Breaking News

Your Ad Spot

Aug 26, 2010

UFAFANUZI KUHUSU TAARIFA ILIYOTOLEWA NA BAADHI YA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MANENO NILIYOYASEMA WAKATI WA UZINDUZI WA KAMPENI ZA CCM MOSHI MJINI


Agosti 26, 2010

Taarifa kwa vyombo vya habari
Napenda kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa za kupotosha zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari hivi karibuni kuhusu uzinduzi wa kampeni za CCM Moshi Mjini, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Moshi Mjini Agosti 21, 2010 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, akiwemo Katibu wa Mkoa, Mzee Kazidi ambaye alikuwa mgeni rasmi. Pia alikuwepo Mgombea Ubunge (Moshi Mjini) kwa tiketi ya CCM, Bw. Justin Salakana, viongozi wa jumuiya mbalimbali za CCM, madiwani na wananchi.

Taarifa hizo zilizopotoshwa zilikuwa na nia kunichonganisha na chama changu na kumjenga Mbunge wa Moshi Mjini anayemaliza muda wake, Mh. Philemon Ndesamburo na kuonyesha kuwa mimi kada wa CCM, nina msimamo tofauti na Chama changu CCM.

Pamoja na mambo mengine, taarifa hizo ziliashiria kwamba katika mkutano huo wa hadhara, mimi, kada wa CCM, mbele ya viongozi wa CCM, katika mkutano wa kumnadi mgombea wa CCM, nilisema kuwa juhudi zilizofanywa na Ndesamburo zisibezwe na kwamba nilimjenga Ndesamburo wakati mimi nilikuwa nazungumzia mapungufu yake kwa kutaka kutofautisha kati ya uwezo wa mbunge anayetegemea nguvu zake binafsi na mbunge anayetokea kwenye chama tawala.

Ukweli ni kwamba nilimaanisha kuwa wananchi wa Moshi hawatapata maendeleo ya kweli bila serikali na nikatoa mifano nikasema, huenda Ndesamburo ameongeza madarasa matano katika shule tano lakini pengine mahitaji ya wilaya yalikuwa kupata shule tano kitu ambacho mbunge ambaye hayuko ndani ya chama tawala hawezi kufanya.

Mfano mwingine niliotoa ni kuwa huenda amefanikiwa kuongeza vyumba vitano katika zahanati tano za wilaya wakati mahitaji ya wilaya ni zahanati tano na sio vyumba vitano. Pia huenda aliweza kuchangia katika ujenzi wa kilomita moja ya lami lakini pengine mahitaji ya wilaya ni kilomita 31 za lami na ukizingatia kuwa kilomita moja inagharimu Shilingi Bilioni 1.5. Ni dhahiri kuwa bila mkono wa serikali, Ndesamburo anashindwa kukidhi mahitaji ya wananchi.

Nia na madhumuni ya ujumbe wangu ilikuwa kuwaeleza wananchi na wapiga kura wa manispaa ya Moshi kwamba ili tuondokane na umaskini na kukaribisha maendeleo na maisha bora kwa manufaa ya wananchi wa Moshi, ni vizuri wana CCM wa Moshi wawe wakweli na wajiepushe na kurubuniwa na wapinzani ili wauze kura ambayo ni sawasawa na kulia njaa na kulishwa pipi. Nawahisi wasifanye hivyo na badala yake wamchague Bw Justin Salakana kwa kumpa kura ili aweze kufanya kazi na serikali ya Chama tawala kinachoongozwa na Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

Niliwasihi wananchi wa Moshi kuwa wasipofanya hivyo, basi la maendeleo halitasimama Moshi na badala yake litaenda katika mikoa jirani kama vile Arusha, Tanga, Manyara, na mikoa mingine jirani.

Nimestushwa mno na taarifa potofu zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa mimi, Kada wa CCM, kwenye mkutano wa kuzindua kampeni na kumnadi mgombea wa CCM, mbele ya wana CCM, nimethubutu kusema kuwa jitihada za Ndesamburo zisibezwe wakati ni dhahiri kuwa Wilaya ya Moshi Mjini imerudi nyuma baada ya kushikiliwa na upinzania kwa miaka 15.

Ni wazi kuwa Ndesamburo ameshindwa kukidhi mahitaji ya wakazi Moshi na kuikosesha Moshi msukumo wa kiuchumi unaopatikana wakati kuna ushirikiano mzuri na serikali.

Nimesema nimestushwa na upotoshaji huu wa taarifa lakini sijashangaa maana naelewa mbinu zinazotumika sasa hivi Moshi Mjini kwani kuna watu maalumu waliopandikizwa wenye nia ya kumkashifu na kumharibia mgombea wetu Bw. Salakana. Watu hawa wamepandikizwa kwenye daladala, mabaa, viwanja vya michezo na vijiweni ili kueneza haya maneno yenye kashfa.

Yote haya ni kwa sababu ni wazi kuwa wananchi wa Moshi wamechoka na umaskini, ukosefu wa ajira na maendeleo kwa ujumla. Mwaka 2000 Ndesamburo alisema hatagombea mwaka 2005 lakini aliendelea na hata 2005 alisema hivyo kuhusu 2010. Wananchi wanalia njaa wanapewa pipi wakati haiuwi njaa.

Wapinzani walipewa miaka 15 ya kufufua uchumi wa Moshi na wameshindwa. Ni wazi kuwa bila kuwa na mbunge wa CCM Moshi Mjini wananchi wataendelea kukosa msukumo mkubwa wa kiuchumi kutoka kwa serikali.

Kuendelea kukalia kiti cha Jimbo la Moshi Mjini bila kuwa na uwezo wa kukidhi mahitaji ya wananchi ni sawa na mtu asiyekula nyama (vegeterian) kulinda friji lililojaa nyama na yeye mwenyewe hali na wala hataki wengine wale.

Muda umefika sasa wa wakazi wa Moshi Mjini kufanya maamuzi sahihi kwa kumchagua mgombea wa CCM, Bw. Justin Salakana. Wapinzani wamepewa dhamana kwa miaka 15. Wakazi wa Moshi wanasema, “Sasa mzee basi.”

Ahsanteni kwa kunisikiliza

Imetolewa na;

AGGREY MAREALLE

Kamanda UVCCM Moshi Mjini

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages