Breaking News

Your Ad Spot

Oct 27, 2010

UVCCM TAIFA, WAMPIGA TAFU MWENYEKITI WAO WA ZAMANI MASAUNI HAMADI MASAUNI KATIKA KAMPENI ZA KUWANIA UBUNGE, WAMPA SH. MILIONI MOJA

Na Richard Mwaikenda, Zanzibar
Hamad Masauni Yusufu, ambaye ni baba mzazi wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Masauni  Hamad Masauni, amempongeza Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la umoja huo, Ridhiwani Kikwete kwa kitendo cha kwenda kumpa nguvu mwanawe anayegombea ubunge Jimbo la Kikwajuni, Zanzibar.

Mzee Masauni alitoa pongezi hizo kwa Ridhiwani aliyemtembelea nyumbani kwake, baada kushiriki kikamilifu katika mkutano wa kampeni za kumnadi mwanawe juzi katika Jimboni humo.

Ridhiwani ambaye katika ziara hiyo ameambatana na kikosi kazi cha vijana makada wa UVCCM, baada ya
kumaliza mkutano huo wa kampeni, waliongozana na mgombea hadi nyumbani kwa Mzee Masauni ambapo
walilakiwa vizuri na kukaribishwa ndani.

Baada ya utambulisho, Ridhiwani alimkabidhi mgombea Masauni, sh. 1,000,000 zilizotolewa na UVCCM Taifa,
za kumsaidia katika kampeni hizo. makabidhiano hayo yalishuhudiwa pia na Mzee Masauni.

Mzee Masauni ambaye ni Mwenyekiti wa zamani wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), alimshukuru
Ridhiwani pamoja na UVCCM, kwa kitendo walichofanya cha kumuunga mkono mwenzao katika kampeni hizo.

Alisema kuwa kitendo hicho kinampa faraja,pia kinampa nguvu mwanawe katika harakati za kampeni za kuwania
ubunge katika jimbo hilo.
Akihutubia katika mkutano wa kampeni,Ridhiwani alimnadi mgombea huyo kwa kummwagia sifa lukuki za
utendaji wake alipokuwa Mwenyekiti wa UVCCM Taifa. "Mchagueni Masauni kwani ni kijana mwenye uwezo,
mwadilifu na muajibikaji tena bado anahitajika na chama ili asaidie katika utekelezaji wa Ilani ya chama,"alisema Ridhiwani.

"Masauni tunamkumbuka kwa mambo mengi aliyoyafanya akiwa Mwenyekiti wa UVCCM, aliufanya umoja huo upate magari yaliyogawiwa kila mkoa, pikipiki moja kila wilaya pamoja na baiskeli moja kwa kila Kata chini,"alisema.

Mgombea huyo, alitoa shukrani nyingi kwa Ridhiwani na jopo lake pamoja na UVCCM,kwa uamuzi wao wa kwenda Zanzibar kumpa nguvu katika kampeni.Pia alimpongeza kwa kazi kubwa ya kukikampenia chama aliyoifanya katika mikoa ya kusini na Nyanda za Juu Kusini.

"Nakupongeza wewe na jopo lako kwa kuonesha mshikamano wa hali ya juu wakati wa kampeni za kukitakia chama ushindi wa kishindo mlizzoifanya katika mikoa mbalimbali nchini," alisema Ridhiwani.

Alisema kuwa Ridhiwani, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi ya UVCCM Taifa, amefanya kazi kubwa ya kuhakikisha umoja huo unakuwa na vitegauchumi vikubwa,Makao Makuu ya UVCCM Dar es Salaam, ujenzi wa jengo la ghorofa 27 unaendelea na kwa upande wa Zanzibar tayari mchakato wa mradi
mkubwa unaendelea.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages