.

MAHABUSU WATOROKA CHINI YA ULINZI WA POLISI KIBAHA

Apr 16, 2010


Na Scolastica komba, Kibaha.
JESHI la Polisi mkoani Pwani linawasaka mahabusu wawili kati ya sita waliotoroka chini ya ulinzi wa
askari polisi wakati wakisafirishwa kwenda katika gereza la Mkuza wilayani Kibaha baada ya kuhudhuria
mahakamani kusikiliza kesi za unyang'anyi wa kutumia silaha na mauaji inayowakabili.  
   Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Absaloom Mwakyoma alisema tukio hilo limetokea juzi majira ya saa 8
mchana wakati mahabusu sita walipokuwa wanasafirishwa kurudi gerezani hapo.
   Mwakyoma amesema mahabusu hao kwa pamoja walikuwa wakisafiri chini ya ulinzi wa askari Polisi G
1428 PC Sospeter, E 7943 PC Fredrick  na askari E 6126 PC Stephen kwa kutumia gari namba  PT 0823
Land Rover Defender ambapo walipofika eneo la Tamco jirani na msitu wa shirika la Elimu waliwashinda
nguvu askari hao wasindikizaji na kufanikiwa kuruka garini na kutokomea msituni.
   Mwakyoma amesema siku hiyo mahabusu hao wote sita walitoroka lakini muda mfupi baadae askari polisi
walifanya msako mkali uliokuwa ukiongozwa na Mkaguzi msaidizi wa Polisi Khatibu Sanduku na kufanikiwa
kuwakamata watuhumiwa wanne katika maeneo mbalimbali.
  Amewataja mahabusu hao sita waliotoroka kuwa ni Ramadhani Hamza,Mwinyimvua Juma,Simon
Maneno,Fabian Simon maarufu Mkwera,John Samweli maarufu kwa jina la Mapuri pamoja na Shaban
Mrisho maarufu kwa Jalala.
 Akielezea walivyokamatwa watuhumuwa hao wanne amesema katika eneo la tukio walifanikiwa
kukamatwa wawili ambao ni Mwinyimvua na Simon huku mtuhumiwa John akikamatwa eneo la Kwambonde
kilomita tano kutoka eneo la tukio na wa nne Ramadhani yeye alijisalimisha mwenyewe katika gereza la
Mkuza na kuletwa kituo cha Polisi Kibaha na askari Magereza
 Mwakyoma amesema juhudi za kuwatafuta watuhumiwa wawili Bw.Shabani na Bw.Fabian ambao
wanakabiliwa na kosa la unyanganyi wa kutumia silaha na mauaji zinaendelea kwa kutumia askari wa
kikosi cha intelijensia na vikundi vya ulinzi shirikishi na polisi jamii .
 Kamanda huyo amesema ili kuondoa mazingira yoyote ya utatanishi juu ya tukio hilo uchunguzi na hatua za
kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya wote waliohusika na zoezi la usafirishaji wa mahabusu hao ikiwa ni
pamoja na Jeshi hilo limetangaza zawadi kwa yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao
wawili  na pia Kamanada huyo aliwashauri watoro hao kujisalimisha wenyewe katika kituo chochote cha
polisi ili wajibu mashauri yao mbele ya vyombo vya sheria.
 

 

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช