Augustine Mrema |
Dar es Salaam
WAZIRI wa zamani wa mambo ya ndani ya nchi, Augustino Mrema amewataka Watanzania kuyapuuza maandamano ya Septemba Mosi mwaka huu yaliyoandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na badala waendelee na shughuli za ujenzi wa Taifa.
Mrema alisema hakuna haja ya kufanya maandamano Septemba Mosi kwani hayana faida yoyote kwa taifa badala yake wananchi wa kawaida ndio watakaoathirika.
Akizungumza katika mahojiano maalum na mwandishi wa habari hii leo Jijini Dar es Salaam, Mhe. Mrema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Misamaha kwa Wafungwa (Parole) alisema mikutano ya hadhara na maandamano yasiyokwisha kila kukicha yatasababisha wananchi wasifanye kazi.
Nchi yetu ni maskini hivyo tunahitaji wananchi wafanye kazi kwa bidii” alisema Mrema. Alisema iwapo CHADEMA wataona wameonewa ni vyema watumie njia za mazungumzo au ikibidi kwenda mahakamani badala ya kufanya maandamano ambayo yanaweza kusababisha vurugu na kuharibu amani na utulivu wa nchi.
Aliwataka Watanzania kukumbuka maandamano ya mwaka 2001 yaliyoitishwa na Chama cha Wananchi (CUF) huko Zanzibar ambapo watu kadhaa waliuwawa na mamia kukimbilia uhamishoni nchini Kenya na Somalia.
Akizungumzia kuhusu utendaji kazi wa Serikali ya Awamu, Mhe. Mrema alimpogeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa hatua yake ya kurejesha maadili na miiko ya utumishi kwa watumishi wa umma nchini hali iliyosaidia kurejesha uwajibikaji wa Serikali kwa wananchi.
Mrema alisema tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu Tano, kumekuwepo na mabadiliko kwa watendaji wa umma katika ngazi mbalimbali za kimamlaka ukitofautisha na miaka ya nyuma ambapo baadhi ya watendaji walikuwa wakifanya kazi kwa mazoea.
“Viongozi wengi wa umma walikuwa wakifanya kazi kwa mazoea bila kujali wajibu wao na wala hakukuwa na uwajibikaji cha kusikitisha mamlaka husika zilikuwa haziwachukulii hatua za kinidhamu, hivyo viongozi wa umma badala ya kuwatumikia wananchi wakawa wanatumikia matumbo yao” alisema Mrema.
Mrema alisema Rais Magufuli ameanza kutekeleza kwa vitendo ahadi yake aliyoitoa kwa wananchi ya kuwaondoa madarakani viongozi wazembe na wasiowajibika na wasiokuwa na uwezo wa kufanya kazi katika kuwatumia wananchi.
Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inastahili pongezi kwa hatua inazochukua katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa na ufisadi ikiwemo uanzishwaji wa Mahakama ya Mafisadi nchini, kwani hakuna maendeleo yatakayoweza kupatikana katika nchi pasipo na kupiga vita rushwa.
Mrema alisema ni wajibu wa kila mwananchi kuichukia rushwa kwa vitendo ikiwemo kuwafichua hadharani kikundi cha watu kinachojihusisha na rushwa kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia Tanzania kupiga hatua kubwa za maendeleo.
“Kama mnavyokumbuka mimi nilifukuzwa kazi serikalini kwa sababu ya kupinga ufisadi ambao kwa wakati ule ulikuwa umekithiri serikali, ivyo nilichokuwa nikikipigania mimi ndicho anachifanya Rais Magufuli” alisema Mrema.
Akizungumzia kuhusu hatua ya Serikali ya Awamu ya Tano kuhamishia shughuli zake Mjini Dodoma, Mrema alipongeza uamuzi huo kwani kiulinzi na kiusalama Dodoma ni pazuri zaidi kuliko Dar es Saalam kwani ni katikati ya nchi.
“Dodoma panafaa sana kiulinzi na usalama kwa kuwa ni vigumu kwa adui watoke baharini wafike hadi Dodoma kabla hawajadhibitiwa” alisema Mrema.
“Kuhusu ubora wa miundombinu ya Mkoa wa Dodoma Mrema alisema Mkoa huo unafikika kirahisi zaidi kwa wananchi waishio mikoa ya pembezoni na mipakani kufika Dodoma kuliko ilivyo Dar es salaam ambayo iko Mashariki kabisa ya nchi” alisema Mrema.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269