Breaking News

Your Ad Spot

Nov 5, 2017

WADAU WA KOROSHO PWANI KUKATWA SH. 20 KWA KILA KILO KUCHANGIA ELIMU

MKUU wa mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, akizungumza na wadau wa korosho katika kikao cha tathmini na maandalizi ya msimu mpya wa zao hilo la biashara, kilichofanyika Mkuranga. (Picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi, Mkuranga
Wadau wa zao la korosho mkoani Pwani, wamekubaliana kukatwa sh. 20 kwa kila kilo moja ya korosho itakayouzwa msimu huu kwa ajili ya kuchangia sekta ya elimu mkoani humo..

Katika msimu wa korosho 2016/2017 wadau hao waliazimia ikatwe sh. tano kwa kila kilo kiasi ambacho kimeonekana hakitokidhi mahitaji.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wajumbe wa kikao cha tathmini na maandalizi ya msimu mpya wa korosho,akiwemo mzee Juma Mkwanywe,kilichofanyika Mkuranga,walisema zao hilo ni la biashara hivyo linaweza kuwainua katika kutatua changamoto zinazowakabili kielimu .

"Zipo bado changamoto nyingi za elimu ikiwemo kuharibika kwa miundombinu, shule chakavu na kuongeza madarasa" 

"Kiasi hiki sio kidogo hata kidogo ,kwani tukichukulia msimu wa 2016/2017 ziliuzwa tani 13,257,856 kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani "

"Sasa tani zote hizo tungetoa shilingi 20 kwa kila kilo tungekuwa na mamilioni mangapi ya fedha" alieleza.

Mkwanywe alielezea elimu ni jambo muhimu kwa watoto hivyo endapo wakitekeleza maamuzi yao itasaidia kupunguza baadhi ya kero hizo.

Hata hivyo alisema kuwa ,inawezekana kukawepo sheria zinazokataza kutoa fedha hizi za wakulima kufanya jambo kama hilo lakini kutokana ni maamuzi ya umoja hakuna kitakachopingika .

Aidha wadau hao wameazimia pia minada inayotarajiwa kuanza novemba 8 iwe inafunguliwa mapema.

Hata hivyo ,walisema wataalamu wa  ubora waongezwe na elimu ya matumizi ya dawa itolewe kwa wakulima .

Madai ya watoaji huduma yakapelekwe bodi ya korosho mapema ili kupata fungu lao na vitini vya taarifa vipelekwe kwa wajumbe ili wakapatiwe na wakulima wengine kujua kinachoendelea .

Baada ya wadau hao kuazimia mambo hayo kwa umoja wao ,mwenyekiti wa kikao hicho,ambae pia ni mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo alisema mkakati wa serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha wanafunzi wanasoma kwenye mazingira bora.

Alielezea ipo baadhi ya  mikoa iliyonufaika na mazao ya biashara ya mikoa yao ikiwemo kahawa mkoani Kilimanjaro ,Kagera ,Mbeya na pamba katika kanda ya Ziwa sanjali na miwa mkoa wa Morogoro .

Mhandisi Ndikilo alisema inawezekana zao la korosho likainua uchumi na kutatua matatizo yaliyopo mkoani humo.

“Tumekubaliana kwa umoja wetu kutenga sh.20 kwa kila kilo moja ya korosho itakayouzwa katika msimu huu naamini tutafanikiwa kupambana na changamoto mbalimbali zinazotukabili kwenye elimu”alisema mhandisi Ndikilo.

Mhandisi Ndikilo aliwataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi kuimarisha ulinzi kwenye vizuizi kudhibiti utoroshaji wa korosho .

Alisema msimu huu hawana simile kwa wale watakaobainika kutumia mifumo isiyo rasmi zaidi ya mfumo wa stakabadhi ghalani ambapo aliwataka wakulima kuanika korosho zao ili ziwe na ubora .

Mkuu huyo wa mkoa alihimiza kufufuliwe mashamba ya mikorosho ,na kupalilia mwezi January badala ya mwezi June .

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages