DODOMA, TANZANIA
Jukwaa la
Watumiaji Tanzania limeandaa maadhimisho ya Tisa ya Kitaifa ya Siku ya Haki za
Mtumiaji yatakayofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere katika Chuo cha
Mipango, Mkoani Dodoma kuanzia Machi 13 hadi 15, 2017.
Jukwaa la
Watumiaji ni chombo kinachounganisha Juhudi za kumuelimisha na kumtetea Mtumiaji
kupitia Taasisi za Serikali zinazojishughulisha na utetezi wa Mtumiaji ambazo
ni Mabaraza ya Ushauri kwa Watumiaji wa Huduma zinazodhibitiwa na: Mamlaka ya
Usafiri wa Anga (TCAA-CCC), Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA-CCC),
Mamlaka ya Udhibiti wa Sekta ya Mawasiliano (TCRA-CCC), Mamlaka ya Udhibiti wa
Sekta za Nishati na Maji (EWURA-CCC) na Tume ya Ushindani (FCC).
Kaulimbiu ya
maadhimisho hayo inasema ‘Haki ya Mtumiaji katika
Ulimwengu wa Kidigitali”. Kaulimbiu hii
imetoholewa kutoka Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Mlaji Kimataifa kwa
mwaka 2017 iliyotolewa na Asasi Huru ya Utetezi wa Mlaji ‘’Consumers International’’ ambayo inasema "Consumer Rights in the Digital Age’’.
Maadhimisho hayo
yatapambwa na shughuli mbalimbali zikiwemo vipindi mahsusi katika redio za kijamii
(Community Radios) mjini Dodoma, semina kwa makundi ya wadau mbalimbali ambayo
ni wanafunzi wa shule za Sekondari, Wadau kutoka Asasi za Kiraia, Serikali za
Mitaa, Madiwani wa Dodoma Mjini na Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu.
Maadhimisho hayo yatafunguliwa
na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Jordan Rugimbana tarehe 13 Machi, 2017 na
yatafungwa na Mwakilishi wa Waziri Mkuu, Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana,
Ajira na Walemavu, Mhe. Jenista Mhagama (MB) tarehe 15 Machi, 2017 katika
ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere, Chuo cha Mipango, Dodoma.
Kaulimbiu hii inayotaka haki
za mtumiaji katika ulimwengu huu wa kidigitali kuboreshwa imekuja wakati
muafaka ambapo inakadiriwa kuwa kwa sasa watu wapatao bilioni 3 ulimwenguni
(sawa na asilimia 40 ya idadi ya watu ulimwenguni) kwa sasa wanatumia huduma
mbalimbali kupitia mitandao ya mawasiliano ya tovuti ikilinganishwa na asilimia
moja tu ya idadi ya watu ulimwenguni waliokuwa wakitumia huduma hizo mwaka
1995.
Kufikia Mwaka 2016,
Watanzania wapatao milioni 45 walikuwa wamesajiliwa katika huduma za fedha
kupitia mitandao ya simu za mkononi. Miamala inayohusisha huduma za fedha
katika simu ni mingi na ya thamani kubwa, na hivyo wateja wanatakiwa kulindwa
ili waziamini huduma hizo na kuendelea kuzitumia.
Aidha, Kumekuwa na
matatizo ya watumiaji wa huduma hizi kutapeliwa na watoa huduma na wauza bidhaa
mitandaoni wasio waaminifu. Wapo watoa huduma ambao pia wamekuwa wakitoza
gharama kubwa kwa wateja wanaonunua bidhaa mitandaoni lakini wakaambulia bidhaa
zilizo bandia, au chini ya kiwango. Aidha, watumiaji wengine wamelalamikia
kutapeliwa na kuibiwa kupitia huduma za fedha katika simu za mikononi.
Kwa kuwa idadi hii
inaongezeka kwa kasi, changamoto ya uwepo wa uhakika wa usalama na ulinzi wa
mtumiaji wa mitandao hiyo ni jambo muhimu kwa ajili ya maendeleo endelevu ya
huduma za manunuzi pamoja na utumaji na upokeaji pesa kwa njia ya mitandao ya
wavuti na simu za mikononi.
Azimio la Baraza Kuu la
Umoja wa Mataifa Namba 70/186 Kuhusu Utetezi wa Mlaji la tarehe 22 Desemba,
2015, pamoja na mambo mengine, limebainisha miamala ya manunuzi kwa njia za
kielektroniki, pamoja na huduma za fedha kuwa ni maeneo ambayo watumiaji
wanatakiwa kulindwa wanapotaka kupata huduma hizo.
Tanzania imekwishaanza
kuchukua hatua katika eneo hili kwa kutunga ‘’Sheria ya Mifumo ya Malipo’’ ya
mwaka 2015 na kanuni zake za mwaka 2015 pamoja na Sheria ya Kudhibiti Miamala
ya Kielektroniki ya mwaka 2015. Aidha, Benki Kuu ya Tanzania, imeanzisha
Kurugenzi ya Mifumo ya Malipo inayodhibiti miamala ya fedha kupitia simu za
mikononi.
Kwa upande wa huduma za
Fedha, Benki Kuu ya Tanzania, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa huduma za
kifedha na utetezi wa mlaji wakiwemo FCC, TCRA, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa,
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Bima (TIRA), Wizara ya Fedha kwa kushirikiana
na Asasi ya Kiraia ya Financial Sector Deeping Trust (FSDT) wamekwishaanza
juhudi za kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kuelimisha Watumiaji wa Huduma za
Kifedha ili waweze kuelewe haki na wajibu wao na kuchukua hatua pale wanapoonewa.
Sambamba na hilo wamekwishaanza mikakati ya kuanzisha mfumo wa utetezi wa
mtumiaji wa huduma za kifedha.
Baadhi ya Taasisi za
Kumtetea Mtumiaji zimeanzisha vilabu vya Utetezi wa Mtumiaji katika shule
kadhaa za msingi na sekondari pote nchini. Taasisi hizo ni pamoja na Tume ya
Ushindani FCC, SUMATRA-CCC, EWURA-CCC na
TCRA-CCC. Vilabu hivyo vimekuwa ni chachu ya mabadiliko makubwa katika
uelimishaji watumiaji kwa jamii ya kitanzania. Madhumuni ya kuanzisha vilabu
mashuleni ni kuwajengea uwezo watoto kuhusiana na masuala muhimu ya utetezi wa mtumiaji
ili wakue wakiwa na ueledi wa masuala hayo na hivyo kuweza kuteta haki zao na
kushiriki kikamilifu katika uchumi wa soko.
Imetolewa na:
MHANDISI THOMAS
MNUNGULI
KAIMU MWENYEKITI -JUKWAA LA WATUMIAJI TANZANIA
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269