Breaking News

Your Ad Spot

Aug 26, 2016

TATIZO LA CHADEMA WANAPIMA HOMA KWA KIGANJA!

Na Daniel Mbega
NILIWAHI kuandika wakati fulani kwamba " UKWELEI WA MWANASIASA NI JINA LAKETU" lakini wakatokea watu wengi kunikosoa, wakipinga uchambuzi wangu huo na wengine wakinitisha kwa maneno kwa sababu tu nilikuwa nimekisema kile ambacho wao ama wapendwa wao hawakupenda kisemwe hata kama kiko wazi.


Ilikuwa ni wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu 2015 wakati nilipozichambua kauli za mawaziri wakuu wa zamani – Edward Lowassa na Frederick Sumaye – waliokwenda kutafuta hifadhi Chadema baada ya kuona ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) hawana nafasi ya kwenda Ikulu tena.

Nilisema kwamba wanasiasa hao wamefuzu katika sanaa. Bora Lowassa tunajua alisomea sanaa, lakini Sumaye alisomea kilimo!

Baada ya kukimbilia Chadema, kwa nyakati tofauti wanasiasa hao walitoa kauli zilizodhihirisha kwamba ukiwa kwenye siasa lazima uwe mwongo, lakini wakasahau kwamba, ukiwa muongo daima usiwe msahaulifu.

Kabla ya kwenda Chadema na kuteuliwa kuwa mgombea urais, Lowassa alipata kumsifu Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete akisema: “Rais Kikwete ni Visionary Leader ana uwezo wa kuona mbali”, lakini alipotua tu Chadema na kuvikwa joho la Ukawa, akasema: “Rafiki yangu Jakaya Mrisho Kikwete ameuharibu uchumi wan chi hii”.

Yako mengi aliyowahi kuyasema akiwa ndani ya CCM ikiwemo kuapa kwamba asingetoka ndani ya chama hicho na ikiwa kuna mtu hamtaki, basi aondoke yeye.

Sumaye ndiye aliyenishangaza kabisa na nitaendelea kumshangaa daima katika maisha yangu. Juni 2, 2008 alinukuliwa na gazeti la Tanzania Daima akisema “Urais basi”, kwamba hakuwa na nia ya kuwania tena nafasi ya urais hata itakapofika mwaka 2015, na badala yake anataka kuwa mtu wa msaada kwa nchi za Afrika, ili ziweze kujikwamua katika lindi la umaskini. Maneno haya aliyasema kwenye mkutano na waandishi wa habari pale kwenye Hoteli ya Protea, zamani Court Yard, jijini Dar es Salaam.

Lakini ghafla bin vuu akajitokeza kuwa miongoni mwamakada 42 wa CCM waliojitokeza kutaka kupokea kijiti cha Jakaya Kikwete. Wakati akiwa na harakati za kuwania urais, alipata kukaririwa akisema: “Endapo CCM itampitisha Lowassa kugombea urais mimi nitahama chama.” CCM haikumpitisha Lowassa, wala yeye hakupitishwa. Akabakia huko kwa muda na baada ya kutafakari akahama kumfuata Lowassa Chadema! Tena basi akateuliwa kuwa Meneja wa Kampeni wa mtu aliyedai hafai kuwa rais akiwa CCM!

Baada ya kwenda Chadema, Sumaye huyo huyo katika uzinduzi wa kitaifa wa kampeni za Ukawa, ndiye aliyempigia kampeni Lowassa akisema: “Lowassa anastahili urais yeye ndiye Jemedari wetu”.

Kwa miaka kadhaa sasa, Chadema imejipambanua kwamba ni chama kinachopinga ufisadi na kiliweza kujijengea sifa na kuaminiwa na wananchi kwa msimamo huo, huku kikiendesha kampeni nchi nzima kupinga ufisadi pamoja na suala la kusamehe kodi ambalo lilikuwa linaikosesha serikali mapato makubwa.

Waliahidi kwamba, mara watakapoingia madarakani – kama wangefanikiwa – wangeanza kusafisha mafisadi wote na kuhakikisha kodi inakusanywa ili nchi isiwe tegemezi.

Kwa bahati mbaya kura za Lowassa ‘hazikutosha’, hivyo CCM imeendelea kushika hatamu ya uongozi wa taifa hili chini ya Rais John Pombe Joseph Magufuli, ambaye naye kwa kiasi kikubwa katika kampeni zake aliahidi kupambana na ufisadi, kubana matumizi na kuigeuza nchi kuwa ya uchumi wa viwanda, huku akienda mbali Zaidi kwa kusema kwamba angeanzisha mahakama ya kuwashughulikia majizi na mafisadi.

Baada tu ya kuingia madarakani akaanzisha ‘Operesheni ya Kutumbua Majipu’ kwa kusafisha uozo wote uliokuwa ukipigiwa kelele ambao uliota mizizi kuanzia kwenye rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka pamoja na uzembe na kufanya kazi kwa mazowea.

Tulishuhudia namna serikali ilivyofanikiwa kukusanya trilioni kadhaa kwa miezi mitano ya mwanzo na inaendelea na kasi hiyo hiyo, huku Rais Magufuli akifanya kile ambacho hakikutarajiwa kwa kuwakamata wafanyabiashara wote wakubwa ambao walikwepa kodi wakati wa awamu ya nne na wakalipa.

Watendaji wa serikali wengi wakaondolewa na baadhi yao kesi zao ziko mahakamani kutokana na kutumia madaraka yao vibaya yaliyoikosesha serikali mapato huku wananchi wakiendelea kuogelea kwenye tope la umaskini.

Kwa hiyo kelele hizo hazikuwa za Chadema tu, bali hata Dk. Magufuli aliziona akiwa CCM na ndiyo maana alipopata dhamana ya kuwatumikia Watanzania akaamua kupambana nazo kwa vitendo bila kumuonea haya yeyote.

Lakini pamoja na jitihada hizo ambazo zilikuwa kero kubwa kwa wananchi na mtaji wa kisiasa wa wapinzani, Chadema wanazibeza na ikafikia mahali viongozi na baadhi ya mawakili wa chama hicho wakaanza kuwatetea wale wote ‘waliotumbuliwa’ na kufikia hatua ya kuahidi kwamba wangeweza kwenda kuwatetea mahakamani.

Kwa maana nyingine, Chadema wanaonekana kukerwa na utendaji uliotukuka wa Rais Magufuli ambaye ameimarisha nidhamu ya kazi na kuhakikisha rasilimali za Watanzania haziendi mifukoni mwa wachache.

Hapa ndipo panapoanzia figisu zote zinazofanywa sasa na Chadema kiasi cha kuanza kumwita Rais Magufuli ni dikteta bila kubainisha udikteta wake ni kwa vile amepambana na ufisadi au kwa sababu amekubalika kwa wananchi kiasi kwamba wapinzani hawana hoja ya msingi ya kuikosoa serikali.

Kitendo cha Chadema kupinga kila jambo linalofanywa na serikali ni ukaidi ambao hauna maana yoyote wala tija kwa taifa na kwa hatua yao ya sasa ya kuitisha maandamano ya kupinga hicho wanachokiita ‘ufisadi’ ni kumjaribu Rais Magufuli kama ‘atawafanya nini’.

Hapa niseme tu kwamba, Chadema wanapima homa kwa viganja, jambo ambalo ni la hatari. Huwezi kusema mtu ana homa kwa sababu tu kwa kutumia kiganja unaona joto la mwili limepanda, utakuwa unakosea.

Wakati wa utawala wa Jakaya Kikwete, ni Chadema hao hao waliomkosoa rais kwamba ‘anacheka cheka’ na wengine wakamwita ‘Marco Polo’ au ‘Vasco da Gama’ kutokana na kusafiri sana ughaibuni.

Leo amekuja mtawala anayefanya kazi kwa vitendo wanamwita dikteta, kwa sababu tu ameweza kupambana na changamoto nyingi zilizoiyumbisha serikali huko nyuma. Sasa wanataka nini?
Kama mtawala aliyepita alikuwa anacheka na wakamkejeli walivyotaka, sasa huyu amenuna, hacheki wala nini, yeye anapiga kazi tu!

Chadema wamekuwa kama ‘mtoto wa kufikia’ ambaye hata ujitahidi kumtunza namna gani, hawezi kuridhika na atafanya visa vingi tu kumgombanisha baba na mama!

Tena hawana tofauti na ‘ndugu wa mume’ ambao watamkosoa mke wa ndugu yao hasa ikitokea kwamba ‘hakuwa chaguo lao’, na siyo ajabu wakamwambia ndugu yao ‘mwache mwanamke huyu hakufai, mchoyo, au hata mchawi!’

Ndivyo wanavyofanya Chadema kwa serikali ya awamu hii kwa sababu wao walikuwa na matumaini kwa asilimia 200 kwamba wangeingia Magogoni baada ya kumpata ‘mchezaji’ Lowassa katika timu yao na kutumia msururu wa wafuasi wa mwanasiasa huyo aliotoka nao CCM.

Kwa kuwa ushindi wa Dk. Magufuli umewanyima fursa ya kuwa mawaziri, ma-RC, ma-DC, mabalozi na kadhalika, sasa wanafanya kila namna kumtoa kasoro ili aonekane hafai, jambo ambalo lina malengo hasi kwa taifa letu.

Kukwamisha jitihada za serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo ni kosa kubwa na kukaidi mamlaka iliyopo ni kosa pia kwa sababu hata vitabu vya dini vinatuagiza tuheshimu mamlaka za dunia kwa sababu “Mamlaka zote zimewekwa na Mungu”, hata kama ulikwenda kupanga foleni kupiga kura.

Moma ni nyoka mpole sana, lakini akiamua kushambulia hagongi kama nyoka wenyine, bali anang’ata na kuondoka na nyama na sumu yake ni kali kiasi kwamba pale alipopang’ata huvimba na kubadilika rangi – matokeo yake ni kifo.

Rais Magufuli alishaonya kwamba watu wasimjaribu kwa sababu kamwe yeye hajaribiwi, maana yake ni kwamba Chadema wasithubutu kumjaribu kwa sababu atakapochukua hatua itakuwa ni hatari.

Hivi siyo vitisho wala siyo udikteta, kwa sababu wakati mwingine kiongozi inabidi ufanye lile linalofaa kwa maendeleo ya taifa lako na kitendo cha kuzuia mikutana na maandamano ni katika kuwafanya wananchi waendelee na shughuli zao za uchumi badala ya kuchelewa siasa – tena zile za kupinga maendeleo.

Wakati mwingine kuna haja ya kuwapuuza wanasiasa wa aina hii kwa sababu kwa kiasi kikubwa wanachelewesha maendeleo.
Ni maoni yang utu.
0656-331974

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages