Breaking News

Your Ad Spot

Mar 10, 2017

WATAMBUE WANAWAKE KUMI AMBAO NI MASHUHURI NCHINI TANZANIA

Na Jumia Travel Tanzania
Kila ifikapo Machi 8 dunia huadhimisha siku ya kimataifa ya wanawake ambapo nchi na taasisi mbalimbali huwa na shughuli kadha wa kadha katika kusherehekea siku hii. Kwa kawaida shirika la Umoja wa Kimataifa Duniani, UN, huwa na kauli mbiu kwa kila mwaka katika kuadhimisha siku hii, kwa mfano mwaka huu inasema, “Wanawake Katika Ulimwengu wa Mabadiliko ya Kazi: Kufikia usawa wa 50 - 50 ifikapo 2030.”   

Tofauti na awali, sasa hivi wanawake wamekuwa na muamko mkubwa katika kuisherehekea siku hii kwani wanaitumia vilivyo kupaza sauti zao juu ya masuala yanayowahusu. 

Hivyo basi, Jumia Travel inakuletea majina ya wanawake hawa 10 wa kitanzania waliojipatia umaarufu mkubwa kupitia shughuli tofauti za kijamii wanazozifanya. 

Mama Samia Suluhu
Unapozungumzia miongoni mwa wanawake wachache waliofanikiwa kupata nyadhifa za juu kabisa za uongozi nchini Tanzania basi huwezi kuacha kumtaja Mama Samia Suluhu Hassan. Huyu ni Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke kuwahi kutokea nchini ambapo aliupata wadhifa huo kufuatia uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 uliomuweka Rais John Pombe Magufuli madarakani. Tanzania kama nchi zingine za kiafrika kwa kiasi fulani imekuwa na kasumba ya kutomwamini mwanamke katika kushika nyadhifa za juu za kiuongozi. 

Lakini kuchaguliwa kwa Mh. Samia Suluhu kumedhihirisha kuwa hakuna lisiloshindikana endapo wanawake wakiwezeshwa, kuaminiwa na kupewa fursa.

Maria Sarungi Tsehai
Miongoni mwa wanawake wanaofanya shughuli nyingi katika harakati za kuiona jamii ya watanzania ikisonga mbele ni Maria Sarungi Tsehai. Kumchambua Maria kwa kila shughuli anayoifanya ni vigumu kwani itachukua muda mrefu ingawa kitaaluma yeye ni mtaalamu wa masuala ya mawasiliano. Kati ya shughuli kadha wa kadha anazozifanya, jina la Maria Sarungi Tsehai lilikuja kujulikana na watanzania wengi baada ya kuteuliwa kuwakilisha kwenye Bunge la kujadili mchakato wa katiba mpya na aliyekuwa Rais wa awamu ya nne, Mh. Jakaya Mrisho Kikwete mwaka 2014.
Maria alichaguliwa kufuatia hamasa yake ya kuibua mijadala ya kimaendeleo nchini Tanzania kupitia mitandao ya kijamii kama vile ‘Facebook na Twitter’ kupitia #ChangeTanzania, na kufanikiwa kuungwa mkono na wafuasi zaidi ya 50,000. 

Dk. Helen Kijo Bisimba
Kwa muda mrefu Dr. Bisimba yupo kwenye tasnia ya sheria ambapo amekuwa kipaumbele katika kutetea maslahi na kutoa msaada kwa watanzania wanyonge wanaonewa na kunyimwa haki zao katika masuala mbalimbali. 

Ni Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini Tanzania (LHRC) nafasi ambayo yupo kwa zaidi ya miongo miwili. Mama huyu msomi aliyebobea katika masuala ya sheria amekuwa na mchango mkubwa juu ya harakati za kutetea haki na usawa katika nyanja mbalimbali. 

Kupitia shughuli za kituo hicho, Dr. Helen Bisimba amekuwa ni alama na nguzo muhimu ya mapambano dhidi ya unyonge na ukandamizwaji wa haki dhidi ya wananchi wa kipato cha chini.    

Faraja Nyalandu
Watanzania wengi walilifahamu jina la Faraja Nyalandu baada ya kuwa mshindi wa kinyang’anyiro cha Miss Tanzania mwaka 2004. Lakini kipindi hicho alikuwa akijulikana kama Faraja Kota kabla ya kuolewa na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii na Mbunge wa Singida Kaskazini kwa sasa, Mh. Lazaro Nyalandu. Faraja ni mwanamke mjasiriamali katika masuala ya kijamii ambaye amejikita zaidi katika shughuli za kielimu ili kuwajengea uwezo watoto na vijana kuipata huduma hiyo. Kupitia dhamira hiyo ameweza kuzindua programu mbili za kuwawezesha wanafunzi kupata masomo kwa njia ya maswali na majibu pamoja na maelezo ya kutosha. Huduma hizi mbili ambazo ni ‘Makini SMS na Shule Direct,’ huwawezesha wanafunzi na walimu kuweza kusoma na kufundisha kupitia njia za simu na mtandao na hivyo kuepuka changamoto kama vile za uhaba wa walimu, vitabu na muda wa kujisomea.

Jokate Mwegelo
Jokate Mwegelo si jina geni miongoni mwa watanzania wengi na hii ilitokana na ushiriki wake katika mashindano ya urembo ya Miss Tanzania mwaka 2006 na kuibuka nafasi ya pili. Mbali na shughuli za urembo pia anajihusisha na muziki, ujasiriamali, uanamitindo na mavazi, uigizaji wa filamu, utangazaji wa luninga, ushereheshaji, na shughuli za kielimu. Jina lake ni kubwa na hamasa kwa mabinti wanaokua kutokana na mafanikio aliyonayo. Mpaka hivi sasa amefanikiwa kuanzisha kampuni yake mwenyewe ya masuala ya urembo na mavazi inayojulikana kama ‘Kidoti.’ Mbali na hapo anaendesha shughuli za kusaidia jamii yake kwenye nyanja ya elimu kupitia kampeni inayokwenda kwa jina la ‘Be Kidotified.’ Mpaka sasa amekwishajenga viwanja vya netiboli na kikapu katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Jangwani.  

Doris Mollel
Jina la Dorris Mollel limeanza kusikika na kujulikana baada ya kushinda taji la mashindano ya Miss Singida mnamo mwaka 2014. Baada ya hapo alianzisha harakati za kuwasaidia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati au miezi 9 yaani njiti ambapo alianzisha taasisi yake aliyoipa jina la Doris Mollel Foundation mwezi Februari mwaka 2015. Lengo kuu la kuanzisha taasisi hiyo ni kukusanya fedha kwa ajili ya kuwasaidia watoto wanaozaliwa njiti. Pia ameazimia kuielemisha jamii kwani tafiti zinaonyesha kwamba idadi ya watoto hao ni ndogo kutokana na wazazi wengi kutokuwa na tamaduni ya kwenda kujifungulia hospitali. 

Mercy Kitomari 
Huyu ni Afisa Mtendaji Mkuu na Muasisi wa kampuni inayojihusisha na utengenezaji wa ‘Ice Cream’ inayokwenda kwa jina la Nelwa’s Gelato. Mercy alishawishika kwa kiasi kikubwa kuanzisha biashara hii baada ya kuwa masomoni London nchini Uingereza ambapo alikuwa akivutiwa na vibanda vinavyouza ‘ice cream.’ Alikuwa anajiuliza endapo kama akirudi nchini atafanya kitu kama hiko kwani havikuwepo. Ametimiza ndoto hiyo na kwenda mbele zaidi kwa kuwawezesha watanzania wengine na kuwapataia mafunzo ya namna ya kuendesha biashara hiyo. Katika biashara hiyo Mercy hutumia viungo vya hapa nyumbani kutengenezea ‘ice cream’ zake kama vile matunda na karanga, hivyo kutoa ajira pia kwa wakulima. 

Joyce Kiria

Ongezeko la vituo vya luninga nchini Tanzania limekuja na fursa ya kuibuka kwa wazalishaji wa vipindi lukuki vinavyohusu masuala tofauti ya kijamii. Joyce Kiria ni miongoni mwa watangazaji wachache wanaovuma kwa kuwa na kipindi cha luninga kinachoivutia hadhira kubwa nchini. Kipindi chake cha ‘Wanawake Live’ kinachorushwa kwenye kituo cha luninga cha East African Television (EATV) kimejipatia umaarufu mkubwa hususani kwa kujikita zaidi katika kujadili na kuibua masuala mbalimbali yanayowakabili wanawake na kuwasaidia. Kipindi chake kimekuwa ni chanzo kizuri na msaada mkubwa kwa wanawake wanaokumbwa na changamoto mbalimbali na hatimaye kupatiwa msaada na serikali, taasisi au viongozi kuchukua hatua.

Wakonta Kapunda
Inawezekana kuwa habari ya huyu binti ndiyo iliyowagusa watanzania wengi zaidi nchini Tanzania kwa mwaka 2016. Maisha ya Wakonta Kapunda yalibadilika baada ya kupata ya kugongwa na gari na mwanafunzi mwenzao siku ya mahafali ya kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Korogwe, Tanga mwaka 2012. Ajali hiyo ilipelekea kupooza mwili mzima na kumlazimu kufanya shughuli zake kwa kutumia kichwa tu. 

Kilichowagusa wengi ni ari ya kutokata tamaa kwake ambapo aliweza kushiriki shindano la kuandika mswada wa filamu (script) lililodhaminiwa na kampuni ya Filamu ya Maisha ya nchini Uganda. Kwa kutumia ulimi wake aliweza kuandika na kufanikiwa kuchaguliwa kuingia hatua ya kwanza. Alijitokeza hadharani kuomba msaada baada ya kutakiwa kwenda visiwani Zanzibar kushiriki mafunzo ya siku 10 ambayo yalikuwa yanagharimu takribani kiasi cha shilingi milioni 4 za kitanzania. Wakonta alikuwa anaishi na familia yake mkoaniRukwa na haikuwa na uwezo wa kumsafirisha mpaka Zanzibar kwenda kujumuika na wenzake. Kupitia ushujaa wake, kutoka tamaa na kuamini kwamba ulemavu sio mwisho wa maisha, habari za Wakonta ziliwagusa watanzania na taasisi nyingi ambapo kampeni mbalimbali zilianzishwa kumsaidia kutimiza azma yake.   

Lady Jay Dee
Malkia wa muziki wa bongo flava nchini Tanzania tangu mwanzoni mwa mwaka 2000, Lady Jay Dee, inawezekana ndiye akawa msanii pekee wa kike aliyefanya vizuri katika tasnia hii kwa miaka yote ambayo amekuwa akifanya kazi hiyo. Mbali na kuyumba kidogo kwenye muziki na maisha yake binafsi miaka michache iliyopita, Lady Jay Dee au Jide aliwadhihirishia mashabiki wake kwamba bado anao uwezo mkubwa wa kufanya muziki. Alirudi kwa kuachia nyimbo ya ‘Ndi Ndi Ndi’ iliyomrudisha kwa kishindo kwenye chati mbalimbali za muziki nchini na kumfanya afanye matamasha na kuzungumziwa kila pembe ya nchi. 

Kwa hakika Lady Jay Dee ni mwanamke ambaye aliyashinda magumu yaliyomkumba ndani ya kipindi cha muda mchache na kufanikiwa kusimama tena. Kwa mashabiki wa muziki wa Tanzania itabakia kuwa hakuna kama yeye utakapozungumzia wasanii wa kike kwenye muziki waliofanikiwa zaidi na kuwashawishi wengi kuingia kwenye shughuli hiyo. 

Wapo wanawake wengi ambao wanastahili pongezi kwa shughuli wanazozifanya katika kuwainua wanawake wenzao na jamii kwa ujumla ambao Jumia Travel isingeweza kuwaorodhesha hapa. Lakini kwa hao waliotajwa hapo juu ni wazi kabisa mwanamke anaweza kufanya mambo makubwa sawa na zaidi ya mwanaume. 

Na ni matumaini yetu kwamba itafikia kipindi ambacho hakutakuwa na dhana ya kujadili jinsia tena ya mtu katika ufanisi wa jambo fulani kama inavyohubiri kauli mbio ya Shirika la Umoja wa Kimataifa mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages