JONAS KAMALEKI - MAELEZO
Ajali za barabarani zimepungua kwa asilimia 40 katika kipindi cha Julai- Septemba 2017 ikilinganishwa na kipindi hicho hicho mwaka jana.
Hayo yameelezwa leo katika mahojiano maalum kati Mwanasheria wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Deus Sokoni na Idara ya Habari (MAELEZO).
Sokoni amesema katika kipindi cha Julai – Septemba mwaka 2016 ajali za barabarani zilikuwa 2639 wakati mwaka huu katika kipindi hicho hicho jumla ya ajali 1375 zimetokea nchini.
Kwa mujibu wa Kamanda Sokoni, idadi ya vifo pia imepungua kutoka 923 hadi 652 na ajali za pikipiki zimepungua kutoka 653 hadi 367 ambayo ni sawa na asilimia 44.
“Kupungua kwa ajali hizo na vifo imetokana na madereva kutii sheria bila shuruti, ushirikiano baina ya wananchi na jeshi la polisi na elimu kwa umma ambayo tumekuwatukiitoa kwa wadau mbalimbali, ikiwemo wanafunzi, vituo vya bodaboda na kambi za jeshi la wananchi,” alisema Sokoni.
Aidha, Sokoni amesema makosa yanayotokana na ulevi yameongezeka kutoka 7589 hadi 7617 jambo ambalo limeelezwa kuwa elimu bado inahitajika ili kupunguza changamoto hiyo.
Majeruhi wa ajali za barabarani wamepungua kutoka 570 hadi 284 ambayo ni sawa na takriban asilimia 50 jambo ambalo linaonyesha mabadiliko makubwa katika kuzingatia sheria za usalama barabarani.
Sokoni aliongeza kuwa elimu inayotolewa kwa waendesha pikipiki imesaidia kupunguza ajali na vifo vya waendesha pikipiki na abiria kiasi kwamba kwa mwaka 2016 katika kipindi husika vifo vilikuwa 246 na kwa mwaka huu ni 182.
Kupungua kwa ajali, majeruhi na vifo kumetokana na Mkakati wa Kitaifa chini ya Kikosi cha Usalama Barabarani wa kupunguza ajali za barabarani zinasosababisha majeruhi na vifo.
Kamanda Sokoni amewataka madereva, watembea kwa miguu, abiria na wadau wote wa usafiri kuzingatia sheria kanununi na taratibu za usalama barabarani.
Katika kutekeleza Mkakati huo zimefanyika operesheni za usalama barabarani katika mikoa ya Njombe, Tanga, Mbeya, Kilimanjaro, Arusha na Manyara. Katika operesheni hizo madereva 64 wamefungiwa leseni, wengi wao wakiwa madereva wa mabasi ya abiria ambapo madereva 14 wamefungwa jela.
Usalama barabarani ni jukumu la kila mtu, kwani watanzania karibu wote ni watumia barabara, hivyo kila mmoja inabidi awe mwangalifu katika sula hilo.
Ikumbukwe Kauli Mbiu ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani ya mwaka huu ilisema Zuia ajali, Tii Sheria, Okoa Maisha. Hivyo, madereva na waenda kwa miguu pamoja na abiria inabidi watii sheria bila shuruti ili kuzuia ajali na kuokoa maisha.
Your Ad Spot
Nov 9, 2017
Home
Unlabelled
AJALI ZA BARABARANI ZAPUNGUA NCHINI KUTOKANA NA ELIMU, KUTII SHERIA
AJALI ZA BARABARANI ZAPUNGUA NCHINI KUTOKANA NA ELIMU, KUTII SHERIA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269