CHAMA Cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania
(TASWA) na wahariri wa habari za michezo nchini, tumepokea kwa masikitiko
makubwa taarifa ya kushambuliwa kwa mwanahabari John Dande (Pichani), zinazodaiwa
kufanywa na straika wa Yanga, Obrey Chirwa, juzi Jumanne Uwanja wa Uhuru, Dar
es Salaam.
TASWA
na wahariri wa habari za michezo, tunaalani tukio hilo la kushambuliwa kwa
Dande ambaye ni mpigapicha wa Kampuni ya New Habari 2006 Limited, kwani kitendo
hicho si cha kiungwana bali ni udhalilishaji wa taaluma ya habari na hujuma kwa
tasnia na mambo kama haya yanadhoofisha
nguzo muhimu ya kujenga jamii yenye uelewa wa mambo yanayoendelea nchini na
kudhoofisha mfumo wa kidemokrasia, ambao tunajitahidi kuuimarisha nchini.
Kukaa
kimya, hata tukiliwazwa na kuombwa samahani kwa jambo hili, hakutatoa tafsiri
nyingine kwa wana taaluma ya habari na jamii kwa ujumla isipokuwa kuliona jambo
hili kama ni la kawaida.
Kama
tukio hilo lingefanyika eneo la starehe au mitaani na mwandishi hakuwa kazini,
tungelichukulia suala hilo kama faragha inayowahusu watu wawili, aliyepiga na
aliyepigwa, lakini kutokana na kumtokea mwandishi akiwa kazini tena uwanjani, ndio
tumelazimika kutekeleza wajibu wetu wa kuitetea taaluma na haki ya mwandishi wa
habari kufanya kazi bila kusumbuliwa au vitisho.
Kifungu cha 7 cha sheria za huduma za habari
Na 12 ya mwaka 2016 kinaaainisha uhuru wa habari katika kukusanya habari kwa
muktadha wa kuwepo maeneo ya matukio kama hakuna sababu nyingine za kuzuiwa. Hivyo ni vyema
wadau wetu wakatambua kuwa uandishi
wa habari ni taaluma adhimu na nadhifu inayopaswa kuheshimiwa, kuenziwa, kulindwa
na kutoingizwa katika migogoro.Tunatoa tamko hili la kulaani kitendo hicho kwa sababu sio cha kawaida hapa nchini kama ilivyo baadhi ya nchi nyingine ambazo waandishi wanapigwa na hata kuuliwa. Lakini tunachelea kulifumbia macho tukio hili kwa sababu kufanya hivyo ni kusema tunaridhika kupigwa na wachezaji na baadaye viongozi na hata mashabiki.
TASWA na wahariri wa habari za michezo na waandishi wa habari kwa ujumla hawana na hawatakuwa na muhali na mchezaji, kiongozi au shabiki yeyote wa michezo anayefanya kitendo kama hiki, kwani huo ni uhuni na sio mwanzo mzuri na tunataka mwendo kama huu ukome mara moja na yeyote mwenye malalamiko kwa mwandishi wa habari binafsi, au chombo chake afuate taratibu za kistaarabu zilizopo.
Hata
hivyo kwa kuwa mhusika ameripoti tukio hilo kwenye vyombo vya usalama, tunawaomba
waandishi wa habari wawe watulivu na waziachie mamlaka husika zitekeleze
majukumu yake kwa mujibu wa sheria za nchi.
Tunaomba
ushirikiano mzuri kati ya waandishi, wachezaji na viongozi wa michezo ili
tucheze na tufurahie michezo kwa amani na kila mmoja aheshimu kazi ya mwenzake.
Michezo iwe furaha kwa wote. Tucheze bila kupigana.
UANACHAMA AIPS
Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Duniani (AIPS), chenye makao
yake makuu Lausanne, Uswisi, kimeanza
kupokea maombi ya kadi kwa wanachama mwaka 2018/2019 kwa waandishi wa habari za
michezo kutoka nchi mbalimbali duniani.
Maombi hayo yanafanyika kwa
njia ya mtandao kwa wanachama wapya na wale wa zamani kupitia mtandao wao wa www.aipsmedia.com, ambapo ukiingia katika hiyo tovuti, utakuta
maelekezo ya namna ya kupata kadi mpya, haichukui dakika tano kujaza na
ukishaituma itakupa maelekezo zaidi ya hatua ya kufuata.
Tunawahimiza wanachama wetu kuchukua
pia uanachama wa AIPS, kwani una faida nyingi, ikiwa ni pamoja na kupata kadi
ya uanachama ambayo inatoa fursa mbalimbali ikiwemo mafunzo ya muda mrefu na semina
za michezo mbalimbali.
UCHAGUZI MKUU
Mapema
mwezi huu tulitoa tamko la kuwepo Uchaguzi Mkuu wa chama chetu na kuwataka
wanachama ambao wapo kwenye leja kuanzia Julai mwaka 2007 hadi Julai mwaka huu
walipie ada zao za mwaka mmoja, ili kuhuisha uanachama wao na mwisho wa kufanya
hivyo ni Septemba 30.
Lakini
kutokana na muitikio mdogo sana katika ulipaji wa ada, Kamati ya Utendaji ya
TASWA imeongeza muda hadi Oktoba 10 mwaka huu wanachama wote wahakikishe wanalipia
ada hizo ili wahesabike wapo hai.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269