Breaking News

Your Ad Spot

Sep 18, 2010

WAZIRI MKUU AENDA MAREKANI KWENYE MKUTANO WA MALENGO YA MILENIA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 18.09.10

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameondoka nchini jana jioni (Ijumaa, Septemba 17, 2010) kwenda New York, Marekani kuhudhuria mkutano wa siku tatu wa Wakuu wa Nchi na Serikali utakaofanya tathmini ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia (MDGs).
Waziri Mkuu anakwenda kuhudhuria mkutano huo utakaoanza Jumatatu, Septemba 20, 2010 kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete ambaye yuko kwenye ziara mikoani akifanya kampeni kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu.

Waziri Mkuu amepewa fursa ya kuhutubia mkutano huo wa Malengo ya Milenia (Jumatatu mchana) na pia atahutubia kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN General Assembly) mnamo Septemba 27, 2010.
Mkutano huo Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Malengo ya Milenia (Summit on the Millennium Development Goals) umeitishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Ban Ki Moon ikiwa ni miaka 10 tangu kufanyika kwa mkutano uliopitisha malengo hayo, Septemba 2000.

Mkutano huu unafanyika sasa ikiwa ni miaka 10 kamili tangu walipokutana Wakuu wa Nchi na kutafakari kwa kina njia muafaka za kuharakisha maendeleo ya binadamu hasa wale wanaoishi katika nchi zinazoendelea. Viongozi hao walijiwekea malengo manane ambayo waliamini kwamba endapo yangetekelezwa, yangeweza kupunguza umaskini unaowakabili mamilioni ya watu na kuboresha maisha yao.

Vilevile, Bw. Ban Ki Moon amekaririwa akisema kwamba mkutano huo unafanyika wakati muafaka ikizingatiwa kuwa imebakia miaka mitano kufikia mwaka 2015 ambao viongozi hao walijiwekea mkakati malengo hayo yawe yametimia ifikapo mwaka huo.

Mkutano wa Umoja wa Mataifa ulioweka Malengo ya Milenia mwaka 2000 uliazimia kuondoa umaskini, njaa, maradhi, na kupunguza vifo vya akinamama na watoto ifikapo mwaka 2015. Pia uliweka malengo ya kudumisha hifadhi ya mazingira kwa maendeleo endelevu na kujenga utawala bora ili kuleta mshikamano wa kimaendeleo duniani.
Ends

IMETOLEWA NA OFISI YA WAZIRI MKUU
DAR ES SALAAM

18.09.2010
Irene K. Bwire,
Cell:+255-784-365-214,

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages