Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto,DK.Hamisi Kigwangalla akizungumza katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu ukimwi unaoendelea hapa Umoja wa Mataifa, |
Na Mwandishi Maalum, New York
Mkutano wa nganzi ya juu kuhusu
ukimwi jana ( alhamis) uliingia
katika siku yake ya pili ambapo viongozi
mbalimbali wakiwamo Mawaziri na Naibu waziri wanaohusika na masuala ya afya wameendelea
kuelezea nini ambacho nchi zao
zinatekeleza katika kukabili na kudhibiti
maambukizi mapya ya virusi vinavyo sababisha ukimwi pamoja na
huduma wanazopatiwa watu ambao wamekwisha kuathirika na kuugua.
Mmoja ya
nchi ambayo iliwasilisha
mafanikio, changamoto na
mwelekeo wa baadaye katika kukabiliana
na janga
la ugonjwa wa ukimwi, ugonjwa
ambao jumuiya ya kimataifa umejiweka
lengo la kuutokomeza ifikapo mwaka 2030
ili kuwa ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Juhudi za Tanzania dhidi ya Ukimwi, zilielezwa
na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dr. Hamis A Kigwangalla (Mb).
Ambaye katika maelelezo yake, amesema, Tanzania inaamini kuwa inawezekana kufikia hali ya kutokuwa na
maambukizi mapya, kumaliza
ubaguzi na unyanyapaa, na kuwa na
kiwago sifuri cha vifo vinavyohusiana na ukimwi fikapo mwaka 2030.
Hata hivyo anasema, ili kufikia
hatua hiyo au mafanikio hayo, mambo
kadhaa yanapashwa kufanyika, yakiwamo ya uimarishwaji wa elimu ya kinga, vijana na
jumuiya kwa ujumla kufundishwa mbinu
za kuepukana na tabia hatarishi ambazo zinachangia ongozeko la waathirika na kuhakikisha upatikanaji
kirahisi wa za dawa na ambazo
zitakuwa za gharama nafuu.
Kwa mujibu wa Naibu
Waziri ambaye anaongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano
huu, amekwenda mbali zaidi kwa
kusema pia patahitajika kupunguza
vifo vitokanavyo na ugonjwa wa Kifua
Kikuu kwa watu wanaoishi na virusi vya
ukimwi, kujadili masuala ya jinsia pamoja na
mila na tamaduni, kutenga
raslimali za kutosha kwaajili ya watu
wenye mahitaji wakiwamo vijana, kuwa na
viwanda vitakavyoweza kuzalisha
dawa.
Akizungumza baadhi ya mafanikio
ambayo Tanzania imekwisha kuyafikia katika kukabili tatizo la ukimwi, Naibu Waziri ameyataja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni pamoja
na kupunguza maambukizi mapya
kutoka 140,000 mwaka 1990 hadi kufikia
63,000 mwaka 2014. Vile vile vifo vitokanavyo au vinavyosaabishwa na ukimwi
pia vimepungua kwa asilimi 40 katika
kipindi hicho.
Akaeleza pia kwamba hata watu wanaopatiwa huduma ya matibabu nayo imeongezeka kufikia asilimia 60
huku ongezeko likiwa kwa watoto na hasa baada ya kupitisha mpango unaotambulika kama Option B+ miaka sita iliyopita.
Kuhusu kupungua kwa raslimali fedha hususani kutoka kwa wafadhili, Dr. Kingwangalla, amesema katika
kukabiliana na changamoto hiyo, na
kwa kuzingatia wito wa jumuiya ya kimataifa kupanua wigo wa mapato ya
ndani, serikali ya Tanzania ilianzisha Mfuko wa ukimwi, (AIDS
Trust Fund) mfuko anaosema hadi sasa
serikali ndiyo imekuwa mchangiaji mkuu, ingawa pia kwamba sekta binafsi nayo inatazamiwa kuchangia.
Akasema sehemu
au nusu ya fedha hizo (55%) itakwenda kusaidia upatikanaji wa huduma na
kuongeza kuwa juhudi hizo za serikali pia zimesaidiwa na ushirikiano
baina ya Tanzania na nchi
nyingine rafiki pamoja na mashirika ya
kimataifa na akatumia fursa hiyo kuwashukuru wale wote ambao wanachangia juhudi za serikali.
Kuhusu
mipango mingine ambayo serikali
inaendelea nayo , Naibu waziri
alikuwa na haya ya kueleza “ baada ya
kuwa tumeanza utaratibu wa kupima na kutibu kwa baadhi ya wilaya chache
nchini, tunakusudia kuisambaza huduma
hiyo lakini itakuwa ni kwa hatua ili kutoa nafasi ya kuwajengea uwezo watoaji wa
huduma ya afya, kuhuisha mifumo ya usambazaji wa vifaa
ikiwa ni pamoja ushiriki wa jamii ili iweze
kupokea na kuukubali mfumo huu mpya wa utoaji wa huduma” ameeleza Naibu Waziri.
Akasisitiza zaidi kwa kusema
ingawa ugonjwa wa ukimwi umeendelea kuwa changamoto kubwa kwa maendeleo ya nchi ambapo
inakadiriwa watu 1.5 milioni wameathirika, huku mzingo mkubwa
ukiwaelemea wanawake na vijana hasa
watoto wa kike, serikali ya tanzania
itaendelea na jitihada zake za kuhakikisha inafikia lengo la kutokuwa na maambukizi mapya, kutokomeza unyanyapaa na ubaguzi, na vifo
vinatokanavyo na ukimwi.
Katika hatua nyingine amesema
ili kutorudisha nyuma mafanikio ambayo
Tanzania imeyafikia hadi sasa pamoja na
nchi nyingine kusini mwa Jangwa la Sahara Jumuiya ya
Kimataifa inaombwa kusaidia jitihada zinazofanywa na serikali za nchi hizo
za kuwa na mapato yake yenyewe ya
kugharamia huduma za afya kwa wagonjwa
wa ukimwi na pamoja na huduma nyinginezo badala ya kuziachia kabisa jukumu hilo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269