM
walibeba mabango yaliyokuwa na maneno ya kibaguzi kama vile kuwataka
machotara waondoke na kwamba Zanzibar ni nchi ya Waafrika.
Mabango
hayoyalikuwa kama kidonda kipya juu ya kovu mbichi na kupelekea hali
tete zaidi visiwani humo. Kukhusiana na hilo Bwana Zamil alisema "Eti
wanasema machotara wende kwao, haya yote yamewakera Wazanzibari, kwa
sababu, matusi kama yale ni matusi ya kibaguzi"
Mada
hiyo pia ilijitokeza kwenye maadamano ya jijini Ottwa ambapo baadhi ya
mabango yalibeba ujumbe uliosomeka "Ubaguzi ni saratani kwa jamii ya
Zanzibar yenye mchanganyiko wa watu wa rangi tofauti, wakati umefika
sasa wa kumaliza ubaguzi wa rangi"
Baadhi
ya mabango hayo yaliyoandikwa kwa lugha rasmi za Canada za Kiengereza
na Kifaransa, yalibeba ujumbe ukiitaka serikali ya nchi hiyo kukata
uhusiano wa Kibalzi na Tanzania, kusimamaisha misaada ya kiuchumi kwa
Tanzania na Zanzibar, kupinga kurudiwa kwa uchaguzi na badala yake
kutangazwa mshindi wa Uchaguzi uliopita, kumsuta Rais Magufuli kwa
kujishughulisha na kuzuia ubadhirifu wa fedha za taifa badala ya kuzuia
damu za Wazanzibari zisimwagike na mengineyo.
Akijibu
swali la mwandishi wetu iwapo kuna majibu yoyote kwa risala yao, Bwana
Zamil alisema "Wamesema kuwa watalishughulikia haraka iwezekanavyo kabla
mambo hayajaharibika zaidi Zanzibar".
Aliongeza
kuwa Afisa wa Umoja wa Ulaya aliepokea risala yao aliahidi kuifanyia
kazi mara moja. "Amesema leo hii ataisambaza kwa wanachama wote wa Umoja
huo ile risala ili waisome na kuchukua hatua za haraka zaidi"
alisisistiza Bwana Zamil.
Kukhusu
ukimya wa Rais wa Tanzania juu ya yale yanayoendelea Zanzibar, Bwana
Zamil amlimtolea wito Dkt John Pombe Magufuli kuushughulikia mzozo wa
Zanzibar ili kuepusha janga la kibinadamu.
"Rais
wa Tanzania ana jukumu, ni lazima asimamie haki na usalama wa
Wazanzibari wote, na Wazanzibari lazima haki yao aisimamie, siyo kama
hivi kukaa kimya" alisihi mwanaharakati huyo, na kuongeza, "Hii
inaonesha kama kwamba anakubaliana na yale yanayotokea Zanzibar"
Kwa
upande mwengine, mwanaharakati huyo aliwatolea nasaha WanaCCM wa
Zanzibar kwenda na wakati na kuwa washindani wa kweli, huku wakijua
demokrasia ni kubadilishana madraka kwa njia za amani.
"Zanzibar
ni mali ya Wazanzibari wote na wala siyo milki ya CCM. Kwa hiyo
aliyeshindwa akubali kushindwa, na aliyeshinda wampongeze ili watu
waishi kwa hali ya mapenzi na amani kuliko kusubiri mpaka watu
kupigana, mambo ambayo yataleta madhara makubwa", alisema Bwana Zamil na
kuonya "...inaweza kufika mahala watu kufikishana kwenye Mahakama za
Kimataifa"
Alitoa
ukumbusho kwa viongozi walioko Madarakani Zanzibar kuwa kinga ni bora
kuliko tiba, na kusema "Ningeiomba Serikali isikubali kufika huko"
Halkadhalika alitoa wasia maalum kwa Rais wa Zanzibar Alhaj Ali Mohammed
Shein kwa kusema "Namuusia Rais Shein asikubali kufikishwa mahala
ambapo patakuja kumletea khasara hapa dunianiu na huko Akhera"
Maandamano
ya Wazanzibari nchini Canada yanakuja kufuatia yale ya Jumuiya ya
Wazanzibari waishio nchini Marekani (ZADIA) yaliyofanyika Ikulu ya nchi
hiyo (White House), na kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New
York.
Maandamano
kama hayo pia yalifanyika nchini Uingereza na sehemu nyengine za Ulaya.
Kwa muqtadha huu Bwana Zamil amewatolea wito Wazanzibari popote
Ulimwenguni kuchukua hatua za kushinikiza kupatikana ufumbuzi wa amani
kwa mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar.
"Nawashauri
Wazanzibari walioko katika sehemu nyengine duniani waungane na
Wazanzibari wenzao ili kupigania demokrasia ya kweli katika nchi yao"
alishauri, na kunasihi "Na katika kufanya hivyo, wapiganie kwa njia za
amani haki na usawa"
Vile
vile, Bwana Zamil alitoa shukrani maalum kwa Polisi wa Canada kwa
ushirikiano wao mzuri tangu mwanzo mpaka mwisho wa shughuli yao.
Ikumbukwe
kwamba, mgogoro wa sasa wa kisiasa Zanzibar uliripuka kufuatia Uchaguzi
Mkuu uliofanyika tarehe 25 Oktoba mwaka jana baada ya uamuzi wa
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Bwana Jecha Salim Jecha wa
kutangaza kuufuta uchaguzi wa Zanzibar na matokeo yake kwa madai ya
kuwepo kwa kasoro nyingi za uchaguzi khususan Kisiwani Pemba ambako
ndiko kwenye ngome kuu ya Chama cha upinzani cha CUF.
Wataalamu
wa maswala ya Sheria za Zanzibar wanaona kuwa hatua hiyo ya Bwana Jecha
haikuwa ya kisheria, na wasimamizi wa uchaguzi, wachunguzi, wadadisi na
wachambuzi wa nje na ndani ya nchi waliuelezea uchaguzi huo kuwa
ulifanyika katika mazingira huru na ulikuwa wa haki.
Inaaminika
kuwa hatua ya kufutwa kwa uchaguzi huo ilikuja baada ya kubainika kuwa
mgombea wa Urais kwa tiketi ya Chama cha CUF Maalim Seif Sharif Hamad
alikuwa amemtangulia mpizani wake mkubwa aliyekuwa akitetea kiti chake
Rais Ali Mohammed Shein.
Kufuatia
kufutwa kwa uchaguzi huo, vikao vya siri vya mzungumzo vilifanyika kwa
zaidi ya miezi miwili katika Ikulu ya Zanzibar vikiwashirikisha Rais Ali
Mohammed Shein, Makamo wake wa Kwanza Maalim Seif Sharif Hamad, Makamo
wa Pili Balozi Seif Ali Idd pamoja na Marais wastaafu wa Zanzibar,
Mabwana Amani Karume, Salmin Amour na Ali Hassan Mwinyi.
Wakati
vikao hivo vya siri vikiwa vinaendelea, mitaani kukazaliwa msamiati
mpya uliojulikana kwa jina la "drips" zikiwa ni tetesi kuhusu kile
kinachoendelea katika mazungumzo hayo.
Hatimaye
mfuko wa drips ukapasuliwa baada ya mazungumzo hayo kushindwa kufikia
mwafaka, na Bwana Jecha kujitokeza tena na kutangaza kuwa uchaguzi
utarudiwa tarehe 20 Machi mwaka huu na hivyo kupelekea mtafaruku zaidi
wa kisasa Visiwani humo.
Kufuatia
uamuzi huo, chama cha CUF kimesema kuwa hakitoshirki kwenye uchaguzi wa
marudio, na kushikilia msimamo wake wa kutaka matokeo ya uchaguzi wa
Oktoba yatangazwe, kwa vile uchaguzi ulikuwa huru na wa haki.
Hali
ya mgando wa kisiasa Zanzibar imepelekea athari mbaya za kiuchumi na
kijamii, huku mfumko mkubwa wa bei khususan bidhaa muhimu kama vile
chakula ukiarifiwa kufikia zaidi ya asili mia 10
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269