------------------
Na Bashir Nkoromo
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)-Bara Philip Mangula, amesema wapinzani hawakuwa na uwezo wa kushinda katika baadhi ya majimbo na kata jijini Dar es Salaam, katika uchaguzi mkuu uliopita isipokuwa walisaidiwa na wasaliti ndani ya chama.
Amesema, kutokana na madhara hayo, CCM itaendelea kuwasaka na kuwang'oa wasaliti hao, wakiwemo wale waliofanikiwa kujipenyeza na kushinda nafasi mbalimbali katika uchaguzi ndani ya Chama CCM na ndiyo maana CCM imefuta uchaguzi kwenye baadhi ya kata.
Mangula amesema hayo leo katika kikao chake na Wenyeviti wapya wa Mashina ya CCM, kutoka kata za Kawe na Kinondoni, waliochaguliwa hivi karibuni, kilichofanyika leo Vijana Social Hall, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Amesema, tayari chama kimeshachukua hatua mbalimbali kwa wasaliti kuanzia ngazi ya taifa, mikoa na kata kwa kuwapa adhabu zikiwemo za kuwafuta uanachama, onyo kali na wengine kuendelea kuchunguzwa.
"japokuwa tumekwishachukua hatua mbalimbali dhidi ya wasaliti lakini bado kazi hii inaendelea hadi tuhakikishe tabia hii chafu ya usaliti inakoma ndani ya chama, kwa sababu ni jambo la kushangaza CCM yenye wanachama wengi kiasi hiki kuliko chama chochote inapoteza majimbo katika mazingira yasiyo na majibu", alisema Mangula.
Akitoa tathimini kuhusiana na wasaliti ngazi ya mkoa, alisema jumla ya viongozi 4595 walikuwa wasaliti ndani ya Chama walipewa onyo, huku 3907 wapo chini ya uangalizi wa miezi 12.
Wengine waliopewa kalipio ya miezi 18 walikuwa 4, wengine 398 wapo katika uchunguzi, 465 wameadhibiwa, huku waliofukuzwa na kuvuliwa uwanachama wapo 2267.
Mangula aliwataka Wenyeviti hao wapya kuwa mstari wa mbele kuhakikisha CCM inaimarika katika maeneo yao kwa kuzingatia misingi na kanuni ambayo mojawapo ni kuepuka kupokea na kutoa rushwa hasa nyakati za uchaguzi.
Akimkaribisha mangula kuzungumza na wenyeviti hao, katibu wa CCM mkoa wa Dar es Salaam Saad Kusilawe aliwataka watendaji katika matawi yenye miradi kuisimamia kwa makini midari hiyo hasa upande wa mapato, ili mapato yanayopatikana yatumike pia kuwalipa japo kidogo wenyeviti wa mashina.
Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara Philip Mangula akiwasili katika ukumbi wa Vijana Social Hall, Kinondoni Dar es Salaam, kuzungumza na Wenyeviti wa Mashina kutoka Kata za Kawe na Kinondoni, leo. Kulia ni Katibu wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, Saad Kusilawe.
Wenyeviti wa CCM wa matawi wakimshangilia Mangula alipoingia ukumbini
Mangula akiwa meza kuu baada ya kuwasili ukumbini
Wenyeviti hao wakishangilia ukumbini
Katibu wa CCM mkoa wa Dar es Salaam Saad Kusilawe akimkaribisha Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara Philip Mangula, kuzungumza na wenyeviti hao wa mashina
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Bara Philip Mangula akizungumza na Wenyeviti hao wa mashina kutoka katika Kata za Kawe na Kinondoni, Dar es Salaam, leo
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Bara Philip Mangula akikabidhi vitendea kazi kwa mwenyekiti wa shina namba 12 Oysterbay, James Nyakyoka, alipokabidhi vifaa hivyo kwa wenyeviti hao baada ya kuzungumza nao leo
PICHA BASHIR NKOROMO
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269