Breaking News

Your Ad Spot

Sep 2, 2010

MWAKILISHI wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzanoia kewenye Umoja wa Mataifa,Balozi, Ombeni Sefue akimkabidhi Katibu Mkuu wa Umoja wa Maatifa, Ban Kimoon, hati zake za utambulisho.
Balozi ombeni Sefue akaiwa na baadhi ya maofisa wa Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, baada ya kukabidhi hati zake.

HABARI KAMILI
NA MWANDISHI MAALUM, NEW YORK
NEW YORK-Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon amemtakia kampeni njema , Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, Rais Jakaya Mrisho Kikwete, na mafanikio mema katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba.
      Ban Ki Moon ametoa salamu hizo wakati wa Mazungumzo yake na Mwakilishi mpya wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Ombeni Sefue, mara baada ya Balozi huyo kumkabidhi hati zake za utambulisho katika hafla fupi iliyofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
      Katibu Mkuu wa UN, pamoja na kumtakia kila la kheri na mafanikio Rais Kikwete, pia amempongeza Rais Kikwete na Tanzania kwa ujumla kwa kuwa nchi kiongozi na ya mfano wa kuigwa Barani Afrika katika kutekeleza na kuendeleza malengo ya Umoja wa Mataifa. Hususani amani na usalama Duniani.
     Aidha Ban Ki Moon, ameonyesha imani kubwa kwa mwakilishi huyo wa Tanzania huku akimpongeza kwa nafasi za ubalozi alizoshika nchini Kanada na Marekani kabla ya wadhifa wake huo mpya.
     Akamtaka kuendeleza msimamo wa Tanzania wa kuwa nchi kiongozi katika Afrika na ndani ya Umoja wa Mataifa kwa kudumisha na kuendeleza malengo yenye maslahi kwa Serikali ya Tanzania, Bara la Afrika na Umoja wa Mataifa kwa ujumla.
     Ban Ki Moon akatumia pia nafasi hiyo kutoa shukrani zake, kwa mtangulizi wa Balozi Sefue, Balozi Augustine Mahinga ambaye katibu Mkuu alimteua kuwa mwakilishi wake maalum huko Somalia.
    Katibu Mkuu akabainisha kuwa kutokana na heshima kubwa ambayo Tanzania imejijengea ndani ya Umoja wa Mataifa, anaitegemea Tanzania katika kuwasiliana na mataifa mengine hasa yale yanayoendelea.
    “Tanzania mmejijengea heshima kubwa ndani ya Umoja wa Mataifa, kwa hiyo usitegemee kuwa utakuwa unaisemea Tanzania peke yake, bali na mataifa mengine pia, na hilo ndio tegemeo langu kubwa kutoka kwako Mhe. Balozi” akasisitiza Ban Ki Moon.
     Katika mazungumzo hayo, Katibu Mkuu amemhakikishia Mwakilishi huyo wa Tanzania ushirikiano kutoka kwake yeye binafsi na sekretariati ya Umoja wa Mataifa.
     Kwa upande wake, Balozi Ombeni Sefue amemwahidi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kwamba atafanya juhudi zote kuendeleza maslahi ya Tanzania katika UN, kudumisha ushirikiano mzuri kati ya UN na Tanzania, na kuchangia katika kuendelelezaji wa majukumu na malengo ya Umoja wa Mataifa.
     Akatumia nafasi hiyo Kumpongeza Katibu Mkuu kwa kusimamia vema utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia, huku akimwomba aendelee kuzihimiza na kuziomba nchini zenye uwezo mkubwa kiuchumi ziendelee kuzisaidia nchi zisizokuuwa na uwezo ili ziweze kutekeleza Malengo ya Maendeleo ya Millenia.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages