Tume ya Uchaguzi katika Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo, imetangaza kuahirishwa uchaguzi wa rais nchini
humo hadi mwezi Julai 2017.
Habari hiyo ilitangazwa, Agosti 20, 2016 na Mwenyekiti wa Tume
ya Uchaguzi ya Kongo, Corneille Nangaa na kuongeza kuwa, shughuli ya
uandikishaji majina ya wapiga kura iliyoanza mwezi Machi mwaka huu,
itahitajia muda wa miezi 16 hadi kukamilika. Awali mahakama ya juu ya
Jamhuri ya Kidokrasia ya Congo ilitangaza kuwa iwapo serikali ya Rais
Joseph Kabila haitaweza kuanda uchaguzi wa rais katika wakati
ulioainishwa basi kiongozi huyo anaweza kubakia madarakani hadi wakati
wa kufanyika uchaguzi mkuu. Kabila alishika hatamu za kuiongoza Congo
mwaka 2001 baada ya mauaji ya baba yake, Laurent Kabila, na kisha
akashinda uchaguzi wa rais uliofanyika mwaka 2006. Kwa mujibu wa katiba
ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rais Joseph Kabila
haruhusiwi kugombea tena kiti hicho baada ya kuhudumia vipindi viwili
vya miaka mitano mitano.
Migogoro ya kisiasa imekuwa ikishuhudiwa nchini humo kwa muda sasa.
Kabla ya hapo viongozi wa chama tawala walikuwa wametangaza kuwepo
uwezekano wa kuahirishwa kwa uchaguzi wa rais kutokana na upungufu wa
bajeti na kadhalika kuchelewa shughuli ya uandikishaji wa majina ya
wapiga kura, suala ambalo lilibua wimbi la malalamiko ya wapinzani
nchini. Wapinzani wanamtuhumu Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo kwamba amechelewesha zoezi hilo kwa lengo la
kusalia zaidi madarakani. Kabla ya hapo Etienne Tshisekedi, kiongozi wa
chama kikuu cha upinzani kinachoitwa 'Umoja kwa ajili ya Demokrasia na
Maendeleo ya Kijamii' (UDPS) alimtaka rais huyo kung'atuke madarakani na
kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi mkuu kufikia mwishoni mwa mwaka
huu. Kadhalika mzee Tshisekedi alimtaka rais huyo kuondoka madarakani
tarehe 20 Disemba mwaka huu kama ilivyopangwa, hatua ambayo
ingetanguliwa na uchaguzi wa rais.
Mwanasiasa huyo aliitaja hatua ya kuahirisha uchaguzi kuwa ni uhaini
mkubwa huku akimuonya Rais Kabila kunako kujaribu kugombea muhula wa
tatu kwenye uchaguzi ujao. Licha ya kwamba wiki chache zilizopita
kulikuwa kumepangwa kufanyika mazungumzo ya kitaifa kati ya wapinzani na
chama tawala kwa ajili ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa nchini
humo, hata hivyo ghafla na katika hali ambayo haikutarajiwa mpatanishi
wa Umoja wa Afrika katika mazungumzo hayo ameibuka na kutangaza
kuahirishwa kwake. Edem Kodjo, Waziri Mkuu wa zamani wa Togo na
mpatanishi wa Umoja wa Afrika katika mazungumzo ya umoja wa kitaifa
nchini Kongo DR, ametangaza kuwa kuahirishwa mazungumzo hayo, kumetokana
na pande husika kutokuwa na maandalizi kamili ya ushiriki wao kwenye
mazungumzo. Kodjo ameongeza kuwa, mazungumzo ya kitaifa ndiyo njia pekee
ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo kwa maslahi ya taifa.
Pamoja na hayo wapinzani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,
hawakuwa tayari kushiriki mazungumzo hayo. Kuachiliwa huru wafungwa wote
wa kisiasa kutoka jela za serikali, lilikuwa sharti la wapinzani kwa
ajili ya kushiriki katika mazungumzo hayo na serikali ya Rais Joseph
Kabila. Kufuatia uamuzi wa kuahirishwa uchaguzi wa rais, Jumamosi ya
jana muungano wa vyama vya upinzani ulitangaza rasmi upinzani wake wa
kufanya mazungumzo na Rais Joseph Kabila kuhusiana na suala zima la
uchaguzi. Aidha umoja huo umetangaza mgomo wa nchi nzima hapo siku ya
Jumanne katika kulalamikia suala hilo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269