Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar 31.03.2018
Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar ZFDA umeteketeza Tani 24.5 za bidhaa mbali mbali ambazo zimebainika kuwa hazifai kwa matumizi ya binadamu.
Zoezi la uteteketaji limefanyika Kibele Wilaya Kusini na kusimamiwa na Wadau mbalimbali ikiwemo, Maafisa kutoka ZFDA, Wadau wa mazingira pamoja na Jeshi la Polisi ili kuhakikisha linateketelezwa kama ilivyopangwa.
Akizungumza na Wanahabari Msimamizi wa zoezi hilo kutoka ZFDA Aisha Suleiman amezitaja Bidhaa hizo kuwa ni pamoja na Mchele, Dawa za kuulia wadudu, Sabuni, Mafuta na Vipodozi ambazo zimebainika kutokana na zoezi la ukaguzi lililoendeshwa Bandarini, katika Maghala na Maduka tofauti.
Amesema Bidhaa hizo zilikuwa mali ya Wafanyabiashara na Kampuni tofauti hapa nchini.
Aisha amefahamisha kuwa Mchele Tani mbili ulibanika Bandarini kuwa umeharibika kutonana na kuingia maji wakati wa kusafirishwa kuja Zanzibar.
Bidhaa zingine zilibainika katika maghala ambapo kwa mujibu wa Sheria Wafanyabiashara wa bidhaa hizo hulazimika kulipia gharama za kuteketeza bidhaa hizo.
Aisha amesema muitikio wa Wafanyabiashara kuingiza Biashara halali kwa matumizi ya binadamu ni wa kuridhisha ikilinganishwa na siku za nyuma.
Hii inatokana na ZFDA kuongeza kasi ya ukaguzi na utolewaji wa elimu na taarifa mbalimbali kwa wafanyabiashara na Wananchi wa ujumla.
Amesema kwa sasa hali inaendelea vyema ambapo miaka ya 2007-8 ZFDA ilikuwa ikiteketeza zaidi ya Tani 100 ambazo zilikuwa hazifai kwa matumizi ya binadamu.
Hivyo amewataka Wananchi kutoa mashirikiano kwa ZFDA ikiwemo kutoa taarifa za bidhaa watakazozibaini zimepitwa na wakati kwa taasisi hiyo.
Kwa upande wake Mkaguzi wa dawa na vipodozi Mohamed Hassan Mohamed amesema miongoni mwa Vipodozi vilivyoteketezwa ni vile vilivyoisha muda wake wa matumizi na vile ambavyo haviruhusiwi kuingizwa Zanzibar maarufu kama Vipodozi haramu.
Amewataka wananchi kujenga mazoea ya kuzichunguza vyema bidhaa wanazonunua ili kujua muda wa kutengenezwa kwake na muda wa mwisho wa matumizi.
Aidha Mohamed ametoa wito kwa Wafanyabiashara kuwa karibu na ZFDA ili kujua baishara gani inafaa kuingizwa na ipi haifai kwa maslahi mapana ya Wananchi na Taifa kwa ujumla.
Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar ina jukumu la kusimamia udhibiti wa bidhaa za chakula, Dawa, na Vipodozi ambapo miongoni mwa kazi zake ni kuhakikisha kuwa bidhaa hizo zinazozalishwa nchini au nje ya nchi zinakuwa salama kwa matumizi ya binadamu
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269