Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema,
mpango wa serikali ya Marekani wa kutuma wanajeshi wake nchini Syria
hautakuwa na matokeo mengine ghairi ya kuongeza mgogoro katika eneo la
Mashariki ya Kati na duniani kiujumla. Amesema hayo pambizoni mwa
mkutano wa usalama uliofanyika mjini Munich, Ujerumani wakati
alipohojiwa na televisheni ya CNN.
Kwa mujibu wa shirika la habari la
IRNA, Muhammad Javad Zarif amekumbushia hatua ya Marekani ya
kuishambulia na kuikalia kwa mabavu Iraq na kusema kuwa, uvamizi huo wa
Marekani nchini Iraq ndio uliozaa genge la kigaidi la Daesh (ISIS).
Amesema, kuweko wanajeshi wa kigeni
nchini Syria kutayatia nguvu magenge ya kigaidi ambayo yatatumia fursa
hiyo kushawishi vijana wengi zaidi kujiunga nayo. Waziri wa Mambo ya Nje
wa Iran ameongeza kuwa, wale ambao wameanzisha genge la kigaidi la
Daesh ndio hao hao waliokuwa wamempa silaha dikteta wa Iraq Saddam
Hussein na ndio wao walioanzisha mtandao wa al Qaida.
Kwa upande wa hatua za kiadui za
Marekani dhidi ya Iran, Zarif amesema, mtu yeyote ayaneijua historia ya
Iran anaelewa vyema kwamba Wairani kamwe hawababaishwi na kauli za
vitisho na njia pekee ya kupata majibu mazuri kutoka kwa Wairani ni
kuheshimiana na kulinda manufaa ya pamoja.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aidha
amesema, serikali ya Barack Obama huko Marekani iliamua kutumia vikwazo
vya kiuchumi kudhihirisha chuki za Marekani dhidi ya taifa la Iran
lakini mwenyewe alilazimika kufanya mazungumzo na Iran kuhusu miradi
yake ya nyuklia baada ya kufeli vikwazo vyake hivyo.
Amesema, jamii ya kimataifa inakubaliana
kwa kauli moja kuhusu umuhimu wa makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa
baina ya Iran na kundi la 5+1 na kuongeza kuwa, watu wote wakiwemo
wataalamu wa Marekani wanatambua vyema kuwa JCPOA ni makubaliano bora
zaidi ya nyuklia na hayana faida kwa Iran pekee, bali hata kwa Marekani.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269