Beit Al Jaib, Zanzibar |
Ufalme wa Oman umeonyesha nia ya kukarabati majengo ya makubusho ya kale ya Beit Al Jaib maarufu kama “ House of Wonders” yaliyopo mjini Unguja, Zanzibar.
Nia hiyo imeonyeshwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Yusuf bin Alawi bin Addullah, katika mazungumzo yake, alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Augustine Mahiga na kufanya mazungumzo maalum wakati wa mkutano wa 71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambapo Mawaziri hao walikuwa wakiongoza ujumbe wa nchi zao.
Katika mazungumzo ya mawaziri hao ambayo yalijikita katika uimarishwaji wa uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo baina ya Oman na Tanzania, pamoja na mambo mengine, Waziri Mahinga aliomba serikali ya Oman kuangalia uwezekano wa kuanzishwa kwa mradi wa kutunza mambo ya kale zikiwamo nyaraka muhimu zinazohusu uhusiano baina ya nchi hizo mbili.
Waziri Mahiga alimweleza Waziri huyo wa Omani kwamba, moja ya majengo yenye nyaraka za kumbukumbu muhimu za za kihistoria ni lile la Beit Al Jaib ( House of wonders) lililokuwa Ikulu ya Utawala wa Kifalme, Zanzibar.
Alisema jego hilo lenye makubusho yaliyosheheni historia ya uhusiano na ushirikiano kati ya Zanzibar na Sultanate of Oman na Afrika Mashariki kwa Ujumla limekuwa chakavu kutokana na kuwa la mda mrefu sasa.
Na kutokana na historia hiyo na umuhimu wa jengo hilo ambalo limejengwa mwaka 1883, Waziri ameiomba Serikali ya Oman kuangalia uwezekano wa kulihifadhi ili pia liendelee kuwa kivutio kikubwa cha utalii.
Akijibu ombi hilo na mengine yaliyowasilishwa na Waziri Mahinga, Waziria wa Mambo ya Nje wa Oman, Yusuf bin Alawi bin Addullah amemtaka Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuandaa andiko na kuliwasilisha katika Serikali ya Oman ili pendekezo hilo liweze kufanyiwa kazi pamoja na mapendekezo mengine.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Augustine Mahiga amekuwa na kuwa na mazungumgo na Linda Thomas Greenfield, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayehusika na masuala ya Afrika.
Mazungumzo ya Waziri Mahinga na Linda Greenfield yalijikita zaidi katika uhusiano na ushirikiano baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Marekani.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Augustine Mahiga na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sultanate of Oman Yusuf bin Alawi bin Abdullah wakizungumzia kuhusu namna ya kuendelea kuimarisha uhusiano mzuri baina ya nchi hizo mbili.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269