Breaking News

Your Ad Spot

Jul 1, 2017

BENKI YA DUNIA YAIPATIA TANZANIA MKOPO NAFUU WA BILIONI 180 KUBORESHA ELIMU

NA BENNY MWAIPAJA, WFM-Dodoma
BENKI ya Dunia imeipatia Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wa Dola za Marekani milioni 80 kwa ajili ya kusaidia mpango wa Serikali wa miaka 11 wa Elimu bila malipo kuanzia elimu ya msingi hadi sekondari nchini.

Kiasi hicho cha fedha ni nyongeza ya Dola milioni 122 zilizotolewa na Benki hiyo katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa maboresho ya elimu kupitia Mpango wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa sasa-BRN, uliolenga kuondoa changamoto za elimu nchini.

Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia anayehudumia nchi za Tanzania, Somalia, Malawi na Burundi, Bella Bird amesema wakati wa utiaji saini mkataba wa nyongeza ya fedha hizo kati yake na>>
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James, kuwa nyongeza ya Dola milioni 80 imetokana na Benki hiyo kuridhishwa na namna Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dokt. John Pombe Magufuli, ilivyosimamia kikamilifu mpango huo wa utoaji elimu bure na kuwanufaisha wanafunzi wengi wakiwemo wanaotoka katika familia masikini.

Amesema kuwa uamuzi huo umesababisha ongezeko kubwa la wanafunzi wanaojiunga na elimu ya msingi, kuongezeka kwa ufaulu, wanafunzi kujua maarifa ya hesabu, kusoma na kuandika, utoaji wa ruzuku  ya elimu kwa wakati, hatua ambayo pia imesababisha kuwepo kwa changamoto za ukosefu wa miundombinu ya shule, changamoto ambazo anaamini zinapungua kupitia mkopo huo wenye masharti nafuu.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James ameishukuru Benki ya Dunia kwa kutoa fedha hizo ambazo amesema zitasaidia kwa kiasi kikubwa mipango ya Serikali ya kuboresha elimu nchini na kuondoa changamoto zinazoukabili mpango huo likiwemo ongezeko hilo kubwa la wanafunzi.

Bw. James ameeleza kuwa fedha hizo zitasaidia ujenzi wa miundombinu ya madarasa, ubora wa eimu, ukaguzi wa shule, upelekaji wa walimu, na kuwasaidia wanafunzi wenye mahitaji maalumu ili waweze kupata haki hiyo ya msingi ya elimu.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Simon Msanjila, amesema kuwa katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi wa elimu wa lipa kulingana na matokeo upitia mkopo wenye masharti nafuu wa Dola za Marekani milioni 122 zimetumika kujenga madarasa 1,400, matundu 3,390 ya vyoo, mabweni 261, majengo ya utawala 9, mabwalo ya chakula 9 nyumba za walimu 11, uchimaji wa visima vya maji katika shule nne na kukarabati vyuo vya ualimu. 

Amesema kuwa  mkopo mpya wa dola za Marekani milioni 80 uliotolewa na Benki ya Dunia hata kabla ya awamu ya kwanza ya mradi huo kumalizika hapo mwakani, umeonesha nia ya dhati ya Benki ya Dunia kusaidia maendeleo ya elimu nchini.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages