Breaking News

Your Ad Spot

Mar 23, 2010

OBAMA ATIA SAINI MUSWADA WA BIMA YA AFYA

RAIS Barack Obama akitia saini muswada wa bima ya afya, katika hafla iliyofanyika katika Ikulu ya Marekani, leoWASHINGTON, Marekani
SIKU mbili baada ya Baraza la Wawakilishi kupitisha muswada wa huduma za afya, Rais Barack Obama, ameutia saini kuwa sheria katika hafla iliyofanyika Ikulu, mjini hapa.
     Kiongozi huyo aliwapongeza wawakilishi hao kwa kuupitisha muswada huo unaoelezewa kuwa ni wa kihistoria katika kuleta mabadiliko kwenye huduma a afya, hususani bima ya afya.  
     Sheria hiyo mpya itawawezesha Wamarekani milioni 32 ambao walikuwa  wanabaguliwa na kampuni za bima ya afya, kupata bima hiyo.
     Rais Obama alisema kwamba anautia saini mswada huo kuwezesha watu kama mama yake "ambaye alikuwa akijibizana na kampuni za bima wakati akiugua kansa katika siku za mwisho za maisha yake."
    "Muswada ninaoutia saini leo, ni mwanzo wa mabadiliko ambayo vizazi na vizazi vya Wamarekani walipigania, waliandamana na kusubiri kwa hamu yatokee," alisema Rais Obama.
     Katika hafla hiyo, walikuwepo watu waliokuwa wakiunga mkono muswada huo miongoni mwao Wawakilishi wa chama chake cha Democrats.
    Alimsifu Spika wa Bunge, Nancy Pelosi na Seneta Harry Reid kwa jitihada zao hadi kupitishwa kwa muswada huo, licha ya baadhi ya Wawakilishi kuupinga.
    Baada ya mjadala mkali katika Baraza la Wawakilishi upigaji kura ulifanyika ambapo Wawakilishi 219 waliuunga mkono na 212 waliukataa.
    Hakuna mwakilishi wa chama cha Republican aliyeunga mkono, huku baadhi ya wa Democrats nao wakiukataa.
    Pamoja na kuongeza idadi ya watu watakaolindwa na bima za afya, pia sheria hiyo inakataza kampuni za bima kuwabagua watu wenye magonjwa sugu.
    Kesho, Rais Obama atakwenda jimbo la Iowa kuelezea namna sheria hiyo itakavyosaidia kupunguza gharama za matibabu kwa wajasiriamali wadogo na familia.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages