Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa
Mkoa wa Njombe Dkt. Rehema Nchimbi, kufuatia kifo cha ghafla cha Mkuu
wa Wilaya ya Njombe Bi. Sara Dumba, Kilichotokea jana jioni tarehe 21
Machi, 2016.
Bi. Sara Dumba aliugua ghafla
kuanzia jana mchana na baadaye kukimbizwa katika hospitali ya Mkoa wa
Njombe (Kibena), ambako wakati akipatiwa matibabu alifariki dunia majira
ya saa moja za jioni.
Katika salamu hizo Rais Magufuli
ameelezea kushitushwa na kifo cha ghafla cha Bi. Sara Dumba, ambaye
amesema alimfahamu kwa uchapakazi wake, uaminifu na uadilifu katika
utumishi wa umma na katika uongozi.
“Nimeshitushwa sana na kifo
cha Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi. Sara Dumba, kwa mara nyingine Taifa
limempoteza mtu muhimu ambaye mchango wake ulikuwa bado unahitajika” amesema Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli amebainisha kuwa
Marehemu Sara dumba atakumbukwa kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuhimiza
maendeleo ya wananchi, hususani katika kilimo na ufugaji, kuhimiza
nidhamu ya utumishi serikalini na kuwatetea wananchi wa hali ya chini
wakati wote wa majukumu yake ya ukuu wa wilaya.
Rais Magufuli amesema anaungana
na familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na
msiba huu mkubwa, katika kipindi hiki kigumu na pia amewataka wote kuwa
na subira na uvumilivu.
Amemuombea kwa Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi, Amina.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
22 Machi, 2016
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269