Wanaharakati wanaopinga
Sheria ya Huduma za Habari iliyopitishwa hivi karibuni wamepata pigo baada ya
mmoja wa wakili Bw. Francis Stolla kujitoa katika utetezi.
Akiongea leo Jijini Dar
es Salaam Wakili nguli wa Kujitegemea Bw. Stolla alisema kuwa ameamua kujitoa katika
kesi hiyo iliyofunguliwa na wanaharakati dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutokana
na kukabiliwa na majukumu mengine.
“Wakati Shauri linafunguliwa
Arusha sikuwepo kwa sababu ya majukumu mengine, pia lilivyofunguliwa Mwanza
sikuwepo hivyo kutokana na hilo nimeamua kuwaachia mawakili wengine waendelee
na shauri hilo na mimi niendelee na majukumu mengine” alisisitiza Wakili
Stolla.
Alisema kuwa madai
makubwa ya mawakili hao ni kwamba Sheria ya Huduma za habari inakiuka mkataba
wa Afrika Mashariki, na kusema kuwa kesi iliyofunguliwa Mwanza inaitaka
Mahakama itamke kwamba kuna baadhi ya vifungu vilivyotajwa kwenye Sheria ya
Huduma Habari inakiuka Katiba ya nchi.
Akiongea kuhusu dalili
za kushindwa kwa kesi hiyo iliyofunguliwa na wanaharakati dhidi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali katika mahakama ya haki ya Afrika Mashariki na Mahakama kuu
Mwanza Bw. Francis Stolla alisema suala hilo anaiachia mahakama kwani ni
kinyume kutoa mapendekezo wa kesi kushindwa au kushinda.
“Mara nyingi huwa
tunaiachia Mahakama na mashauri hayo yote mawili yapo Mahakamani huwezi sema
shauri hili litashinda ama kushindwa kwa sababu mashauri yakiwa mahakamani
haturuhusiwi kusema shauri hili litashinda ama kushindwa ili Mahakama ibakie
kuwa huru” alisema Wakili Stolla.
Kesi hiyo ilifunguliwa
na wanaharakati katika mahakama ya haki ya Afrika Mashariki mkoani Arusha na Mahakama
kuu ya Tanzania Mkoani Mwanza.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269