Breaking News

Your Ad Spot

Jan 29, 2017

TANZANIA NA ZAMBIA ZASAINI MAKUBALIANO YA KUANZISHA KITUO CHA PAMOJA CHA FORODHA

tz1
Makatibu Wakuu kutoka Tanzania na Zambia wanaohusika na masuala ya fedha, biashara na viwanda wakiwa katika kikao cha kupitia nyaraka mbalimbali za mikataba ya namna ya kuendesha Kituo cha Pamoja cha Mpakani, Tunduma/Nakonde, uliofanyika Jijini Mbeya. Kutoka kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Prof. Adolf Mkenda, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban, Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Uwekezaji wa Zambia, Kayula Siame, Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Miundombinu wa Zambia, Mhandisi Charles Mushota, na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais wa Zambia, Bright Nundwe.
tz2
Baadhi ya wataalamu wa sheria na masuala ya kodi kutoka Tanzania wakifuatilia kwa makini majadiliano na maboresho ya mikataba na nyaraka mbalimbali zilizosainiwa kwa ajili ya kuanzishwa rasmi kwa Kituo cha Pamoja cha Mpaka wa Tunduma/Nakonde cha nchi za Tanzania na Zambia, Jijini Mbeya.
tz3
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda (Kulia), akisisitiza jambo wakati wa kikao kilichowahusisha Makatibu Wakuu wa baadhi ya wizara zinazohusika na masuala ya Fedha, Biashara, viwanda na.....
Uwekezaji kutoka nchi za Tanzania na Zambia, uliofanyika Jijini Mbeya, wakijadili namna bora ya kuanzisha Kituo cha Pamoja katika mpaka wa nchi hizo mbili wa Tunduma na Nakonde
tz4
Baadhi ya wataalamu wa sheria na masuala ya kodi kutoka Tanzania wakifuatilia kwa makini majadiliano na maboresho ya mikataba na nyaraka mbalimbali zilizosainiwa kwa ajili ya kuanzishwa rasmi kwa Kituo cha Pamoja cha Mpaka wa Tunduma/Nakonde cha nchi za Tanzania na Zambia, mkutano uliofanyika katika eneo la Vwawa, mkoa wa Songwe.
tz5
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban (kushoto), na Mwenyekiti Mwenza wa Kikao cha kupitia Mikataba na nyaraka mbalimbali za uanzishwaji wa Kituo cha Pamoja na Mpakani (One Stop Border Post) ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Uwekezaji wa Zambia, Bi. Kayula Siame, wakiangalia Mkataba huo kabla ya kusainiwa.
tz6
Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, Bw. Jocktan Kyamuhanga (kushoto), Mtaalamu kutoka idara ya Sera Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Zuberi (katikati) na Naibu Kamishna wa TRA Bw. Charles Kichere, wakiangalia kwa makini nyaraka za kuanzishwa kwa Kituo cha Pamoja cha Mpakani kabla ya mikataba hiyo kusainiwa ili kuanzishwa rasmi kwa kituo hicho cha Tunduma/Nakonde, ifikapo Februari Mosi, 2017.
tz7
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda (kushoto) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Uwekezaji wa Zambia, Bi. Kayula Siame, wakitia saini mmoja wa Mikataba ya kuanzishwa kwa Kituo cha Pamoja cha Mpakani cha Tunduma/Nakonde, ifikapo Februari Mosi, 2017.
tz8
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda (kushoto) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Uwekezaji wa Zambia, Bi. Kayula Siame, wakionesha  Mikataba ya kuanzishwa kwa Kituo cha Pamoja cha Mpakani baada ya  kusainiwa ili kuruhusu kuanzishwa rasmi kwa kituo  cha mpakani cha Tunduma/Nakonde.
tz9
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda (kushoto) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Uwekezaji wa Zambia, Bi. Kayula Siame, wakibadilishana Mikataba ya kuanzishwa kwa Kituo cha Pamoja cha Mpakani Tunduma/Nakonde baada ya  kusainiwa ili kuruhusu kuanzishwa rasmi kwa kituo  hicho.
tz10
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban (kushoto), na Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Uwekezaji wa Zambia, Bi. Kayula Siame, wakitia saini moja ya mikataba ya kuanzishwa kwa Kituo Cha Pamoja na Mpakani katika Mpaka wa Tunduma na Nakonde unaotarajiwa kuanza kufanyakazi rasmi Februari mosi, 2017.
tz11
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban (kushoto), na Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Uwekezaji wa Zambia, Bi. Kayula Siame, wakionesha mikataba waliyosaini ili kuruhusu kuanzishwa rasmi  kwa Kituo Cha Pamoja cha Mpakani katika Mpaka wa Tunduma na Nakonde unaotarajiwa kuanza rasmi Februari mosi, 2017.
tz12
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban (kushoto), na Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Uwekezaji wa Zambia, Bi. Kayula Siame, wakibadilishana Mikataba waliyosaini ili kuruhusu kuanzishwa rasmi kwa Kituo Cha Pamoja na Mpakani katika Mpaka wa Tunduma na Nakonde unaotarajiwa kuanza rasmi Februari mosi, 2017.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM)
…………………………………………………………………………………………
Benny Mwaipaja-WFM, Mbeya
TANZANIA na Zambia, zimetiliana saini Mikataba Minne kwa ajili ya uanzishwaji rasmi wa kituo cha pamoja katika mpaka wa Tunduma na Nakonde, kitakachoanza kufanyakazi rasmi Februari mosi mwaka huu, ili kurahisisha ufanyaji biashara kati ya nchi hizo mbili
Uamuzi wa kuanzishwa kwa huduma hiyo ijulikanayo kama One Stop Border Post, ni utekelezaji wa maagizo ya Marais wa nchi hizo Mbili, Waheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, na Edger Lungu, waliyoyatoa wakati Rais huyo wa Jamhuri ya Zambia, Edger Lungu alipofanya ziara ya kikazi hapa nchini hivi karibuni.
Mikataba iliyotiwa saini ni makubaliano ya Mwongozo wa Utendaji wa Kituo cha Pamoja cha Tunduma/Nakonde pamoja na Mfumo wa Urahisishaji Biashara kwa lengo la kukuza biashara kati ya nchi hizo mbili.
Waliosaini Mikataba hiyo kwaniaba ya Serikali ya Tanzania, Mjini Vwawa, wilaya ya Momba, mkoani Songwe, ni Naibu Katibu Mkuu wa Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Adolf Mkenda, huku Zambia ikiwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Uwekezaji wa nchi hiyo, Bi. Kayula Siame.
Wakizungumza baada ya kutiwa saini kwa mikataba hiyo Makatibu wakuu hao wamesema kuwa Uanzishwaji wa Kituo cha Pamoja Mpakani Tunduma/Nakonde, utarahisisha ufanyaji wa biashara kati ya Tanzania na Zambia kwa kupunguza ukaguzi kwani ukaguzi utafanyika mara moja katika kituo cha kuingia badala ya kufanyika mara mbili katika nchi zote mbili pamoja na kuongeza makusanyo ya kodi
“Lengo la kituo hicho pia ni kuifanya biashara kati ya Tanzania na Zambia kuwa huru lakini ikifuata misingi na taratibu za kufanya biashara mpakani. Pia kitarahisisha biashara katika eneo la mpakani na kuvutia wananchi na wafanyabiashara kutoka nchi zote mbili kutumia kituo hiki na kuepuka kutumia njia zisizo rasmi kupitisha mizigo na hivyo kupunguza ufanyaji wa biashara za magendo kama si kukomeshwa kabisa” Alisisitiza Bi. Amina Khamis Shaaban
Alisema kuwa utaratibu huo unatarajia kuona  kuongezeka kwa ushirikiano kati ya taasisi za serikali za nchi hizi kwani shughuli katika kituo zitakuwa zinafanyika kwa uwazi katika eneo moja.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara wa Zambia, Bi. Kayula Siame, amesema kuwa anatarajia kuwa  wananchi wa nchi hizo mbili watatumia fursa ya kuwepo kituo hiki kuweza kufanikisha biashara zao  na kuepuka kupitisha bidhaa zao kwa njia za magendo ama njia za panya ili kukwepa kukamatwa na vyombo vya dola.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Tanzania, Prof. Adolf Mkenda, alieleza kuwa kuboresha kwa huduma katika Mpaka huo wa Tunduma na Nakonde utaongeza biashara ya kusafirisha mizigo katoka Bandari ya Dar es salaam kwenda Zambia na nchi nyingine jirani.
Kwa upande wake Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere Amesema kuwa huduma hiyo itaanza Februari mosi mwaka huu kwa kutumia majengo ya forodha yaliyopo katika mpaka huo wa Tunduma na Nakonde nchini Zambia baada ya kufanyiwa ukarabati na kuwekwa mifumo ya teknohama, wakati kazi ya ujenzi wa kituo kipya kwa upande wa Tanzania ukiendelea kujengwa.
Kituo cha Tunduma/Nakonde kitakuwa kituo cha Tano kufanya kazi baada vituo vinne kukamilika na kufanya kazi katika mipaka ya Tanzania na nchi jirani za Kenya, Rwanda na Burundi.
Vituo hivyo ni Holili-Taveta katika mpaka wa Tanzania na Kenya, Kituo cha Rusumo katika mpaka wa Tanzania na Rwanda, Mutukula katika mpaka wa Tanzania na Uganda na Kabanga/Kobela katika mpaka wa Tanzania na Burundi.
Kwa upande wa Zambia, hiki kitakuwa kituo cha Pamoja cha Mpakani cha pili baada ya kituo cha Chilundu kilichopo katika mpaka wa Zambia na Zimbabwe.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages