Umoja wa Mataifa umesema jeshi la Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo limeua makumi ya watu katika makabiliano na kundi
la waasi kati ya Februari 9 na 13.
Taarifa ya UN iliyotolewa leo Jumanne imesema kuwa, watu 101,
wakiwemo wanawake 39 wameuawa katika mapigano hayo makali katikati mwa
nchi, baina ya askari wa jeshi la Kongo DR na waasi wa kundi la Kamwina
Nsapu, katika mji wa Tshimbulu, yapata kilomita 60 kusini mwa mkoa wa
Kananga.
Liz Throssell, msemaji wa shirika la kutetea haki za binadamu amesema
mapigano kati ya pande mbili hizo yalianzishwa na kundi hilo la waasi
wanaotaka kulipiza kisasi cha kuuawa kamanda wao, Kamwina Nsapu.
Nsapu aliuawa mwezi Agosti mwaka jana, baada ya kutishia kuuvamia
mkoa wa Kasai ya Kati, akiwatuhumu maafisa usalama kuwa wanawakandamiza
raia katika eneo hilo. Tangu baada ya kuuawa Nsapu, miji kadhaa na
vijiji vya Kasai ya Kati na Kasai ya Mashariki imekuwa ikisumbuliwa na
vurugu, machafuko na mapigano kati ya askari wa kulinda usalama na
wanamgambo hao wanaomuunga mkono kiongozi wao huyo wa zamani.
Mapigano yanaripotiwa kukithiri kote Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
kutokana na hatua ya Rais Joseph Kabila ya kukataa kuondoka madarakani
baada ya muhula wake wa urais kumalizika mwezi Disemba mwaka jana.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269