Breaking News

Your Ad Spot

Feb 2, 2010

JW ANAYEDAIWA KUJERUHI RAIA KUTINGA MAHAKAMANI LEO

SIKU chache baada ya askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kufikishwa mahakamani kwa madai ya mauaji ya raia, askari mwingine anatarajiwa kupandishwa kizimbani leo kwa kujeruhi kwa risasi.

Tukio hilo lilitokea Jumamosi wiki iliyopita saa sita usiku, kwenye baa ya GMS Pub, Ukonga, Dar es Salaam, inayomilikiwa na askari wa JWTZ Yohana Lugendo wa Kikosi cha Ushonaji Chang’ombe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala Faustine Shilogile, alisema Lugendo, alimfyatulia risasi mbili Joseph Nyanda (23), aliyekuwa katika baa hiyo. Alisema risasi moja ilimjeruhi pajani na nyingine kwenye makalio.

Kwa mujibu wa Shilogile, shambulio hilo lilitokana na kutoelewana kati yao wakati muda wa kufunga baa ulipowadia. “Amedai Nyanda alikuwa anataka kumpiga ndiyo maana alijitetea kwa kumrushia risasi,” alisema Kamanda Shilogile.

Shilogile alisema alipohojiwa Lugendo alikiri kutenda kosa na kwamba, wanaendelea kumshikilia hadi atakapofikishwa mahakamani.

Akizunguza jana akiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili anakopatiwa matibabu, Nyanda alidai siku ya tukio alikuwa akinywa katika baa hiyo lakini alishangaa kuona mwanajeshi huyo akimsukuma alipokuwa akitoka baada ya baa kufungwa.

Nyanda alidai akiwa katika baada hiyo alikaa karibu na mmoja wa wahudumu, jambo lililoonyesha kumchukiza Lugendo, ambaye baadae alimwagiza muhudumu huyo kumuuliza Nyanda anataka kinywaji gani ili amnunulie.

Kwa mujibu wa Nyanda, muhudumu huyo alipomuuliza alimweleza anatumia Red Bull na kwamba, alipatiwa kinywaji hicho. Alidai wakati akiendelea kunywa, muhudumu huyo alikwenda kubadili nguo kwa ajili ya kuondoka na alipokuwa akitoka naye akiwa getini mwanajeshi huyo alimsukuma na kumfokea.

“Nilishangaa kwa kuwa sikujua kwa nini alifanya hivyo, lakini kabla sijachukua hatua yoyote alinipiga na baadae kunifyatulia risasi mbili ambazo bado zipo mwilini hadi leo (jana),” alidai Nyanda, aliyelazwa wodi ya Kibasila namba 13 .

Alidai baada ya kuripoti tukio hilo kituo kidogo cha polisi cha Ukonga, alipelekwa Hospitali ya Amana na kutakiwa kwenda Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Wiki iliyopita askari wa JWTZ Koplo Ally Ngumbe na Sajini Rhoda Robert wa JKT, walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakituhumiwa kumuua Swetu Fundikira (45).

00000

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages