Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani
shambulio la kigaidi lililotokea jana Alkhamisi katika mkoa wa Sindh
nchini Pakistan, ambapo makumi ya watu waliuawa na wengine wengi
kujeruhiwa.
Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran
sanjari na kutoa mkono wa pole kwa serikali ya Pakistan, waathirika wa
hujuma hiyo ya kigaidi na taifa kwa ujumla, amelitaja shambulizi hilo
kama 'jinai mbaya ya kutisha'.
Qassemi amesema mbinu chafu kabisa ya kisiasa ni kutumia ugaidi na
vitisho kwa maslahi ya kisiasa akisisitiza kuwa, juhudi za pamoja na za
dhati zinahitajika ili kung'oa mizizi ya ugaidi katika eneo na kote
duniani.
Zaidi ya watu 80 wakiwemo watoto wadogo 20 waliuawa na wengine 250
kujeruhiwa jana Alkhamisi, baada ya magaidi wa Daesh kushambulia kwa
bomu Haram ya Kisufi ya Hazrat Lal Shahbaz Qalandar, katika mji wa
Sehwan Sharif, mkoani Sindh.
Magaidi wapatao 39 wa kundi la kitakfiri la Daesh/ISIS wameuawa na
maafisa usalama kufuatia hujuma hiyo, baadhi wakiuawa kwa kufyatuliwa
risasi mkoani Sindh, na wengine katika eneo la Khyber Pakhtunkhwa.
Septemba mwaka jana, watu zaidi ya 23 waliuawa na makumi ya wengine
kujeruhiwa katika shambulio jingine la kigaidi lililofanywa ndani ya
msikiti katika Sala ya Ijumaa wilayani Mohmand nchini Pakistan.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269